TANZANIA YACHAGULIWA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA KIMATAIFA WA 65 WA UTALII WA UNWTO

 Tanzania imechaguliwa  kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Utalii wa 65 wa Kanda ya Afrika utakaoandaliwa naShirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Utalii (UNWTO) kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania utakaofanyika  mwezi Oktoba mwaka 2022 katika Jiji la Arusha huku ukijumuisha Mawaziri wote wa  Utalii wa Bara la  Afrika

Aidha, Katika mkutano huo Tanzania imechaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Bajeti na Mipango ya UNWTO kwa kipindi cha muda wa miaka mitatu kuanzia sasa

Akizungumza  jana nchini Cape Verde katika  mkutano huo mbele ya jumla ya  mawaziri 30 wa utalii,  Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro amewashukuru Mawaziri hao kwa kuipa heshima nchi ya Tanzania huku akiowaomba mawaziri wote wa utalii kuja kushiriki katika mkutano huo mwakani.

Katika uchaguzi huo uliowakutanisha mawaziri  30 wa utalii wa Bara la  Afrika, Mawaziri hao waliridhia kwa kauli moja kuwa Tanzania ina sifa zote za kuwa mwenyeji wa mkutano huo mara baada ya Tanzania kuwa nchi pekee iliyokuwa imeonesha nia ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo.

Kufuatia hali hiyo Tanzania inakuwa ni nchi ya kwanza kupita bila kupingwa na katika mkutano  wa Kimataifa wa utalii wa 64  unaoendelea kufanyika  kwa muda wa siku nne kuanzia jana  katika kisiwa cha SAL nchini Cape Verde

Akizungumzia manufaa ya  mkutano huo, Dkt. Ndumbaro amesema  kufanyika mkutano huo nchini  utaiweka Tanzania katika ramani ya dunia kwa kutangaza fursa uwekezaji katika sekta ya utalii pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Katika hatua nyingine, Dkt. Ndumbaro amesema kitendo cha Mawaziri wote kuridhia kwa kauli moja kuwa Tanzania iwe mwenyeji wa mkutano huo ni  imani kubwa ya waliyonayo kwa nchi ya  Tanzania na Watanzania wote kwa ujumla

 Dkt. Ndumbaro amesema kufanyika kwa mkutano huo nchini Tanzania ni hatua mahsusi kwa nchi kujitangaza kimataifa kwa vile washiriki mbalimbali duniani watahudhuria mkutano huo wakiwemo wabobezi wa utalii pamoja na  makampuni makubwa ya kutangaza vivutio vya utalii kutoka nje yatatangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na Afrika kwa ujumla

Kwa upande wake Waziri wa Utalii na Mambokale wa Zanzibar, Mhe.Lela Mohamed Mussa amesema huo utachagiza idadi ya watalii watakaoitembelea Tanzania kupitia mkutano huo.

‘’ Tunajisikia fahari kuona ajenda yetu kama nchi ya kuja kushiriki katika mkutano huu umefanikiwa na tuna matumaini makubwa kuwa mkutano huo utatangaz vivutio vya  utalii vilivyoko Zanzibar na Tanzania bara’’ alisisitiza Mhe. Lela Mussa.

Naye Katibu Mkuu wa UNWTO, Zurab Pololikashvili amesema katika kipindi chake cha uongozi moja ya kipaumbele chake kikubwa ni kufanya uwekezaji katika  bara la Afrika ili kuongeza ajira kupitia sekta ya utalii.

Ujumbe wa Tanzania katika Mikutano  huo unaongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ambaye ameambatana na Waziri waUtalii na Mambokale wa Zanzibar Mhe.Lela Mohamed Mussa

Pia  Wajumbe wengine walioambatana na Mhe. Waziri ni pamoja Kamishna Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, Kamishna Uhifadhi kutoka TAWA, Mabula Misungwi, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Philip Chitaunga , Balozi wa Tanzania Paris, Mhe. Samweli Shelukindo pamoja na maofisa kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) , TTB pamoja na TANAPA