Wakazi Mtunduwaro wasubiri ‘chungu na tamu’ ya uwekezaji wa madini

*Machungu wanayajua, matamu wanasimuliwa tu
Na Tumaini Makene
Mzee Wasiwasi wa Kijiji cha Mtunduaro, ni mmoja kati ya mamia ya wananchi wa mitaa miwili katika Kijiji cha Mtunduaro, Kata ya Ruanda, wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma, ambao mpaka sasa hawana uhakika na maisha yao ya baadae, mara uzalishaji wa makaa ya mawe katika eneo la kijiji chao utakapoanza kufanya kazi.
Wakiwa wamezuiliwa kufanya shughuli zao hasa za ukulima tangu mwezi wa tatu mwaka huu, kwamba wakati wowote wanaweza kuhamishwa katika makazi hayo ambayo wameishi miaka na miaka, tangu enzi za mababu zao, Mzee Wasiwasi na wanakijiji wenzake bado hawana ufahamu wa kutosha juu ya kinachoendelea na kitakachoendelea.
Mbali ya kutojua kiwango cha fidia watakacholipwa kama kitauwiana na uhalisia wa tathmini ya mali zao, lakini pia wanauliza wao kama jamii ‘iliyolea’ makaa hayo ya mawe yanayoonekana kuwa na thamani sasa hata kuiondolea Tanzania tatizo la nishati umeme, watanufaikaje?
Wanakijiji hao hawataki kushuhudia yale yanayotokea huko North Mara, Geita, Buzwagi, Nzega, Bulyaghulu, Mererani, Buhemba, Tulawaka, Kahama na kwingineko, ambako sasa wawekezaji wanaonekana ni waporaji, badala ya kuwa wabia wa maendeleo. Wananchi wanashuhudia uhamishwaji mkubwa wa mali ukiwatajirisha watu wengine wachache, lakini wao wakiendelea kuishi katika lindi la umaskini wa kutupwa, kandokando ya utajiri unaotambulika duniani.
Mradi wa uchimbaji makaa ya mawe katika eneo hilo la akina Mzee Wasiwasi, utamilikiwa kwa ubia kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) pamoja na Kampuni ya Atomic Resources ya Australia, ambapo kwa pamoja wameunda kampuni tanzu ya TANCOAL Energy kwa ajili ya kuchimba Makaa ya Mawe eneo la Ngaka Wilayani Mbinga kwa lengo la kuzalisha Umeme 450MW. NDC wanatarajiwa kumiliki asilimia 30 za hisa.
Gharama za uwekezaji katika mradi huo zinatarajiwa kuwa takriban Dola za Marekani 350m. Na hapa ndipo moja ya maswali ya akina Mzee Wasiwasi linajitokeza, wanakijiji hao watanufaikaje na maisha yao kubadilika kutokana na uwekezaji huo mkubwa wa mabilioni ya shilingi?
Mradi huo wa Makaa ya Mawe unaojulikana zaidi kwa jina la Ngaka (Mbinga) ni kati ya maeneo matatu ambayo yamepewa jina la ‘Eneo Mkakati la uzalishaji wa Megawatt 1500 za Umeme Kusini mwa Tanzania’. Maeneo mengine ni Liganga na Mchuchuma (Ludewa, Iringa) na Kiwira (Ileje/Kyela) mkoani Mbeya.
Eneo hili linatajwa kuwa moja ya ‘mwarobaini’ wa matatizo ya umeme nchini, yakiisaidia nchi kuondokana na utegemezi wa vyanzo vya maji. Inakadiriwa kuwa eneo hili la miradi ya makaa ya mawe kusini mwa Tanzania kwa pamoja linaweza kuzalisha umeme wa Megawati 1500 ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo na kuendelea na uzalishaji kwa kipindi cha miaka 150 ijayo kabla ya makaa ya mawe hayajamalizika.
