HOTUBA YA RAIS KWENYE UZINDUZI WA MATOKEO YA AWALI YA SENSA 2012

HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
KWENYE UZINDUZI WA MATOKEO YA AWALI YA
SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2012,
VIWANJA VYA MNAZI MMOJA, DAR ES SALAAM
TAREHE 31 DESEMBA, 2012

Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Balozi Seif Idd, Makamu wa Pili wa
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Viongozi na watendaji wakuu wa Serikali;
Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Jamii; Wanahabari;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;

Nashukuru kwa kunialika kuja kushiriki kwenye tukio hili muhimu na la
kihistoria la kutangaza matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi ya
Mwaka 2012. Haya ni matokeo ya kazi ya kuhesabu watu iliyofanyika kwa
siku 14 kuanzia tarehe 26 Agosti, 2012 hadi 4 Septemba, 2012.
Ndugu wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa wale wote
waliofanikisha zoezi la kuhesabu watu na wale waliokamilisha uchambuzi
unaotuwezesha leo kutangaza idadi ya Watanzania ilivyo sasa. Kwanza
kabisa napenda kutambua Kamati ya Taifa ya Sensa iliyoongozwa na
Mheshimiwa Mizengo Peter Kayanza Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania akiwa na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idi, Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa Mwenyekiti upande wa Zanzibar.
Nawashukuru kwa uongozi wao mzuri ambao matunda yake ndiyo haya
yanayotukusanya leo. Pia nawashukuru wajumbe wa Kamati za Sensa za
Mikoa na Wilaya nchini.
Pili, napenda kuwatambua viongozi na wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu ya Jamhuri ya Muungano chini ya uongozi wa Mama Albina Chuwa
na wenzao wa Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar chini ya uongozi wa
Ndugu Mohammed Hafidh Rajab. Nawapongeza kwa umahiri wao katika
kuongoza, kuratibu na kisimamia utekelezaji wa jukumu lenyewe la
kuhesabu watu. Ni wao kuliko mtu mwingine ye yote ndiyo
waliokabidhiwa kazi ngumu ya kutengeneza mipango na taratibu za
kufanya zoezi lenyewe. Walitayarisha madodoso, kuyachapisha,
kuyasambaza, kuteua watu wa kuhesabu watu na wasimamizi wao.
Waliwafundisha wajibu wao na kuwasimamia katika utekelezaji wao. Ni
wao pia waliohakikisha kuwa madodoso yote yanakusanywa na uchambuzi
unafanywa mpaka sasa tuko tayari kutangaza matokeo.
Nawatambua na kuwashukuru makarani wa sensa waliopita nyumba kwa
nyumba kuhesabu watu na kukusanya taarifa mbalimbali kwa mujibu wa
madodoso waliyokuwa nayo. Tunatoa shukrani na pongezi maalum kwao kwa
sababu ni wao hasa waliowezesha kupatikana taarifa itakayotangazwa leo
na nyingine zitakazofuatia siku za usoni. Kama si wao
tusingekusanyika hapa leo. Nawapongeza kwa umakini wao na moyo wao
wa uvumilivu na uzalendo. Haikuwa kazi rahisi kwa ukubwa wa kazi
yenyewe. Pia, walikumbana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na
baadhi ya maeneo kuwa na mazingira magumu ya kufanyia kazi kama vile
ya usafiri. Lakini pia kulikuwa na ugumu wa kupata taarifa kutoka kwa
wanaoulizwa. Baadhi hawakutoa ushirikiano unaotakiwa. Yalikuwepo
pia matatizo ya kupata huduma stahiki za kufanyia kazi na hasa posho.
Nafahamu kuwa wapo bado wanaodai stahili zao. Hazina wamekiri hilo na
kuahidi watalimaliza haraka.
Ndugu wananchi;
Kufanya sensa ni kazi kubwa na ghali sana. Hata hivyo nchi zote
duniani hufanya sensa kwa sababu ya umuhimu wake. Kupitia Sensa,
hupatikana taarifa muhimu za kutumiwa na Serikali kupanga mipango ya
maendeleo ya nchi na jinsi ya kuhudumia wananchi. Taarifa hizo
hutumika na wadau mbalimbali katika shughuli zao za kuwahudumia
wanadamu. Ndiyo maana madodoso yalikuwa na mambo mengi na ndiyo maana
tumeambiwa kuwa taarifa ya leo ni ya mwanzo tu. Zipo taarifa
zitakazofuatia zenye uchambuzi wa mambo mbalimbali. Naomba tuwe na
subira kwa taarifa mbalimbali tunazozitaka, kwani tutazipata wakati
wake utakapofika. Kwa niaba yenu niwaombe wahusika wafanye kila
wawezalo kuhakikisha kuwa taarifa hizo zinapatikana kwa wakati
uliopangwa.
Ndugu Wananchi;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawatambua watu wengine wafuatao: Wa
kwanza ni Hajat Amina Mrisho, Kamishna wa Sensa ambaye tulimkabidhi
