HOTUBA YA RAIS KIKWETE DODOMA, TAREHE 30 AGOSTI, 2011

HOTUBA YA MH. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, KWENYE BARAZA LA EID-EL-FITR, DODOMA, TAREHE 30 AGOSTI, 2011

Mheshimiwa Sheikh Issa bin Shaaban Simba, Sheikh Mkuu
na Mufti wa Tanzania,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA;
Wajumbe wa Baraza la Ulamaa;
Waheshimiwa Masheikh na Viongozi wa BAKWATA;
Waheshimiwa Viongozi wa Dini wa
Madhehebu Mbalimbali;
Viongozi Wenzangu wa Chama na Serikali;
Ndugu Wananchi; Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana;

Assalaam Ellaykum Warahmattullah Taallah Wabarakatuh!

Eid-Mubarak!!

Nakushukuru sana Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania kwa kunialika
kuja kujumuika nanyi katika siku hii adhimu ya kusherehekea kumalizika kwa
mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Naungana na nawe na Katibu Mkuu wa
BAKWATA Sheikh Suleiman Saidi Lolila kumshukuru Allah Subhana Wataalah kwa
kutuwezesha kufunga na kutimiza moja ya nguzo tano za Uislamu. Inshaalah
tuzidi kumuomba Mola wetu aendelee kutujaalia uhai na uzima ili tuweze
kufunga Ramadhani ijayo na za miaka mingi ijayo.

Mheshimiwa Mufti wa Tanzania;

Naungana nawe pia, kuwapongeza Waislamu wote nchini na duniani kwa kumaliza
salama ibada ya swaumu kwa mwaka huu. Inshaalah tuombe kwa Mwenyezi Mungu
sote tuwe miongoni mwa wale ambao funga zao zitakuwa zimekubaliwa. Aidha,
tuombe tuwe miongoni mwa waja wake ambao toba zao zimetakabiliwa na
kusamehewa madhambi yao na adhabu ya moto.

Napenda nami nijumuike nawe pamoja na , Katibu Mkuu wa BAKWATA na Masheikh
wote nchini kuwaomba na kuwasihi Waislamu wote nchini kwamba, ucha Mungu
tuliouonyesha katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan usiwe umeisha
jana bada ya kuandama kwa mwezi. Badala yake, hauna budi uwe endelevu, kwa
maana ya sisi kuendelea kutenda mema na kuepuka kutenda dhambi na mambo
yanayomchukiza Mwenyezi Mungu. Katu ucha Mungu siyo kwenye kipindi cha Mwezi
mtukufu peke yake.

*Risala *

Mheshimiwa Mufti;

Nawashukuru sana kwa risala yenu iliyowasilishwa vizuri na Katibu Mkuu wa
BAKWATA. Yote mliyosema kuhusu Serikali, nchi yetu, Waislamu na Watanzania
kwa jumla nimeyasikia na kuyaelewa. Napenda kuanza kwa kusema kuwa Serikali
inaunga mkono na inapenda sana kuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu na
mashirika, viongozi na waumini wa dini zote nchini bila ya kubagua wala
kupendelea.

Bila ya shaka mtakubaliana nami kuwa maneno haya niyasemayo leo si mageni
kwako na masikioni mwa Watanzania. Nimeshayasema mara kadhaa siku za nyuma.
Tena haya ni maneno ya dhati na wala siyo ya kuwapaka mafuta kwa mgongo wa
chupa kama msemo wa Kiswahili usemavyo.

Mheshimiwa Mufti;

Serikali ina msimamo huo kwa sababu tunatambua na kuthamini sana nafasi na
mchango wa dini na mashirika ya dini katika maendeleo na ustawi wa jamii na
nchi yetu kwa ujumla. Serikali inaunga mkono mashirika ya dini katika
shughuli zao kwa sababu ya manufaa ya dhahiri ya shughuli hizo kwa taifa
letu. Mashirika ya dini yamekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Serikali
kuwapatia wananchi wa Tanzania huduma muhimu za elimu, afya, maji n.k. Bila
ya ushirikiano, upatikanaji wa huduma hizo kwa baadhi ya maeneo ungekuwa
tofauti sana. Serikali kwa upande wake imekuwa inafanya kazi ya kusaidia
mashirika ya dini yaweze kutoa huduma hizo kwa wananchi.

Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna kitu cho chote ambacho Serikali itatoa
kwa dini moja ambacho dini nyingine itanyimwa. Kwa kweli mbele ya Serikali
dini zote zina haki sawa. Kama hujaomba usimlaumu aliyeomba akapewa au
aliyempa. Kama yupo anayeamini anazo sifa kama mwenzake aliyepewa aombe
naamini atapewa. Iwapo itafanyika vinginevyo dai haki yako kwa mamlaka
zinazohusika.

Mheshimiwa Mufti, Ndugu Zangu Waislamu;

Maelezo yangu haya yanafanana na hoja zenu katika Risala yenu kuhusu Itifaki
ya Maridhiano ya 1992 baina ya Serikali na TEC na CCT. Nafurahi kwamba na
nyie mmeamua kuleta maombi, yaleteni yatashughulikiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Mufti; Ndugu Zangu Waislamu; Watanzania Wenzangu Wote;

Sababu ya pili inayoifanya Serikali kuunga mkono madhehabu ya dini katika
shughuli zao ni kazi kubwa yaifanyayo ya kuwalea Watanzania kuwa wacha
Mungu. Sisi tunaamini kuwa kama madhehebu yatafanikiwa kwa hili nchi yetu
itakuwa mahali pazuri sana pa kuishi. Wacha Mungu ni watu wema, hawatendi
maovu, waaminifu, waadilifu, hawaombi, hawatoi wala kupokea rushwa.
Wacha-Mungu ni watu wenye upendo kwa watu wote na daima hupenda amani,
usalama na utulivu. Kwa sababu hiyo mambo mengi maovu katika jamii na
Serikali yatapungua, watu watahudumiwa ipasavyo na hivyo kuvipunguzia vyombo
vya dola kazi ya kupambana na uovu na uhalifu.

*Uhuru wa Kuabudu *

Sababu ya tatu, Mheshimiwa Mufti, ni kuwa uhuru wa kuabudu unatambuliwa kuwa
moja ya haki za msingi za raia wa Tanzania katika Katiba ya nchi na
unalindwa kisheria. Watanzania wako huru kufuata na kuabudu dini yoyote
waipendayo au kutokukufuata dini yoyote. Tanzania haina dini ya taifa au ya
Serikali ambayo watu wote lazima waifuate. Aidha, hairuhusiwi kisheria
kubeza au kudharau dini au imani ya mtu mwingine na hata nyumba za ibada.
Imefanywa hivyo makusudi kwa nia ya kulinda uhuru wa watu kuabudu na
kudumisha amani katika jamii na nchini. Naamini kama ingekuwa kinyume chake
amani ingeweza kuvunjika.
Mheshimiwa Mufti, Waheshimiwa Masheikh na Watanzania Wenzangu;

Inasikitisha kusikia kuwa wapo viongozi na waumini wa dini zetu nchini
wakipita huku na huko na wakati mwingine wakitumia nyumba za ibada kuhubiri
kejeli dhidi ya dini nyingine. Kukashifiana hujenga chuki na uhasama baina
ya waumini wa dini mbalimbali na kuhatarisha amani na usalama. Hivi viongozi
wangu wa dini, hamuwezi kueneza imani ya dini zenu bila kukashifu dini ya
wenzenu. Kama kweli wewe ni kiongozi wa dini unaetambua wajibu wako
ipasavyo, huwezi kufanya hivyo na wala huhitaji kukumbushwa na Polisi
kutokufanya hivyo. Tafadhali acheni na mamlaka husika acheni ulegevu
kusimamia sheria. Ajizi yenu inaweza kuleta maafa katika taifa. Timizeni
wajibu wenu ipasavyo bila woga wala kuonea au kupendelea.

Pamoja na hayo ni vyema viongozi wa dini zote na madhehebu yote mkafufua na
kuendeleza utaratibu mzuri uliokuwepo siku za nyuma wa mawasiliano baina ya
dini mbalimbali. Itasaidia sana kuzungumzia masuala ya namna hii na hata la
uadui mlilolitaja katika Risala yenu. Nguvu ya dola peke yake si jawabu.

*Hoja za Risala *

Mheshimiwa Mufti; Ndugu Zangu Waislamu,

Katika risala yenu mmezungumza mambo kadhaa mengine na kutoa ushauri mzuri
ambao napenda kuwahakikisha kuwa tutaufanyia kazi. Hata hivyo, niruhusuni
niyazungumzie au kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya mambo.

