Tiiba ya babu imeleta maafa makubwa kwa wagonjwa

Chama cha Madaktari nchini (MAT) kimesema tiba inayotolewa na
Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
Ambilikile Mwasapila, kwa njia ya kikombe kwa ajili ya kutibu magonjwa
sugu, imeleta maafa makubwa kwa wagonjwa.
Makamu wa Rais wa MAT, Dk. Primus Saidia, alitoa tamko hilo wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana suala zima la magonjwa
yasiyoambukiza na tiba mbadala.
Alisema kuwa wagonjwa wengi baada ya kunywa kikombe cha Babu waliacha
kunywa dawa za magonjwa yaliyokuwa yakiwasumbua na kusababisha wengi
wao kupooza, kufa na wengine hali zao kuzidi kuwa mbaya.
“Ni vyema wananchi walio wagonjwa wa shinikizo la damu, kisukari,
anemia na magonjwa mengine wakafuata ushauri wa madaktari badala ya
kulaghaiwa na wachache,” alisema Dk. Saidia bila kufafanua zaidi.
Alisema umma wa Watanzania umekuwa ukilaghaiwa kwa tiba mbadala na
kuacha kutumia dawa za hospitali hivyo kuongeza ukubwa wa tatizo na
wanapokimbilia hospitali tayari hali zao zinakuwa mbaya.
Dk. Saidia alisema ili dawa iweze kutumika hufanyiwa utafiti kwa kati
ya miaka 10 hadi 15.
Naye Katibu Mkuu wa MAT, Dk. Richard Kabangira, ambaye ni daktari
bingwa ya tiba wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, alisema: “Serikali
yetu haisikilizi wana taaluma, mfano Babu wa Loliondo utafiti
uliofanyika pale ni wa dawa kutokuwa na madhara kwa binadamu na sio
kutibu magonjwa.” alisema Dk. Kabangila na kuongeza:
“Hospitali ya Rufaa ya Bugando ilipokea wagonjwa wengi wa kisukari
baada ya kutoka Loliondo kufuatia wagonjwa hao kuacha kunywa dawa
walizopewa hospitalini.”
Alisema waliwasiliana na wanachama wao nchini kote kufuatilia hali za
wagonjwa waliokuwa wamekwenda kwa Babu kupata kikombe na waligundua
kwamba waliokuwa wanatumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV),
shinikizo la damu, kisukari na hata saratani waliacha dawa baada ya
kunywa kikombe cha Babu.
Alisema pamoja na watu kadhaa kutoa ushahidi kuwa wamepona kwa dawa
hiyo, utafiti uliofanywa na MAT, umegundua kuwa hakuna hata mtu mmoja
aliyepona baada ya kunywa dawa ya Babu.
Alisema watumiaji wa ARV walipungua kama ilivyo kwa hao wengine,
lakini baada ya muda hali zao zilikuwa mbaya wengine walikimbilia
hospitalini lakini kwa kuwa walikuwa wamevuruga mtiririko wa tiba,
walipata madhara makubwa.
Dk. Kabangira alisema MAT ilimwandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii juu ya hatari ya tiba ya Babu, na kutoa
ushauri wao, lakini ulipuuzwa kwa sababu za kisiasa.
Kufuatia hali hiyo, MAT imetoa wito kwa Serikali na Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii kuwaeleza wananchi ukweli ili wasiangamie huku
wakieleza kusikitishwa kwao kutokana na tiba hiyo kutumika kisiasa.
Mchungaji Mwasapila alianza kutoa tiba hiyo mapema mwaka huu na
kusababisha maelfu ya wananchi kutoka pembe zote za nchi na nje ya
nchi kukimbilia nyumbani kwake katika kijiji cha Samunge, Loliondo
katika Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha kupata tiba hiyo dhidi ya
magonjwa mbalimbali yakiwemo ya kisukari, Ukimwi, saratani na
shinikizo la damu.
Viongozi mbalimbali wa madheheu ya dini nao walikuwa miongoni mwa
maelfu waliokwenda Samunge na kupata kikombe huku wakitoa ushuhuda
kwamba wamepona kwa dawa ya Mchungaji Mwasapila maarufu kwa jina la
Babu.
Safari ya kwenda Samunge ilikumbana na changamoto ya barabara mbovu
zilizosababisha misongamano na kuilazimisha serikali kuingilia kati
kupanga utaratibu pamoja na kusaidia kuboresha miundombinu.
Chama hicho leo kinafanya mkutano wao mjini Mwanza, suala la tiba ya
Babu linatarajiwa kuibuka katika mkutano huo unaowakutanisha wanachama
wake.

– Nipashe/ippmedia.com/frontend/index.php?l=32629


Sent from my mobile device