Nishati Tanzania na maendeleo ya Watanzania

Ellen Manyangu:

NISHATI ni mhimili mkuu wa maendeleo ya uchumi wa nchi
yoyote duniani. Kwa karne nyingi mafuta asilia (petroli na dizeli) yamekuwa
vyanzo vikuu vya nishati katika sekta za viwanda, usafirishaji na kilimo.

Matumizi ya nishati asilia yanakabiliwa na changamoto
mbalimbali zikiwemo kusababisha kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabia nchi na
uchafuzi wa mazingira utokanao na hewa za salfa na nitrojeni. Pia tatizo
lingine la matumizi ya mafuta asilia limekuwa ni kupanda mara kwa mara kwa bei za mafuta na
upatikanaji usioaminika kutokana na hali ya machafuko inazozikumbuka nchi
zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani ikiwemo zile za Uarabuni na Italia.

Ripoti za tafiti mbalimbali duniani zinaeleza kuwa nishati asilia itakuwa bidhaa adimu sana au
kufikia ukomo ifikapo mwaka 2050. Hii inachangiwa na kupungua kwa hifadhi ya
nishati hii wakati idadi ya watu na mahitaji ya nishati hii yakiongezeka kila
siku.

Kutokana na sababu
hii nchi nyingi duniani zikiwemo za bara la Ulaya, Brazili na Marekani zimekuwa
katika jitihada kubwa za kutafuta vyanzo mbadala vya nishati asilia.

Kufikia sasa chanzo mbadala kinachotiliwa mkazo ni nishati
hai itokanayo na mimea. Zipo aina kuu tatu za nishati hii ambazo ni nishati
mimea ngumu (mkaa, kuni, mabaki ya nafaka), kimiminika (dizeli mimea na petroli
mimea) na gesi kama gesi hai asilia (biogas).

Hata hivyo, tafiti nyingi
zimeelekezwa kwenye matumizi ya nishati kimiminika kutokana na umuhimu
wake viwandani, katika kilimo na usafirishaji. Nishati dizeli mimea hutokana na
mafuta ya mbegu za mimea na ni mbadala wa dizeli asilia wakati nishati
kimiminika alkoholi hutokana na uchachushwaji wa mazao ya nafaka na ni mbadala
wa petroli asilia.

Matumizi ya nishati mimea kwenye injini za magari na mitambo
siyo jambo geni. Mafuta haya ndiyo ya kwanza kabisa kutumika kuendeshea injini
wakati Rudolf Disel kwa mara ya kwanza alipogundua injini hiyo na kujaribia kwa
mafuta ya karanga. Inaelezwa kuwa nishati mimea inaweza kuchangia kutatua matatizo
ya uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi. Hii ni kutokana ukweli
kwamba uunguaji wa mafuta haya huchangia kiasi kidogo cha hewa ya ukaa angani
kwani wakati wa ukuaji mimea hii huitumia hewa hiyo kujitengenezea chakula.

Tofauti na nishati asilia pia mafuta haya mbadala yana kiasi kidogo cha hewa za
salfa na nitrojeni ambazo husababisha mvua za tindikali na pia upatikanaji wake
ni rahisi.

Kutokana na msukumo mkubwa wa mahitaji wa nishati safi haswa
katika nchi za mabara ya Marekani na Ulaya kwa maendeleo ya viwanda, kilimo na
usafirishaji, bara la Afrika sasa limekuwa sehemu pekee inayoonekana kufaa kwa
uwekezaji katika kilimo cha mazao hayo.

Hii ni kutokana na uhaba mkubwa wa ardhi unaozikabili nchi
za mabara yaliyotajwa hapo juu. Katika kutambua fursa hii Tanzania imekuwa
ikipokea wawekezaji katika sekta ya
kilimo cha nishati mimea na kwa sasa mkazo ni upatikanaji wa nishati kutoka
kwenye kilimo cha mibono (Jatropha curcas).

Uwekezaji katika sekta hii muhimu ya nishati mbadala
Tanzania kunaweza kuwa msaada mkubwa sana kwa mkulima wa Kitanzania na kwa
uchumi wa nchi kwa ujumla.

