TAARIFA RASMI YA TEF KUHUSU MGOMO WA MADAKTARI NCHINI

UTANGULIZI

Mgomo
wa Madaktari ambao umedumu kwa takriban wiki mbili nchini sasa ni dhahiri
kwamba umelitikisa Taifa na kuathiri huduma za tiba katika hosipitali kadhaa
nchini. Mgomo huu ulianza taratibu na kuendelea kukua kutokana na mvutano, pia
vita ya maneno baina ya Serikali na Madaktari.

HALI
ILIVYO SASA

Kutokana na
taarifa zinazofikishwa katika vyumba vya habari, ni dhahiri kwamba hali ni
mbaya sana katika baadhi ya hosipitali nchini hasa Hosipitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) ambapo mgomo huu umesababisha vifo vya watu ambao huenda
wangepona kama wangepata huduma.

Wagonjwa
mahututi wanaofikishwa MNH kwa ajili ya huduma za rufaa hawapokelew,maiti
wanaofikishwa kwa ajili ya kuhifadhiwa chumba cha kuhifadhi maiti
(mortuary), hawapewi hifadhi na badala yake wanarejeshwa walikotoka.

Hata katika hosipitali ambazo madaktari
wameripotiwa kurejea kazini, huduma zinazotolewa ni hafifu hii ikimaanisha
kwamba mgomo bado unaendelea hata kama si kwa madaktari kukutana kwenye
kumbi kama ilivyokuwa mwanzo.

Madaktari
kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao wamepelekwa katika
hosipitali za Serikali kuokoa jahazi, hawatoshelezi lakini katika baadhi
ya maeneo wamepata upinzani kutoka kwa wauguzi wa hosipitali husika.

MAPENDEKEZO

Kutokana
na hali ilivyo sasa, Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari katika kikao cha
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kilichokutana leo Jumanne 31 Januari 2012,
wamesema “Inatosha” kwa na kwamba hali isiachwe ikaendelea na kupendekeza
yafuatayo:

Pande husika
katika mgogoro huu ambazo ni Serikali na Madaktari wakubali kukaa katika
meza moja ya mazungumzo kutafuta mwafaka wa suala hili, wenye lengo la
kupata suluhu ya tatizo lililopo, huku kila upande ukiangalia madhara kwa
binadamu yanayotokana na mgogoro huu.
Majadiliano
yalenge kutatua matatizo ya madaktari kwa upande mmoja, lakini pia
yazingatie uwezo wa Serikali kwa upande mwingine. Nia iwe ni kuwawezesha
madaktari kadri uwezo wa Serikali unavyoruhusu lakini pia kuwaokoa
wagonjwa ambao wanakabiliwa na hatari kubwa kutokana na kukosa tiba.

Madaktari
wakubali kurejea kazini haraka iwezekanavyo ili kuokoa maisha ya watu
ambao wanapoteza maisha kutokana na kukosa huduma za tiba, wakati wagonjwa
wakiwa si sehemu ya mgogoro uliopo.

Serikali ifute
amri zake zote dhidi ya madaktari waliokuwa kwenye mgomo (hasa ile ya
kuwafukuza wasiofika kazini jana Jumatatu Januari 30, 2012) ili kuwezesha
mazungumzo kufanyika baina ya pande hizo mbili.

Baada ya
makubaliano kufikiwa, iwepo kalenda ya utekelezaji wa makubaliano husika
ili kuepusha kutokea kwa mgomo mwingine ambao unaweza kuleta athari kubwa
zaidi kwa wananchi.

Baada ya
maafikiano kuwapo, usiwepo mpango wowote wa wazi au wa kificho wa
kuwaadhibu kwa namna yoyote ile viongozi wa madaktari waliogoma kwani
tunaamini kwamba madai yao yalikuwa halali.

Serikali
kuanzia sasa ifanye mapitio ya mishahara, maslahi na stahili nyingine za
wafanyakazi wote katika sekta ya Umma na kuyaboresha, ili kuepuka kufanya
hivyo kwa shinikizo la migomo inayofanywa na watumishi hao kwa makundi.

HITIMISHO

Wakati
tukiamini kwamba busara itatumika kuliondoa Taifa letu katika mtanziko uliopo,
tuseme wazi kuwa sisi Wahariri tunaamini yafuatayo:

Kwanza
tunatambua umuhimu wa kada ya udaktari kwa umma, hivyo kutambua haki yao
ya kupata mahitaji muhimu. Ikiwa madaktari hawapati mahitaji muhimu, basi
ni dhahiri kwamba hawawezi kutoa huduma kwa wagonjwa ipasavyo.

Pili tunatambua
pia ufinyu wa rasilimali za nchi ambazo pengine ndicho kikwazo kwa
Serikali kushindwa kuwalipa watumishi wake vizuri au kadri ya madai yao,
licha ya kwamba wawakilishi kama wabunge wamepewa nyongeza ya posho za
vikao kwa viwango ambavyo vimezua manung’uniko kutoka kwa umma.

Lakini tofauti
zozote zilizopo, ziwe za kiutendaji au kiutawala kamwe haziwezi kuondolewa
bila pande husika kukubali kukaa na kuzijadili ili kupata mwafaka kwa
faida ya Watanzani wote.

Ni
matumaini yetu kwamba busara zitatumika ili kuwaokoa Watanzania.

Neville
Meena

KATIBU
WA JUKWAA LA WAHARIRI (TEF)