*Mahujaji *

Mheshimiwa Mufti,

Napenda kukupongeza wewe na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa
kazi kubwa na nzuri muifanyayo kuhusu upelekaji wa mahujaji Makka na Madina
kila mwaka. Ni kweli kabisa kwamba BAKWATA inayo rekodi nzuri ya
kuwasafirisha, kuwahudumia na kuwarejesha salama nyumbani mahujaji. Napenda
kuwatia moyo kuwa muendelee kufanya vizuri zaidi mwaka hadi mwaka ili
BAKWATA iwe chaguo la hiari la Waislamu wanaotaka kwenda kutimiza ibada ya
Hija.

Pamoja na hayo, zipo taarifa za baadhi ya taasisi zinazoshughulikia
upelekaji wa mahujaji kutokufanya vizuri. Matokeo yake mahujaji wamekuwa
hawahudumiwi ipasavyo na safari ya Hija hugeuka kuwa adha badala ya kuwa
furaha shangwe. Je, hamuoni umuhimu wa jambo hili kulitengenezea vigezo
fulani ambavyo kila taasisi haina budi kuvizingatia katika usafirishaji,
huduma na urejeshaji nyumbani wa mahujaji? Pia ingekuwa bora mkatengeneza
utaratibu wa ushirikiano baina ya taasisi zote. Kufanya hivyo kunaweza
kusaidia kunyoosha mambo pale yanapokuwa hayaendi vizuri. Inawezekana pia
kwamba kupitia ushirikiano huo mnaweza kuandaa usafiri wa pamoja na huduma
za pamoja kwa mahujaji wenu wawapo Makka na Madina na hivyo kupunguza
gharama.

*Ushirikishwaji Masuala ya Kitaifa *

Mheshimiwa Mufti;

Tumeipokea rai yenu ya kutaka Serikali iyatambue na kuyashirikisha mashirika
ya dini kwenye mambo muhimu yahusuyo maslahi ya taifa kabla ya kutekelezwa.
Rai hiyo ni njema na tutaizingatia. Hata hivyo, napenda kuwahakikishia
viongozi wa dini zote na waumini wao kuwa hiyo ndiyo sera na utaratibu wa
Serikali kwa miaka mingi na haujabadilika. Kama itatokea kutofanyika ni
upungufu wa bahati mbaya au wahusika Serikalini ni wageni au wazembe.

Kwa suala hili la mchakato wa Katiba mpya nilikwishaeleza kuwa viongozi wa
dini watashirikishwa katika hatua zote muhimu tangu kutoa maoni kuhusu
masuala ya kuunda Tume, kwenye Tume yenyewe, mjadala, Bunge la Katiba na
katika kura ya maoni.

Mheshimiwa Mufti;

Pamoja na ushirikishwaji huo napenda kurudia rai au tahadhari niliyoitoa
wakati wa mkutano wangu na Maaskofu walio Wajumbe wa Jukwaa la Wakristo
Tanzania tarehe 22 Julai, 2011 jijini Dar es Salaam. Niliomba tujitahidi
kuhakikisha kuwa mjadala wa Katiba haugeuki kuwa mdahalo au malumbano kati
ya Wakristo na Waislamu kuingiza maslahi ya dini zao katika Katiba.
Tukiufikisha hapo, kutatokea mivutano ambayo ni migumu kuipatia majibu na
kuna hatari ya Katiba mpya kushindikana kupatikana au kuchelewa sana na hata
amani kuvunjika. Inaweza kuwa ndiyo mwanzo wa umoja wa taifa letu
tulioujenga kwa takriban nusu karne kuvurugika kwa namna ambayo itakuwa
vigumu kuujenga tena. Napenda kuona wote wanapata fursa ya kushiriki kwa
lengo la kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa nchi ya watu wa dini zote,
wenye umoja miongoni mwao. Tanzania inaendelea kuwa haina dini ingawaje raia
wana dini na uhuru wa kuabudu umehakikishwa na kulindwa ndani ya Katiba kwa
mujibu wa na Sheria za nchi. Hali linawezekana kama viongozi wa dini
tutataka kwa dhati iwe hivyo.