Wananchi wanao wasiwasi
Wananchi wa Kijiji cha Mtunduwaro wanayo madai yao ya msingi hasa wakitumia uzoefu wa maeneo mengine ambako wananchi wamewahi kuathiriwa na uanzishwaji miradi mbalimbali, ikiwemo kama huo wa uwekezaji wa kuchimba madini. Suala muhimu kwao sasa ni namna gani maisha yao yataweza kusonga mbele na pengine kuwa bora zaidi, kuliko ilivyokuwa kabla. Wanataka kunufaika na mgodi ulioko katika eneo lao. Walipozaliwa. Walipokulia, wao pamoja na madini hayo ya makaa ya mawe.
Mzee Wasiwasi kama lilivyo jina lake hilo la utani, kama walivyo wananchi wengine wa Mtunduwaro, amejawa na hofu juu ya hatima ya maisha aliyokuwa akiishi kama yatendelea kuwa sawa tena mara atakapohamishwa kutoka katika eneo ambalo amekuwa akiishi kwa muda mrefu sasa, tangu enzi za mababu zake.
“Hapa tulipo hatuna uhakika itakuwaje, labda ninyi wasomi na mnaojua sheria mtusaidie hapa, hatujui lolote kwa kweli tunaona hawa jamaa wapo hapa muda mrefu na wanaendelea na mambo yao kama kawaida. Tumeshafanyiwa tathmini ya mali zetu lakini kuna mambo hayaeleweki hasa katika bei ya vitu vyetu,” anasema Mzee Wasiwasi akizungumza na Majira.
Anasema wanavijiji hao wamezuiliwa kufanya shughuli zozote za kilimo, husuasn kwenye mazao kama viazi na mihogo tangu mwezi wa tatu mwaka huu, lakini mpaka leo hawajaambiwa lini hasa watahama baada ya kuwa wameshalipwa mafao yao kama inavyostahili. Wanahoji, kutakuwa salama hapa kweli?
Anasema kuwa mpaka sasa hajui serikali itazingatia namna gani suala la wao kumiliki maeneo makubwa ya ardhi kwa njia ya kimila, ambayo walilirithi kutoka kwa mababu zao, huku akidai kuwa Mbunge wao Bw. Gaudence Kayombo alikwenda kuzungumza nao na akwahakikishia kuwa serikali itahakikisha wanalipwa stahili zao zote.
“Lakini tatizo bado lipo la msingi tunalipwaje, maana hatujawahi kukaa nao kuzungumzia malipo yetu yanafanyia vipi na lini hasa watafanya kwani muda unakwenda nasi tunahitaji kujipanga katika hayo maeneo tutakayohamia…isije ikafika wakati tukaanza kuondolewa kwa kasi tu hapa…maana tulitegemea serikali pamoja na kampuni hiyo watusaidie vizuri kupata haki zetu,” anaongeza Mzee Wasiwasi.
Maoni ya Mzee Wasiwasi yanawasilisha maoni ya wanakijiji wengi wa Kijiji cha Mtunduwaro ambao wataathirika na uwekezaji huo mkubwa. Katika moja ya mikutano ya hadhara ambayo ilifanyika kijiji jirani cha Ruanda na Majira kupata bahati ya kuhudhuria hali ya sintofahamu ilionekana dhahiri kuwagubika wananchi hao kwa kiasi kikubwa.
Pamoja na suala la fidia kutawala mjadala, wakihoji haki zao zitakavyolindwa ili kusitokee ubadhirifu wa aina yoyote wa mapunjo, majina hewa au wanaostahili kujikuta wanakosa haki zao kabisa badala yake zikaenda kwa watu wengine, kufanyiwa tathmini isiyokwa sahihi au kukutana na hundi ya fedha benki isiyolingana na matarajio, huku pia wakiwa ‘hawana’ tena fursa ya kulalamika, pia walihoji juu ya athari za uwekezaji wa namna hiyo.