Hata hivyo, kufanikia kiuchumi kutategemea sana kuwepo kwa
maandalizi ya serikali kiuwekezaji hasa katika uundwaji wa kanuni, sera na
sheria zitakazomlinda mkulima na usimamizi thabiti. Lakini kwa miaka kadhaa
tangu kuwepo kwa uwekezaji huo nchini humo inaonekana hakuna faida yoyote ambayo imekwishapatikana
ama kutokana na uchanga wa uwekezaji huo hapa chini au kutokuwepo kwa kanuni,
sera na sheria madhubuti zinazosimamia sekta hii.

Tatizo kubwa lililopo katika uzalishaji au ulimaji wa mazao
haya ya nishati mimea ni sera za nchi husika. Aidha katika tafiti mbalimbali
imeelezwa kuwa endapo matumizi na uzalishaji
wa nishati hii mbadala hautakuwa
makini utasababisha hasara na uharibifu mkubwa wa misitu ikiwa ni pamoja na
kuongezeka kwa majangwa, kupanda kwa gharama za chakula kutokana na ushindani
utakaokuwepo wa kuzalisha nishati na chakula hasa pale mazao ya chakula
yanapotumika kuzalisha nishati hiyo.

Mwaka 2008 Serikali ya Tanzania ilisimamisha huduma ya utoaji ardhi kwa ajili
ya kilimo cha kuzalishia nishati hiyo
ili kuweza kutengeneza sera ambayo itasimamia kwa uangalifu wa hali juu setka
husika. Hata hivyo, utoaji huo wa ardhi uligubikwa na tatizo kubwa la kutokuwepo
kwa mkakati maalum wa kutenga maeneo maalum ya kilimo hicho na mengine kwa
ajili ya kilimo cha chakula.

Imebainika kwamba maeneo mengi yanayochukuliwa kwa ajili ya
kilimo cha nishati mimea ni maeneo yenye rutuba ambayo wananchi wengi wamekuwa
wakiyatumia kuzalisha mazao ya chakula jambo ambalo linaweza kusababisha hatari
ya njaa.

Nchi zinapaswa kufanya maamuzi kwa umakini kabla ya
kuanzishwa kwa uzalishaji wa nishati mimea; inapaswa kuona uzalishaji huo
unaendana na mikakati ya maendeleo ya nchi husika, sera na mifumo ya kitaasisi.

Ni kutokana na kuwepo kwa madhaifu hayo utafiti huu
ulifanyika lengo kuu likiwa ni kubaini endapo uwekezaji katika kilimo cha
nishati mbadala Tanzania kunaweza kusuluhisha tatizo la umaskini au kunaongeza
umaskini kwa mkulima wa Kitanzania.

Matokeo ya Utafiti Wilayani Kisarawe

Matokeo ya utafiti nilioufanya Mkoa wa Pwani Wilayani
Kisarawe katika kijiji cha Mtamba ambako kampuni ya uwekezaji ya Sun Biofuel imewekeza katika kilimo cha
nishati mimea unaonyesha kuwa wananchi wengi kijijini hapo hawajafaidika na
uwekezaji huo kabisa.

Kampuni hiyo ya Sun Biofuel ambayo makao yake makuu yako
Uingereza imejikita katika kilimo cha mimea ya mbono ambapo inashikilia eneo
kubwa lenye hekta 9,000 za ardhi. Kwa mujibu meneja mwajiri wa Sun Biofuel ,
kampuni hiyo imeonyesha nia ya kuwekeza katika mimea hiyo tangu mwaka 2006
lakini kampuni hiyo ilimilikishwa ardhi mwaka 2008.

Aidha ilibainika kwamba mpaka sasa wamekwishavuna mbegu mara
moja tu tangu kuanza kwa uwekezaji na kiasi hicho cha mbegu ni tani 30 zenye
uwezo wa kutoa mafuta ya nishati. Pia ilibainika kwamba pamoja na kuwepo kwa
kiasi hicho kikubwa cha mbegu bado hazijaanza kusindikwa kuzalisha mafuta
kutokana na kutokuwepo kwa mashine ya kusindika.