*Shule za Taasisi za Kiislamu *

Mheshimiwa Mufti; Ndugu Zangu Waislamu na Watanzania Wenzangu;

Nimesikia maelezo na maombi yenu kuhusu shule zilizokuwa zinamilikiwa na
taasisi za Kiislamu zilizotaifishwa na Serikali baada ya Uhuru. Ni kweli
kwamba mara baada ya Uhuru shule zote za msingi, sekondari na vyuo
vilivyokuwa vinamilikiwa na mashirika ya dini na jumuiya za kijamii
zilitaifishwa. Ni kweli pia chache kati ya hizo zilirejeshwa kwa wamiliki wa
awali katika miaka ya 1990. Ni kweli vile vile, kwamba mashirika ya dini
ikiwemo BAKWATA na jumuiya za kijamii zimekuwa zikiomba kurudishiwa shule
hizo lakini Serikali haijayakubali maombi hayo.

Mheshimiwa Mufti; Waheshimiwa Masheikh;

Katika mkutano wangu wa tarehe 22 Julai, 2011 na Jukwaa la Wakristo suala
hili lilijitokeza na nililitolea ufafanuzi ambao napenda nirudie kuueleza
hapa leo. Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa nchi yetu, Mwalimu Julius
Nyerere aliamua kutaifisha shule zote za mashirika ya dini na jumuiya za
kijamii hasa za Wahindi na Wazungu kwa lengo la kutoa fursa sawa ya kupata
elimu kwa watoto wa dini zote, wasiokuwa na dini na wa rangi zote bila
kubaguliwa.

Kutokana na uamuzi ule hakuna mtoto aliyebaguliwa kupata elimu kwa sababu ya
rangi yake au dini yake. Hata wale waliotoka kwenye jamii ambazo kwa dini
zao au rangi zao hawakuwa na shule kabisa au walikuwa nazo kidogo waliweza
kupata nafasi, bora tu wawe na sifa stahiki hasa za kufaulu mitihani na
nyinginezo. Lakini si hivyo tu, ili kujenga usawa kwa upande wa sekondari
Mwalimu alikwenda mbali zaidi. Serikali iligawa sawia nafasi za kwenda
sekondari kwa mikoa na wilaya nchini na siyo tu kufuata kigezo cha mtu
kufaulu mitihani.

Mheshimiwa Mufti;

Baada ya kutaifisha shule hizo, ukiacha shule za msingi zilizojengwa karibu
kila kijiji, Serikali haikuwekeza sana katika ujenzi wa shule mpya za
sekondari. Matokeo yake wakati ule katika mikoa yetu, ukizungumzia shule za
sekondari za Serikali, kwa kweli nyingi, kama siyo zote, ni hizi
zilizotaifishwa kwani Wakoloni hawakuacha shule nyingi na Serikali
haikujenga nyingi mpya. Kwa kweli uwekezaji uliongezeka kwa wingi sana kwa
shule za sekondari za Serikali katika Awamu ya Nne kwa ujenzi wa Sekondari
za Kata.

Kwa kutambua ukweli kwamba shule za Serikali ni kidogo hata baada ya
Serikali kutiliana saini Itifaki ya Makubaliano (MoU) na TEC na CCT mwaka
1992, kasi ya kurejesha shule ilikuwa ndogo sana na baadae ikasimama kabisa.
Kilichosimamisha ni ule ukweli kwamba zingerudishwa zote Serikali ingejikuta
kama vile haina shule za sekondari na badala yake shule zingekuwa mikononi
mwa makanisa. Kitendo hicho kingezua manung’uniko na mgogoro katika jamii
hasa baada ya zaidi ya miaka mingi shule hizo kuwa mali ya Serikali. Kwa
ajili hiyo, pamoja na nia njema iliyokuwepo ya kuziboresha na kuziendeleza
uamuzi huo ulikuwa mgumu kutekelezeka. Serikali ikajipa dhima ya kuziboresha
na kuziendeleza.

Mheshimiwa Mufti; Viongozi wa Dini Zote;

Ushauri na maombi yetu kwa BAKWATA na mashirika mengine ya dini na jumuia
zilizokuwa na shule wafikirie kuwekeza katika ujenzi wa shule na vyuo vipya
badala ya kuendelea kudai shule zao za zamani. Ahadi kubwa ya Serikali
inayotoa kwenu ni kuwa hazitataifishwa tena.