Wamejawa na hofu na matumaini. Wanasubri chungu na tamu ya uwekezaji mkubwa katika sekta ya madini, moja ya sekta zinazokuwa kwa kasi sana nchini huku ikiwa inavutia wawekezaji wakubwa kutoka nje ya nchi kwa takriban miaka 15 iliyopita.
Chungu wanaijua, tamu wanasimuliwa tu kwa maneno. Bado hawana uhakika iwapo utamu huo utaweza kujidhihirisha katika vitendo.
Wanayajua machungu ya uwekezaji mkubwa katika madini nchini kwa kupitia kwa Watanzania wenzao katika maeneo mbalimbali, mathalani Nyamongo- Tarime, Geita, Bulyanghulu, Kahama, Nzega, Buhemba.
Mathalani wanajua namna gani watu walioko karibu na Mgodi wa Resolute huko Nzega wanavyohangaika. Milipuko inayotokea mgodini wakati wa uchimbaji dhahabu si kwamba unawakosesha raha ya maisha ya utulivu waliyoizoea miaka nenda miaka rudi na kuwaweka katika hatari ya hata kuangukiwa na nyumba zao tu, bali unatikisa ‘mihimili’ ya afya zao kuweza kuendelea kuyaishi maisha hayo muda mrefu duniani.
Pia wanajua namna gani wenzao (wao na mifugo yao), watoto kwa wakubwa, wanaume kwa wanawake na vijana kwa vikongwe, wa Nyamongo Tarime, mkoani Mara, ambao badala ya maisha yao kuboreshwa kutokana na utajiri huo unaovunwa kila siku, walijikuta wakimbulia kuathiriwa na sumu kutoka katika Mgodi wa North Mara, iliyokuwa ikitiririkia kwenye maji wanayotegemea kwa shughuli zao za kila siku katika Mto Tigite.
Wanajua pia wenzao katika vijiji vinavyozunguka Mgodi wa GGM huko Geita walivyowahi kuambulia dhahama kama hiyo ya Tigite. Bila kusahau vumbi la milipuko linavyozidi kuweka afya zao rehani.
Akina Wasiwasi na wenzake wanajua hadithi ya kile kilichowapata wananchi wa Bulyaghulu waliokuwa wakidai stahili zao kuweza kupisha uwekezaji mkubwa wa kuchimba dhahabu katika eneo hilo. Waliishiwa kufukiwa na kuzikwa wakingali hai katika mashimo. Mpaka leo serikali imekataa kuunda tume huru kuchunguza ukweli wa madai haya mazito na ya kikatili dhidi ya binadamu. Tena usiojali hata raia wenyeji kwa manufaa ya makampuni makubwa ya kigeni.
Wanajua madhira wanayoyapata baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam ambao maisha yao kila siku yako hataraini kutokana na sumu zinazozalishwa kutoka katika baadhi ya viwanda kama vile vya bia, khanga na mafuta, ambavyo daima, kwa sababu ya sapoti ya wakubwa serikalini, vimeendelea kupuuza madai ya msingi ya haki za binadamu katika maeneo hayo ya uzalishaji.
Wanatambua jinsi Watanzania wengine, mahali pengi hapa nchini wamekosa haki zao za msingi kwa sababu tu serikali yao mara zote inakuwa upande wa kutetea maslahi ya mwekezaji kwa guvu iwayo yote, hata kama ni kwa gharama ya kupoteza uhalali kwa wananchi wake walioiweka madarakani.
Matumaini
Mwalimu Mesa anasema kuwa mpaka sasa wanajua kuwa walau kijiji chao kitaweza kunufaika na sehemu ya mapato ya mgodi huo yatakayokuwa yakipatikana kwa mwaka. Lakini akisema kuwa hiyo ni ahadi tu, lakini bado hwana uhakika na utekelezaji wake.
Kitu kingine Mwalimu Mesa anachozungumzia kuwa ni matumaini kwa watu wa eneo hilo, ni ahadi ya vijana wa maeneo hayo kupewa kipaumbele katika ajira ambazo hazitahitaji utaalam katika kuzifanya. Lakini pia hata zile zitakazohitaji utaalam, basi bila shaka watakaopewa kipaumbele tena ni vijana ‘wao’ wa Kitanzania.
