Vianzio vya mageuzi katika muhula ujao vinapoanza kujitokeza

Na Michael Eneza:
MOJA ya maeneo ambayo hayatabiriki katika mfumo wowote wa siasa ni
kutambua mabadiliko yatakuja kwa kupitia mlango gani, na kwa maana
hiyo, yakiwa yameandaliwa na kundi gani katika jamii – au mwisho,
yachukue jina gani, yakitaka nini cha msingi. Katika nchi tofauti
kumekuwa na kila aina ya mapinduzi, yafikie demokrasia au yaingie
katika utawala wa kiimla, au yashindwe kufikia mageuzi na mpangilio wa
awali urudi, au uendelee na watu wengine. Ni kama ilivyo katika nchi
kama Nigeria, iingie mfumo wa vingi, upinduliwe, lirudi jeshi,
liondoke madarakani, urudi mfumo wa awali, uliojaa rushwa.
Licha ya kuwa kuna kila dalili kuwa chama tawala nchini kinaungwa
mkono na idadi kubwa zaidi ya wapiga kura, kiasi ambacho wagombea wa
upinzani wameshindwa kuweka wagombea karibu kwa nusu ya majimbo, kuna
pengo kubwa kati ya hitaji la mageuzi katika hali za maisha ya watu na
kiwango cha kuungwa mkono na wapiga kura. Na kama ilivyokuwa nchini
Nigeria mwisho wa mwaka 1983, au hapa nchini mwisho wa mwaka 1982
ambako uasi ulikuwa unaiva jeshini kuhusiana na hali ya uchumi, bado
kuna mivutano inayokuja. Wakati ule ilikuwa ni kuchoshwa na kukosekana
vitu madukani, sasa ni hali ya maisha ambayo haiendani na matazamio ya
wananchi walio wengi, na kutoaminika kwa maadili ya CCM.
Ndicho kinachoweza kufanikisha kujipanga kwa makundi kadhaa, au kundi
la msingi ambalo lina uwezo wa kubadili kile kinachosemwa na
kukubalika – kama ilivyokuwa kwa ‘Kundi la 55’ kudai iundwe serikali
ya Tanganyika ndani ya Muungano, au mwaka jana, ‘makamanda wa vita
dhidi ya ufisadi.’ Na siyo tu makundi ya siasa ambayo yameweza
kuchangia kubadilisha sheria, au kuhitaji mabadiliko ya aina moja au
nyingine yafanyike, na kwa upande fulani, wao wenyewe kufanya
mabadiliko kama hayo. Kwa mfano mwaka 1998 ilikuwa ni chama cha
waandishi wa habari wanawake TAMWA ambacho kilisukuma Bunge kukubali
muswada kuhusu ‘ubakaji.’ Uliweka mazingira ya kulazimisha hatia mtu
akishtakiwa kwa hilo.
Kuna wakati enzi za ukoloni ambako wanaume eneo la Same walikamatwa
kutokana na kutolipa ‘kodi ya kichwa’ na walipokuwa rumande wake zao
wakaandamana hadi kwa DC kutaka kuwe na mabadiliko, wakatoa maneno
ambayo yalimstua DC akajua kuwa hapa siyo tu suala la sheria.
Ilisaidia ‘kupindisha’ maamuzi na watu wake wakaachiwa, utaratibu wa
kodi ukabadilishwa ili usiwe kero kupita kiasi. Ni mwaka jana tu
ambako Kanisa Katoliki lilitoa rasimu ya ‘vipaumbele’ vinavyofaa
kuzingatiwa katika kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu, na siyo rahisi
kusema Bunge likirudi ni ‘zamu’ ya nani kutoa rasimu, kwa maana ya
kuingiza changamoto ya kufanyiwa kazi, iwe ni hapo bungeni au katika
jamii kwa jumla.
Eneo lingine ambalo inabidi liangaliwe kama kianzio cha fikra ni
makundi ya jamii ambayo yanakuwa na miingiliano na jamii kwa jumla, na
wanaweza kufikia makubaliano ambayo hayajafikiwa na Bunge, kwa mfano
wahitaji mikopo na mabenki. Pale mtu anapoomba fedha anapewa masharti,
na licha ya kuwa ziko sheria za jumla za kuundwa kwa mabenki na
usalama wa fedha zinazoingizwa, yako maeneo ya masharti ambayo
yanaambatana na kanuni tu za jamii, na hizo zikibadilishwa, mabenki
nayo yanakuwa huru kutoa mikopo kwa kanuni nyingine. Suala ni kuwa
hivi sasa kuna msukumo mkubwa wa kujua jinsi makundi tofauti ya jamii
yatakavyoweza kupata fedha kufikia ndoto zao; yanaona mabenki
‘hayasaidii.’
Ukiangalia suala hilo kwa karibu, unakuta kuwa tatizo kuu la kufikiwa
ndoto za watu katika jamii ni ufinyu wa soko hata kama wanazalisha
bidhaa, ufinyu wa ajira hata kama wanajiendeleza, na ufinyu wa uwezo
wa kununua vitu hata kama wana ajira, ambayo ina msingi wake katika
mfumo wa umiliki mali kwa jumla na ardhi ikiwa ‘nambari wani.’
Akitokea mtu anahitaji kuchimba madini eneo fulani, mkazi wa pale
analipwa miti na nyumba kama ipo; halipwi thamani ya ardhi kwa vile
siyo yake, na anayenunua pia haoni sababu ya kuendeleza eneo hilo kwa
sababu siyo mali yake. Linaweza kutwaliwa serikali ikilihitaji, au
inapoamua tu kuwa siyo vyema kwa mtu huyo kushika eneo hilo, hana
‘usalama’ wa milki aliyonunua.
Bila kurudi katika ‘mjadala mduara’ wa kama sera zimetekelezwa katika
miaka mitano iliyopita, suala la msingi ni kuwa mali isiyohamishika
kutokuwa binafsi kunazuia miingiliano muafaka inayoleta kukua kwa
uchumi na ‘utajiri’ wa watu. Ni uelewa ambao ulizuiwa usikue katika
hisia za watu na Azimio la Arusha tangu mwaka 1967, hivyo makundi ya
watu sasa yanafurika kupiga kelele kuwa tatizo ni ‘utawala bora,’
wakati utawala bora wenyewe unatokana na mahusiano muafaka – pale
ambapo kila mtu analinda mali yake. Tanzania imejaa utapeli kwa sababu
watawala na wataalamu kila mahali, na wazungumzaji wa kuagizwa au
kulipwa, wanajifanya kutetea maslahi ya nchi; hawathubutu kusema
wanayo maslahi kwa jambo fulani. Itabidi lipatikane kundi la jamii
liamue kuwa mali isiyohamishika iwe binafsi, ili tujikwamue; kutokana
na sababu za kihistoria, ni maimamu tu kwa mtindo wa ‘sharia banking,’
walio na hisia hitajika.
(mwisho)