*Dawa za Kulevya *

Mheshimiwa Mufti;

Kuhusu dawa za kulevya, sina budi kuwashukuru kwa msimamo wenu wa kutambua
kuwepo tatizo na utayari wenu wa kushirikiana na Serikali katika mapambano
haya. Msimamo huo unanipa faraja kwani kwa kweli tatizo ni kubwa sana. Sisi
katika Serikali tumejipanga vizuri na tumeongeza sana nguvu ya kupambana na
uovu huu. Tunapata mafanikio lakini kazi iliyo mbele yetu ni kubwa sana
inayohitaji ushirikiano wa jamii nzima wakiwemo viongozi wa dini na waumini
wao. Na huo ndiyo ujumbe wangu wa msingi nilioutoa Mwanza tarehe 29 Mei,
2011 wakati wa kuwekwa Wakfu Askofu Albert Jella Randa wa Kanisa la
Mennonite na Mbinga tarehe 5 Juni, 2011 wakati wa kuwekwa Wakfu Askofu John
C. Ndimbo wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga.
Bahati mbaya sana nilipoelezea masikitiko yangu kwamba hata baadhi ya
watumishi wa Mungu wanajihusisha na biashara hiyo, imeeleweka ndiyo sivyo na
kutafsiriwa isivyo. Ni kweli kama walivyoeleza vyema watu wanaoshughulikia
tatizo hili, kwamba miongoni mwa waliokamatwa na kufikishwa Mahakamani wamo
watumishi wa Mungu wa wa ngazi mbalimbali wa dini zetu zote. Hakuna Askofu
wala Sheikh mzito.
Napenda kuwahakikishia kuwa mimi nitakuwa mtu wa mwisho au kutoa maneno ya
kejeli kwa kuwashutumu watumishi wa Mungu. Kwanza sina sababu ya kufanya
hivyo, lakini pia ninawaheshimu sana. Hata hivyo, nawiwa na wajibu kupeana
taarifa na kutahadharishana na kuomba tushirikiane pale ukweli
unapoonekana.
Nirudie kuwaomba viongozi wa dini zote tushirikiane na tusaidiane katika
mapambano haya ambayo ni yetu sote. Ni jambo lenye maslahi mapana kwa taifa
letu, leo na hasa kesho na kesho kutwa kwani walengwa na waathirika wakubwa
wa dawa za kulevya ni watoto na vijana wetu ambao ndiyo warithi wetu na
taifa la kesho.

*Mahakama ya Kadhi *

Mheshimiwa Mufti;

Kuhusu mchakato wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi, nimeyasikia maoni yenu
kwamba kumekuwa na kulegalega kwa upande wa Serikali jambo linalowafanya
muingiwe na wasiwasi kuhusu nia njema ya Serikali katika mchakato huu.
Napenda kuwatoa hofu kuwa hakuna kulegalega wala kubadilika kwa dhamira ya
Serikali. Msimamo wa Serikali upo pale pale. Huu ni uamuzi uliofanywa na
Chama chetu na Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais Benjamin
Mkapa wa kutaka kulitafutia ufumbuzi suala la Mahakama ya Kadhi na kuachiwa
Serikali ya Awamu ya Nne kutekeleza.

Na sisi katika kufuatilia utekelezaji wa jambo hili tulikabidhi Tume ya
Kurekebisha Sheria kuishauri Serikali. Ushauri wa Tume hiyo ulikuwa kwamba
Serikali haiwezi kuunda Mahakama ya kushughulikia masuala ya kidini ya dini
fulani. Jambo hilo liachiwe Waislamu wenyewe kufanya.
Serikali imekubali ushauri huo na ndipo mchakato ukaanza na tukaunda Kamati
ya pamoja iliyojumuisha Serikali na BAKWATA. Nia ya Serikali ni
kujihakikishia kuwa hicho kitakachoundwa hakiendi nje ya masuala ya kidini
yaani ndoa, takala, mirathi na wakfu kwa mujibu wa dini ya Kiislamu. Katu si
Mahakama ya kushughulikia masuala ya jinai au madai. Haitajihusisha na
masuala ya wizi na kutoa adhabu kama vile za kukatwa mikono. Haitahusika na
kesi za fumanizi na hivyo kutoa hukumu ya kuuawa mkosaji kwa kupigwa mawe.
La hasha !! Narudia kuwa mamlaka yake yatahusu ndoa, takala, mirathi na
wakfu. Isitoshe Muislamu hatazuiliwa kuamua kutumia sheria za nchi kwa
masuala hayo akipenda kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mufti, Waheshimiwa Masheikh, Ndugu Zangu Waislamu;