Hii inaonyesha kwamba bado kiasi kikubwa cha Watanzania
haswa wa eneo hili la Kisarawe wanakosa ajira ambayo ingetokana na usindikaji
wa mafuta hayo. Vilevile ni dhahiri kwamba uhifadhi wa muda mrefu wa mbegu za
mimea ni changamoto katika uwekezaji wa nishati mbadala

Hii ni kutokana na ushahidi wa kisayansi kwamba kila aina ya
mbegu ina muda wake maalum wa kuishi kabla ya kuharibika. Pia utunzaji wa muda
mrefu wa mbegu umebainika katika ripoti za kisayansi kupunguza ubora wa nishati
itakayopatikana kwenye mafuta ya mbegu hizo.

Hii ni sababu tosha
kabisa ambayo inaweza kuwafanya wawekezaji kulazimika kusafirisha mbegu (mali
ghafi) kwenda nchi zao husika jambo ambalo pia linaweza kuikosesha Tanzania
faida kubwa kiuchumi. Kwa mtizamo huu, kama hakutakuwa na mkazo wa serikali
katika kufuatilia kuona wawekezaji wanatimiza masharti ya mikataba kuna kila
dalili za uwekezaji katika sekta hii kutoleta faida zilizotegemewa.

Ingawaje kampuni hiyo haijatoa ajira kwenye usindikaji wa
mafuta, meneja wa kampuni hiyo alibainisha kwamba mpaka sasa imekwishaajiri
wafanyakazi wa kudumu zaidi ya 500 katika nyanja mbalimbali kutoka katika
vijiji jirani vinavyolizunguka eneo hilo.

Ajira hizi zimesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza umaskini
na kukuza uchumi kwa wanakijiji wa maeneo hayo.
Licha ya ajira hizo huduma mbalimbali za kijamii zilizoahidiwa kutolewa
na kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha afya, huduma ya maji,
umeme, ujenzi wa shule, maabara za shule na nyumba za walimu
zimetolewa/hazijatolewa .

Kuhusu hatua za umiliki wa eneo hilo, ilifahamika kwamba
kampuni hiyo kabla ya kuchukua kuwekeza katika eneo hilo ilifuata taratibu zote
za uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wanakijiji wa maeneo husika na
kukubaliana katika hilo.

Kwa upande mwingine, licha ya kupewa ahadi hizo wanakijiji
wa Mtamba ambapo kampuni hiyo ina ofisi zake wameonyesha kutokufaidika na
uwekezaji huo ikiwa ni pamoja na kuonyesha mazingira duni wanayoishi kwa sasa.

Hayo yalibainika katika mahojiano yaliyojumuisha wakazi 70
wa eneo hilo, wakiwemo wakulima wadogowadogo, wanakijiji, uongozi wa kijiji wa
mwenyekiti na mtendaji wa kijiji. Katika mahojiano hayo yaliyofanyika ana kwa
ana na kwa kutumia dodoso, asilimia 71 walikiri kutonufaika, walikanusha kuwepo
kwa faida yoyote katika uzalishwaji wa nishati hiyo katika eneo hilo ilihali
asilimia 29 walikiri kunufaika kwa njia
moja au nyingine na uwekezaji huo.

“Wawekezaji hawa walipokuja walikuja na ushawishi mkubwa wa
ahadi za kujenga barabara, kuleta umeme wa solar[jua], ujenzi wa zahanati,
kujenga nyumba za walimu na maktaba lakini mpaka sasa miaka zaidi ya minne
imeisha hakuna hata moja walilotekeleza”. anaelezea Mtendaji wa kijiji Hamis
Rubalati, kauli ambayo inaungwa mkono na wanakijiji.

Kutokuwepo kwa huduma za jamii kama ilivyoahidi kampuni hiyo
kulithibitika pia baada ya kuzunguka eneo hilo kwa kushirikiana na wanakijiji.

Kwa niaba ya wanakijiji waliounga mkono kauli hii,
Mwanakijiji Mayanga Mwimbe anaeleza kuwa “Wawekezaji hawa wakati wanatafuta
ardhi walikuwa wapole na kauli zao zilikuwa za kushawishi ukizingatia kijijini
hapa hakuna hata duka la dawa baridi, hivyo tulivyooambiwa suala la zahanati ilikua
ni faraja kubwa kwetu kwa kujua sasa mkombozi amekuja, lakini ni kinyume
chake”.