“Tumewahi kukaa katika mkutano wa kijiji na wale mabwana (wawekezaji) tuliomba tupate asilimia kumi ya mapato lakini wao wakasema kuwa wanaweza kutoa asilimia 5, lakini hatukufikia mwafaka kamili katika hilo tunasubiri tena watakaporudi bila shaka mambo yatakuwa mazuri.
“Lakini pia tumeambiwa kuwa vijana wetu hapa watapewa kipaumbele katika kupata ajira zitakazokuwa zikipatikana katika shughuli za kila siku za mgodi wa makaa ya mawe…lakini pia tunatarajia kuboreshwa kwa huduma za jamii katika eneo letu kwa kiasi kikubwa kutokana na utajiri huu,” anasema Mwalimu Mesa. Kwa mujibu wa maoni ya wanakijiji mbalimbali, waliozungumza na Majira juu ya uwekezaji huo, mpaka sasa wananchi wengi hawajui lolote kuhusu sheria zipi zitatumika katika kuhakikisha kuwa wao wanakuwa wanufaikaji katika uwekezaji huo wa mabilioni ya fedha. Kwani maisha yao yapaswa kuwa bora si kurudishwa nyuma katika umaskini ambao wamekuwa wakipigana kutaka kujikwamua.
Hawana habari na kuwa makampuni makubwa yanayofanya uwekezaji mkubwa kama huo yanapaswa kuwa na sera ya kuhudumia jamii inayowazunguka, kwa kushirikiana nayo katika kuboresha huduma mbalimbali za jamii kama vile katika elimu, afya, maji na mioundombinu. Na kwa hakika mengi yamekuwa yakionesha utayari wa kufanya hivyo lakini mara nyingi ama yamekosha msisitizo kutoka serikalini au mengine yanapotoa misaada hiyo huelekezwa kwenye matumbo ya watu.
Lakini pia hawajui kuwepo kwa sheria inayowabana wawekezaji katika uchimbaji madini juu ya kuwaendeleza wao katika maeneo yao, ndiyo maana Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Bw. Kabwe Zitto alisema kuwa kamati yake itahakikisha….
Akizungumza na waandishi wa habari mapema mwaka huu akizungumzia miradi hiyo ya megawati 1500, Bw. Kabwe alisema kuwa kamati ya POAC imependekeza kampuni tanzu itakayoundwa ili kuendesha mradi ifuate taratibu zote za uchimbaji ikiwemo kusainiwa kwa Mkataba wa Uendelezaji Migodi (Mineral Development Agreements-MDA) kwa madhumuni ya kulinda maslahi ya serikali, watu wa eneo husika na kampuni yenyewe.
Huku ubia huo ukizingatia kanuni ya faida (profitability and Pay Back period). Kwa mfano, kama NDC wameanza na kumiliki hisa asilimia 20 lakini mara baada ya mradi kulipa, mgawo wa hisa uwe ni sawa kwa sawa.
Suala la kuwa na sheria mahsusi inayoyaagiza makampuni makubwa yanayojihusisha na uwekezaji mkubwa kama huo wa kuchimba madini kutoa asilimia fulani ya mapato na pia kuhakikisha makampuni yanatimiza wajibu wa kisera huo wa kutoa huduma kwa jamii inayozunguka eneo la uwekezaji (si madini tu) uitwao Corporate Social Responsibility, ni kati ya mambo ambayo yanaelezwa yanaweza kuwa tiba ya migogoro kati ya wawekezaji na wananchi wanaozunguka maeneo husika.
Inaelezwa inaweza kutibu ‘vidonda ndugu’ kama vile vya maeneo ya Wazo huko Dar es Salaam, North Mara Nyamongo na maeneo mengine mengi, ambako wananchi wanaonekana kutonufaika na uwekezaji mkubwa unaovuna utajiri wa kutosha katika eneo wanaloishi.