Napenda kuwatoa hofu pia kwamba hakuna mkono wa mtu wapo mnadhania hivyo.
Maana, tunajuana. Si ajabu kuna hisia kuwa huenda Kanisa limeingilia kati
kuzuia au kuchelewesha. Siyo hivyo hata kidogo. Tarehe 22 Julai, 2011
nilipoalikwa kuzungumza na Maaskofu katika kikao chao cha Jukwaa la Wakristo
katika risala yao kwangu kuhusu suala la Mahakama ya Kadhi walitoa ushauri
ufuatao kuwa:
“Kuanzisha Mahakama ya Kadhi nchini na jambo zuri linalowahusu Waislamu. Kwa
kuwa ni jambo la kidini waachiwe Waislamu wenyewe walifanye ndani ya
Uislamu, pasipo kutumia hazina ya Serikali ambayo ni fedha ya walipa kodi
wote nchini”

Hiyo ni nukuu kutoka ibara ya 6 ya Risala yao kuhusu Uhuru wa Kuabudu na
dhana ya Udini.
Katika maelezo yangu kwao, niliwahakikishia kuwa mawazo yao yanawiana na
yale ya Serikali kama ilivyoshauriwa na Tume ya Kurekebisha Sheria ambayo
Mwenyekiti wake ni Profesa Ibrahim Juma. Mahakama hii itaundwa na Waislamu
wenyewe ndani ya Uislamu wao na wataiendesha wenyewe na haitagharamiwa na
Serikali.

*Sheria ya Ndoa *

Mheshimiwa Mufti;

Ni kweli kwamba Serikali inao mpango wa kupeleka Bungeni Muswada wa Sheria
wa kurekebisha Sheria ya Ndoa ya sasa. Napenda kuwahakikishia kwamba
Serikali inatambua nafasi ya dini katika masuala ya ndoa na mirathi. Si nia
ya Serikali kuanzisha ugomvi na madhehebu ya dini kuhusu suala hili na
lingine lolote. Bahati nzuri taratibu za kutunga sheria ni taratibu zilizo
wazi. Hazina usiri kwa upande wa maandishi na nyaraka wala hauna kificho
katika kuzizungumzia. Miswada huchapishwa katika Gazeti la Serikali kwa kila
mtu kusoma. Pia kuna utaratibu wa kushirikisha wadau kutoa maoni yao kabla
ya muswada kuwasilishwa na kujadiliwa Bungeni.
Naomba nishauri kuwa Muswada utakapochapishwa katika Gazeti la Serikali
muusome na mhakikishe kuwa mnaandaa vyema maoni yenu kuhusu vipengele
mbalimbali vya Muswada. Kisha hakikisheni mnashiriki katika mikutano ya
wadau kuwasilisha maoni yenu hasa katika maeneo mnayoona yana migongano na
vitabu vitakatifu. Serikali yenu ni sikivu, naamini maoni yenu ya kujenga
yatasikilizwa na hata kuzingatiwa.

*Hitimisho *

Mheshimiwa Mufti, Waheshimiwa Masheikh, Waislamu Wenzangu na Wageni
Waalikwa;

Nimesema sana na leo ni sikukuu sipendi kuwapunguzia muda wenu wa kwenda
kusherehekea. Napenda kuwahakikishia kuwa Kiserikali tumejiandaa ipasavyo
kulinda usalama wa mali na maisha ya wananchi katika kipindi chote cha
sikukuu.

Mwisho kabisa nakushukuru tena, Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania
kwa kunipa heshima hii kubwa. Nawatakia Waislam na Watanzania wote kwa jumla
sikukuu ya Idd-El-Fitr yenye furaha na faraja tele. Nawaomba tuisherehekee
kwa amani na salama. Eid Mubarak!!

Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania

Assalam Aleykum Warahmatullahi Taala, Wabarakatuh.

Asanteni Sana kwa kunisikiliza
[image: Picture]
Rais Kikwete akiwasalimu waumini walishiriki swala ya Iddi katika msikiti wa
Kichangani, Magomeni asubuhi ya leo. (picha : Freddy Maro via Michuzi)

source:
http://www.wavuti.com/4/post/2011/08/rais-kikwete-hotuba-swala-ya-idd.html#ixzz1WfaO0UbE