Taifa Msibani, Umoja wetu na Utu wetu shakani

Na Zitto Kabwe:
(Nimeandika makala haya nikiwa katika Benchi la Hospitali ya Mnazi Mmoja
hapa Zanzibar. Mniwie radhi kama kuna spelling mistakes kwani nilitaka hisia
zangu ziwe as raw as possible -Zitto Zitto and not Zitto a politician).
Jana asubuhi tarehe 10 Septemba 2011 Taifa liligubikwa na habari za
kushtusha za maafa. Mwanzoni taarifa zilisambaa kwamba zaidi ya watu 2000
walikuwa kwenye Boti MV Spice Islander lililopinduka na kuzama mbele kidogo
ya Nungwi likielekea kisiwani Pemba.
Habari hazikuwa za uhakika sana kwani vyombo vyetu vya habari na hasa
Televeshini ya Taifa havikuwa vikitoa habari juu ya ajali hii. Habari
zilisambaa kupitia mitandao ya intaneti na kufuatia uchu wa habari
nilianzisha #ZanzibarBoatAccident katika mtandao wa twitter ili tuweze
kufuatilia kwa karibu habari zote za ajali hii.
Habari zilisambaa kuwa Televisheni ya Taifa ilikuwa inaonyesha muziki wa
Taarab na Baadaye vipindi vingine vya kawaida bila kutoa habari kwa Umma
kuhusu msiba huu.
Watanzania waliokoa wakiwasiliana kupitia twitter na facebook walikuwa na
hasira sana na kituo cha TBC1 kutoonyesha au kupasha habari juu ya ajali
hii. Mpaka saa moja jioni kituo hiki cha Televisheni ya Taifa kilikuwa
kinaonyesha watu wakicheza muziki wa Kongo, wanawake wakikatika viuno na
hata ngoma za asili. ‘Hallo, washa TBC1 uone Televisheni yenu inachoonyesha’
yalikuwa ni maneno ya Mwakilishi Ismael Jussa Ladhu aliponipigia kuonyesha
kusikitishwa kwake na kituo hiki.
Mpaka jioni tulikuwa tumepata taarifa kuwa Watanzania wenzetu 198 walikuwa
wamepoteza maisha. 570 hivi walikuwa wameokolewa. Binafsi nilipotembelea
Hospitali ya Mnazi Mmoja niliweza kumwona Binti aliyeitwa Leyla, akisoma
darasa la Nne huko kisiwani Pemba. Leyla alipona, aliokolewa. Nilimwambia
leyla atapona na kurudi Shuleni. Mpaka ninapoandika tumeambiwa kuwa
Watanzania 240 wamegundulika kupoteza maisha na zaidi ya 600 wameokolewa.
Napenda kuwapongeza sana waokoaji wetu, wavuvi wa kijiji cha Nungwi na
vijiji jirani, wamiliki wa mahoteli waliojitolea vifaa vyao kwenda kuokoa
watu na wanajeshi wetu wa majeshi ya ulinzi na usalama kwa kazi hii kubwa ya
kuokoa. Kwa kweli tumeokoa watu wengi kuliko ilivyotarajiwa. Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar imejitahidi sana, ilitulia na kuonyesha uongozi dhabiti
katika juhudi za uokoaji.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akafuta ziara yake huko Canada,
ziara iliyokuwa imeandaliwa muda mrefu na kwa gharama. Lakini Rais aliona ni
vema kupata hasara kuliko kuwa nje ya Nchi kipindi hiki. Hakutaka hata
kumtuma Makamu wa Rais au Waziri Mkuu. Alifuta. Akatangaza siku 3 za
kuomboleza. Hata hivyo waandaaji wa Miss Tanzania waliona hasara kubwa
kuahirisha shindano la Urembo usiku huo. Wangepata hasara! Hata wafadhili
wao Kampuni ya simu za mkononi ya vodacom ambao miongoni mwa waliofariki
wamo wateja wa vodacom, waliendelea na shindano hili. Jumatatu, tarehe 12
Septemba 2011 ni siku ya khitma ya kuwaombea marehemu wetu. Nimeamua
kutotumia simu ya ngu ya Voda kwa siku nzima, sina njia ya kuiadhibu Kampuni
hii isipokuwa kugoma kutumia simu yao japo kwa siku moja kuonyesha
kutoridhishwa kwangu na uamuzi wao wa kutojali msiba huu kwa Taifa.
Misiba huweka jamii pamoja. Msiba huu uliotokea Zanzibar ni jaribio kubwa
kwa Umoja wa Taifa letu. Shirika la Utangazaji la Taifa limeshindwa jaribio
hili la kudhihirisha Umoja wetu katika kipindi hiki. Nataraji wakubwa wa
Shirika hili linaloendeshwa kwa kodi watawajibika au kuwajibishwa!
Jumla ya Majeruhi na marehemu sasa inafikia zaidi ya Abiria 800! Asubuhi ya
jana 10 Septemba 2011 tuliambiwa na Serikali kwamba uwezo wa Boti la MV
Spice Islander ilikuwa ni abiria 500 na wafanyakazi 12. Pia tumejulishwa
kuwa boti hili lilikuwa la Mizigo na sio la Abiria. Natumai mara baada ya
kumaliza maombolezo haya ya siku tatu Wakuu wa Mamlaka zinazohusika na
usafiri wa Majini wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar watawajibika au
kuwajibishwa. Mkuu wa Bandari ya Zanzibar Mustafa Aboud Jumbe na Waziri wa
Miundombinu Hamad Masoud wanapaswa kufukuzwa kazi mara moja kama
hawatawajibika wenyewe kwa kujiuzulu.
Kufukuzwa kwao kazi hakutarudisha ndugu zetu duniani bali itakuwa ni somo
kuwa hatutarudia tena kufanya makosa yaliyoleteleza ajali kama hii.
Mwenyezimungu atupe subira wakati huu wa msiba mkubwa katika Taifa letu.
Alaze roho za marehemu wetu mahala pema peponi na awape unafuu wa haraka
majeruhi wetu.

Zitto Kabwe, Mb
Sent from my BlackBerry® smartphone from Vodacom

__._,_.__