Maliasili na Tamisemi KUSHIRIKIANA KUBORESHA UKUSANYAJI WA MADUHULI YATOKANAYO NA MISITU

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIAWIZARA YA MALIASILI NA UTALIITAARIFA KWA UMMA: Dar es Salaam, 13, April 2012:
Wizara ya Maliasili na Utalii na TAMISEMIzimeazimia kushirikiana kwa karibu zaidi katika masuala ya kukusanya maduhuli ya Serikali yanayotokana na mazao ya misitu. Ili ukusanyaji ufanikiwe Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Tanzania Forest Service – TFS) imetakiwa kuziwezesha Halamashauri za Wilaya kwa kuzipatia fedha na vitendea kazi muhimu, kama usafiri. Hayo yaliazimiwa katika Mkutano wa siku mbili kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na TAMISEMI uliomalizika tarehe 12/4/2012 mjini Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa Mtakatifu Gaspar. Mkutano huo ulihudhuriwa na Watendaji wakuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya, Maafisa Maliasili wa Mikoa, na Maafisa Misitu Wilaya wilaya 59 za mikoa 19 iliyoalikwa. Katika mkutano huo wajumbe walifikia jumla ya maazimio 7 ambayo yalilenga katika kuimarisha ukusanyaji maduhuli bila kuathiri uhifadhi endelevu wa misitu. Wajumbe kutoka pande zote walikubaliana kuimarisha vituo vilivyopo vya ukaguzi wa mazao ya misitu na kuanzisha vingine vipya katika sehemu mbalimbali muhimu. Kufanya hivyo kutasaidia udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu ndani na nje ya nchi. Hata hivyo wajumbe walibaini changamoto mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa watumishi. Ili kutatua uhaba huo mkutano uliazimia kuwa itajengwa hoja ya pamoja kati ya TFS na Halmashauri za Wilaya ambayo itapelekwa Serikalini ili kibali kitolwe cha kuajiri watumishi, ikiwezekana moja kwa moja kutoka vyuoni. Katika mkutano huo wajumbe walisisitiza kupunguza matumizi ya mkaa kama chanzo kukubwa cha nishati hapa nchini. Walisema mkaa unachangia kwa kiasi kikubwa katika kuharibu misitu na mazingira kwa ujumla. Hivyo mkutano uliazimia kuwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS iandae mikakati ya kuhimiza matumizi ya nishati mbadala ya kuendelea kutumia mkaa. Aidha, mkutano ulizungumzia kasi ndogo ya upandaji miti nchini na kuazimia kuwa Mfuko wa Misitu Tanzania (TFF) uweke mikakati ya kufadhili shughuli za kupanda miti. Ili kuimarisha mfuko huo iliazimiwa pia kuwa mfuko uweke mikakati ya kuutunisha. Akufunga mkutano huo Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Bw A. J. Kidata aliwataka wajumbe kujiwekea mkakati wa kutekeleza kikamilifu maazimio ya mkutano huo. Alisisitiza kuwa sharti kila mmoja ajitume na kutambua kuwa mafanikio ya uhifadhi na matumizi mazuri ya misitu yanamtegeme mchango wake. Mafanikio ya utekelezaji wa maazimio hayo itakuwa ni mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira, kukuza uchumi na kupunguza umaskini. Jumla ya wajumbe 200 kutoka Halmashauri za Wilaya, Sekretarieti za Mikoa, TAMISEMI na Wizara ya Maliasili na Utalii walihudhuria mkutano huo uliojadili namna ya kuboresha ukusanyaji wa Maduhuli ya serikali kutokana na mazao ya misitu. Mwenyekiti wa Mkutano huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Nuru Millao.Mikoa iliyohudhuria na Wilaya husika katika mabano ni kama ifuatavyo: 1. Mkoa wa Pwani: (Wilaya za Kisarawe, Mkuranga, Rufiji, Bagamoyo);2. Mkoa wa Lindi: (Wilaya za Lindi, Nachingwea, Ruangwa, Kilwa na Liwale);3. Mkoa wa Mtwara 🙁 Wilaya za Mtwara, Namtumbo, Msasi, na Newala);4. Mkoa wa Ruvuma: (Wilaya za Tunduru na Songea);5. Mkoa wa Rukwa: (Wilaya za Rukwa, Nkasi na Mpanda);6. Mkoa wa Mbeya: (Wilaya za Chunya, Mbeya Vijijini na Mbarali);7. Mkoa wa Iringa: (Wilaya za Mufindi na Kilolo);8. Mkoa wa Kigoma : (Wilaya za Kigoma, Kasulu na Kibondo);9. Mkoa wa Kagera: (Wilaya za Ngara, Biharamlo, Chato, Muleba, Karagwe na Misenye);10. Mkoa wa Mwanza : (Wilaya za Geita, Ukerewe na Sengerema);11. Mkoa wa Tanga: (Wilaya za Handeni, Muheza, Korogwe, Kilindi, Pangani na Mkinga);12. Mkoa wa Kilimanjaro: (Wilaya ya Same);13. Mkoa wa Manyara: (Wilaya za Kiteto, Hanang, Babati na Mbulu);14. Mkoa wa Singida: (Wilaya ya Manyoni);15. Mkoa wa Dodoma : (Wilaya ya Kondoa);16. Mkoa wa Morogoro: (Wilaya za Kilombero, Mahenge, Morogoro, na Mvomero);17. Mkoa wa Shinyanga: (Wilaya za Bukombe na Kahama);18. Mkoa wa Mara: (Wilaya za Serengeti na Tarime);19. Mkoa wa Tabora: (Wilaya za Urambo, Uyui na Sikonge).{MWISHO} George MatikoMSEMAJIWIZARA YA MALIASILI NA UTALII13/4/2012