Mbunge wa Ludewa, Bw. Deo Filikunjombe anasema kuwa kwa uhalisia hakuna kiongozi mpenda maendeleo ya nchi yake angependa kuendelea kuona kero za migodini, kwani kama kungekuwa na utaratibu mzuri wa wananchi kunufaika na utajiri unaochimbwa maeneo yao, hakuna mtu angeweza kuvamia mgodi na bila shaka wananchi hao ndiyo wangekuwa walinzi wa kwanza kulinda.
Akishauri kuwa sheria hiyo na utaratibu wa kampuni kutimiza wajibu wajibu kwa jamii zinazonguka mradi, Bw. Filikujombe anasema “unajua madini ni tofauti na rasilimali zingine kama mbuga au milima…madini haya yanavunwa na kuisha. Lakini pia uchimbaji una mdhara makubwa sana kimazingira, kiafya wananchi wanapata psychological torture kubwa sana, sasa hawa wananufaikaje?
“Mpaka sasa sheria za madini tulizonazo haziwanufaishi watu wa maeneo ya madini. Fujoz zote unazoziona zikitokea migodini zinasababishwa na kwamba wananchi hawana sense of ownership (wanajiona si sehemu ya umiliki wa mali hizo). Wanaona hawana ‘control’ (udhihiti) nayo. Sasa ninavyojua yapo makampuni yako tayari kabisa kutoa sehemu ya faida yake kwa wananchi, lakini tatizo ni sisi hatuna, wala hatutaki kutunga sheria hiyo.
“Wao wanataka tu sheria iwepo ili watekeleze…hawaoni shida kutoa sehemu ya kile walichokipata kwa mwaka mzima…royality…tukitoa mfano billions of money, mfano bilioni nne kwa halmashauri fulani husika, watu hawa watamaliza matatizo yao mengi. Wakipeleka milioni kadhaa katika vijiji vyao, kila mwaka wataboresha shule, watachimba visima, watajenga hata barabara zao bila kuomba fedha kwa mhisani,” anasema Bw. Filikunjombe na kuongeza;
“Tatizo letu ni kutofanya maamuzi. Hakuna mtu anayezipenda kero za mgodini, hakuna mtu anataka watu wavamie mgodi. Tungekuwa na sheria nzuri zinazowanufaisha wananchi ndiyo wangekuwa watu kwanza kabisa kuwa walinzi wa migodi hiyo. Mathalani kama serikali inapata asilimia 5, kisha katika hiyo ikatoa asilimia 1.5 kurudi kwa wananchi…lakini pia makampuni yakalazimika kutoa asilimia 3.5 hivi au 5 kabisa kama mengine yalivyo tayari hata sasa, tungeondoa vurugu hizi,” anasema mbunge huyo.
Akina Wasiwasi wa Mtunduwaro wanajua namna gani wakazi wa Wilaya ya Geita wasivyokuwa na uhakika wa nishati ya umeme wakati Mgodi wa GGM unazalisha umeme wa kutosha kwa ajili ya matumizi yake masaa 24 bila hofu ya kukatika. Wanasikia namna gani wakazi wa Nyamongo wanashuhudia mwanga masaa 24 katika Mgodi wa North Mara, lakini kilometa chache kufikia kwenye makazi yao wanaishi maisha ya kijima ya kibatari au kumulika kwa vijinga vya moto.
Muda unasogea, huku mradi huo wa Ngaka unaowatia wasiwasi akina Mzee Wasiwasi wa Kijiji cha Mtunduwaro ukitarajiwa kuanza ili kutibu gonjwa sugu la tatizo la umeme nchini. Kama watanufaika na mradi huo, ikiwemo hata kupata umeme wa kutosha kwa ajili ya wao kuweza kutafuta fursa za maendeleo katika Karne ya 21, ili washindane na wanavijiji wa China, Korea, Vietnam, Ghana, Misri, Libya au Afrika Kusini ni suala la kusubiri.