jukumu la kutoa uongozi wa kisiasa katika kazi ya kuhesabu watu na
kuwa kiungo kati ya wataalamu na uongozi wa Serikali. Vile vile,
tulimpa kazi ya kusaidia kufikisha ujumbe pande zote ili kuona kuwa
mambo yanakwenda vizuri. Bahati nzuri mwenyewe ni mjuzi wa masuala
ya takwimu. Alitokea huko kabla ya kumchukua na kumleta katika
shughuli za uongozi wa kisiasa. Hivyo, kazi ilikuwa mikononi kwa
mwenyewe. Namshukuru kwa kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa. Anao
mchango mkubwa katika mafanikio haya. Wa pili ni wananchi wa
Tanzania. Nawashukuru kwa ushirikiano wao. Kabla na wakati wa Sensa,
kulikuwa na purukushani na maneno mengi ya upotoshaji na kutishia
kuvuruga zoezi lenyewe. Wapo wenzetu walioamua kuendesha kampeni ya
kutaka watu wasusie. Wapo walioamua kufanya maandamano na mikutano ya
siasa wakati huo na jitihada zote za kuwasihi wasubiri siku 14 zipite
walizipuuza. Wakati mwingine unashindwa kuelewa baadhi yetu tuna
dhamira gani katika kujihusisha na shughuli za siasa? Hivi inakuwaje
washindwe kutambua umuhimu wa kuhakikisha jambo kubwa kama hili
linafanikiwa? Hivi zoezi la sensa lisipofanikiwa kiongozi wa siasa au
wa dini unanufaika nini? Ndiyo maana nawashukuru sana wananchi kwa
ushirikiano wao uliofanya njama za kuvuruga zoezi kushindwa.
Ndugu wananchi;
Wa tatu ni Wajumbe wa Kamati za Sensa za Mikoa na Wilaya kwa
kufanikisha zoezi la Sensa katika Mikoa na Wilaya zao. Nawashukuru
Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote nchini kwa uongozi wao mzuri. Wa nne ni
viongozi wa kijamii wakiwemo wa vyama vya siasa, madhehebu ya dini na
wa kimila waliosimama kidete kuhamasisha wafuasi wao kushiriki katika
zoezi la Sensa ya Watu na Makazi. Tunawashukuru kwa mchango wao
muhimu. Wa tano ni wamiliki wa vyombo vya habari na wana habari.
Nawashukuru kwa kufanya kazi kubwa na nzuri ya kuhamasisha na
kuelimisha jamii katika kipindi chote cha utekelezaji wa zoezi la
Sensa. Wito wangu kwenu ni kwamba, endeleeni kuelimisha na
kuhamasisha matumizi ya taarifa za Sensa kwa maendeleo ya taifa letu.
Wa mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, nawashukuru sana washirika wetu wa
maendeleo wakiwemo UNFPA, DFID, JICA, CIDA na Benki ya Dunia kwa
mchango na msaada wao mkubwa. Nawashukuru Wenzetu hawa wametupa
ushirikiano mkubwa uliotuwezesha kufanikisha zoezi la Sensa hadi
kufikia hatua hii ya sasa ya kutoa matokeo ya awali. Naomba washirika
wetu wa maendeleo waendelee kushirikiana nasi kukamilisha kazi hii na
pia katika kuimarisha sekta ya takwimu nchini.
Ndugu wananchi;
Baada ya kusema maneno hayo sasa nipo tayari kuzindua rasmi matokeo ya
awali ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Kwa heshima na
unyeyekevu mkubwa natangaza kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi
iliyofanyika kwa siku 14 kuanzia Agosti 26, 2012, Tanzania ina watu
44,929,002 ambapo Tanzania Bara kuna watu 43,625,434 na Zanzibar kuna
watu 1,303,568. Katika Sensa ya tatu ya mwaka 2002 tulikuwa milioni
34.4 hivyo tumeongezeka kwa watu milioni 10.5 ongezeko ambalo ni sawa
na asilimia 2.6 kwa mwaka. Naomba taarifa hizi zitumike kwa madhumuni
yaliyokusudiwa ambayo ni kuboresha maisha ya kila Mtanzania.
Ndugu Zangu;
Hii ni Sensa ya nne kufanyika nchini tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania mwaka 1964. Sensa ya kwanza ilifanyika mwaka
1967 ambapo nchi yetu ilikuwa na watu 12,313,054. Tanzania Bara
ilikuwa na watu 11,958,654 na Zanzibar watu 354,400. Kwa maana hiyo,
katika miaka 45 tangu Sensa ya kwanza na hii, Watanzania wameongezeka
kwa watu milioni 33.
Ndugu Wananchi;
Kama kasi ya ongezeko la watu la asilimia 2.6 halitapungua ifikapo
mwaka 2016 nchi yetu itakuwa na watu milioni 51.6. Inawezekana idadi
hiyo ikaonekana kuwa siyo tatizo la kuumiza kichwa kwa nchi kubwa kama
yetu, lakini ni mzigo mkubwa kwa taifa, jamii na uchumi kuwahudumia.
Inabidi pawepo na mikakati madhubuti na ionekane katika mipango ya
maendeleo kuanzia sasa jinsi ya kuhudumia watu hao 51.6 na zaidi ya
hao miaka inayofuata. Kwa familia, lazima tutambue umuhimu wa kupanga
uzazi, vinginevyo hali ya maisha itashuka sana. Kwa ujumla hatuna
budi kufanya kazi kwa bidii zaidi na nguvu zaidi.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.