Naye Mwenyekiti Nassoro wa Kijiji cha Mzeru alieleza kuwa
licha ya kampuni hiyo kushindwa kutekeleza hayo yote bado hata nafasi za ajira
hazitolewi kwa kufuata utaratibu waliokubaliana na mwekezaji.

“Makubaliano yetu yalikuwa ni kutoa ajira kwa vijana wetu wa
vijiji ambavyo eneo lilichukuliwa ili kuweza kujikwamua na umaskini
unaotukabili, lakini hili nalo limekuwa kinyume kwani wanaopata ajira katika
kampuni hiyo ni wageni kutoka sehemu mbalimbali”, anasisitiza.

Aidha Mzeru alielezea
masikitiko yake kwa wanakijiji hasa waliochukuliwa maeneo yao kwa muda mrefu
ilhali kampuni hiyo ikiwa kimya kwa kushindwa kuwalipa fidia wahusika.

Katika mahojiano mengine ambayo yalimhusisha Afisa Programu
wa Hakiardhi Valentin Olyang’iri
ilibainika kwamba licha ya faida zinazoweza kupatikana hapo baadae hivi
sasa wanakijiji hao hawafaidiki na chochote. Hakiardhi iliongeza kwamba
ilifanya utafiti katika eneo hilo na kutoa elimu kwa wanakijiji hao kuhusu haki
za ardhi ambazo wao kama wahusika na walengwa wanapaswa kuzifahamu kwa kina ili
ziweze kuwasaidia.

Aidha kutokana na matokeo ya utafiti huu, serikali inapaswa
kuangalia kwa umakini athari na faida za uwekezaji wa aina hii katika maeneo
mbalimbali nchini.

Pia Serikali iwe msimamizi wa kweli na wa haki katika malipo
ya fidia ya za wanavijiji wanaochukuliwa maeneo ili kuweza kuleta tija na
ushirikiano kati ya wawekezaji na wanakijiji wanaowazunguka. Ni jambo la
kusikitisha kwamba hadi sasa hakuna sera maalum ya uwekezaji katika nishati
mimea.

Iwapo sera
inayotengenezwa itakamilika na haya yote yakazingatiwa na kusimamiwa kwa
ufasaha ni hakika yanaweza kutekelezwa
ipasavyo. Ni wazi kuwa uwekezaji au ulimaji wa mazao haya utakua ni njia
mbadala ya kupungua kwa umaskini wa binafsi na kukuza uchumi wa nchi kwa
kiwango cha juu kwa taifa endapo sera
hizi zitakuwepo na kuzingatiwa kwa umakini na uzalendo.

Ili kuepuka matumizi mabaya ya ardhi yenye rutuba kwa kilimo
cha nishati ni vyema serikali ikatafiti na kuandaa ramani za maeneo yanayofaa
kwa kilimo cha mazao ya chakula au nishati.

Pia imebainika kwamba kitendo cha serikali kuwauzia
wawekezaji ardhi hakifai kwani ardhi ndio rasilimali kuu ya nchi yoyote. Kwa
vile wakulima wakitanzania wana ardhi na mwekezaji ana fedha ni vyema pia
kuwepo na utaratibu wa ubia/shea ambapo mtaji wa mkulima utakuwa ni ardhi na wa
mwekezaji hela.

Hii itasaidia kugawana kipato baada ya kuvuna kulingana na
mchango wa mhusika. Mwisho kabisa uwekezaji bila kuuza ardhi unawezekana endapo
serikali itaamua kuwashawishi wawekezaji kununua mazao ya nishati kutoka kwa
wakulima kama ilivyo sasa kwa wakulima wa kahawa, pamba, tumbaku n.k. Uwekezaji
katika nishati mimea utakuwa wa mafanikio zaidi endapo kipaumbele kitakuwa
matumizi ya nishati hiyo ndani ya nchi na si usafirishaji wa mafuta hayo kwenda
nje.

Ni vyema haya
yakatiliwa mkazo kwenye uwekezaji katika kilimo cha mazao nishati kwani
wawekezaji wengine katika nchi mbalimbali za Afrika wameanza kutumia mwamvuli
wa uwekezaji kujipatia maelfu ya hekta za ardhi.

manyanguellen@gmail.com

Mwisho.