SERIKALI KUCHIMBA MABWAWA YA MAJI WILAYANI MASASI.

(Na Veronica Kazimoto – MAELEZO)
Dodoma
31Julai, 2012.
Serikali kupitia Halimashauri ya Masasi imeazimia kuchimba mabwawa ya
maji kwa matumizi ya binadamu na tayari kibali kimeombwa Wizara ya
Maji ili kutumia fedha za Program ya Maji na Usafi wa Mazingira
Vijiji.
Akijibu swali kwa niaba ya Waziri Mkuu bungeni leo,Naibu Waziri, Ofisi
ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Majaliwa
Kassim Majaliwa amesema baada ya kupata kibali hicho, mabwawa ya maji
yatachimbwa mara moja ili kusaidia upatikanaji wa maji katika
Halimashauri hiyo.
“kutokana na visima vinavyochimbwa katika halimashauri hiyo kupata
maji yasiyotosheleza mahitaji, Halimashauri ya masasi imeridhia
pendekezo la kuchimba mabwawa ya maji kwa matumizi ya binadamu,”
amesema Majaliwa.
Mabwawa hayo yatachimbwa katika vijiji vya Nambawala, Namatuwe,
Chingukungulu na Sululu. Vijiji vingine ni pamoja na Mbonde, Matawale
na Chakama.
Majaliwa amesisitiza kuwa katika mwaka wa fedha wa 2011/2012
Halimashauri ya Masasi imepokea jumla ya shilingi milioni 941 kwa
ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji katika vijiji vya Mihima,
Nambawala, Mraushi, Lilala na Mtakuja ambavyo vimechimbwa visima na
kupata maji ya kutosha.
Kutokana na maji hayo kutotosheleza mahitaji katika maeneo mengine,
Halimshauri hiyo imetengewa jumla ya shilingi milioni 195 kwa mwaka wa
2012/2013 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mingine ya maji.
Upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Halimashauri ya
Wilaya Masasi ni asilimia 45 ya wakazi wote na huduma hii inapatikana
kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vikiwemo visima vifupi 7, visima
vilefu 12, miradi ya maji bomba 2 na mabwawa manne.
MWISHO.