JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
MSIMAMO WA WIZARA KUHUSU UGAWAJI WA VITALU VYA UWINDAJI
UGAWAJI WA VITALU HAUTARUDIWA
Wizara ya Maliasili na Utalii haina mpango wa kurudia ugawaji wa
vitalu. Mchakato wa ugawaji ulikamilika mwezi Septemba mwaka jana
(2011) na matokeo yake kutangazwa wazi.
Mapema mwezi Septemba 2011, Wizara ilitoa orodha ya kampuni 60
zilizofanikiwa kugawiwa vitalu. Kati ya kampuni hizo, kampuni 51 ni za
kizalendo na kampuni 9 za kigeni kwa kuzingatia kifungu 39(3)(b) cha
sheria ya wanyamapori Na. 5, ya 2009.
Hata hivyo, kumekuwa na taarifa mbalimbali zilizoripotiwa na baadhi ya
vyombo vya habari kuhusu kuwepo kwa harakati zinazofanywa na waombaji
waliokosa vitalu zikihusisha kuchafuana baina ya kampuni zilizopata na
zilizokosa kwa nia ya kuzorotesha sekta ya uwindaji wa kitalii kwa
ujumla. Vyombo hivyo vimeripoti kuwa mchakato wa ugawaji wa vitalu
utarudiwa.
Wizara inasisitiza kuwa mchakato wa ugawaji wa vitalu hautarudiwa na
watanzania wanahakikishiwa kuwa hatua zilizochukuliwa na serikali za
kuleta mabadiliko kwenye sekta hii tangu mwaka 2008, zimesaidia sana
kuimarisha usimamizi wa Sekta hii.
Kuna mabadiliko zaidi ya 21 yaliyofanyika tangu wakati huo kwa
kuzingatia Sheria ya Wanyamapori, hivyo kufanya isiwe rahisi kwa mtu
au kikundi cha watu kufanya tofauti (yaani, the dicretionary powers of
decision makers have been seriously controlled).
Aidha, Wizara imesikitishwa na taarifa zilizoripotiwa na gazeti moja
la kila siku toleo la tarehe 10/1/2011 likinukuu taarifa kutoka
Dallas, Marekani kwamba zoezi la ugawaji vitalu litarudiwa kwa
shinikizo la Ikulu.
Madai hayo siyo kweli na  kwamba Wizara haijapokea maelekezo yoyote
kutoka Ikulu wala sehemu nyingine yoyote kuhusiana na suala hili la
vitalu.
Wizara inasisitiza kuwa waombaji waliopata vitalu wamehakikiwa na
Waziri na kuwa barua walizopokea kutoka Wizarani kuhusu kugawiwa
vitalu ni nyaraka halali za Wizara.
KABLA YA SHERIA MPYA YA WANYAMAPORI
Kabla ya 2008, taratibu za uendeshaji wa tasnia ya uwindaji wa kitalii
zilijumuisha vipengele vifuatavyo ambavyo vilikuwa na  mapungufu:
      i.           Ukubwa (size) wa vitalu ulikuwa hauna ukomo
kisayansi kuzingatia rasilimali zilizopo;
    ii.           Bei ya vitalu ilikuwa moja kwa vitalu vyote;
 iii.           Hayakuwepo madaraja ya ubora wa vitalu;
 iv.           Vitalu vilikuwa vinatolewa na Mkurugenzi wa Wanyamapori;
    v.           Hakukuwepo ushauri wowote ambao Mkurugenzi
alilazimika kupewa na mtu au kikundi chochote kinachotambulika
kisheria, kabla ya kumgawia mwombaji kitalu;
 vi.           Hakukuwepo uwazi juu ya uombaji, kama vile
vigezo/sifa za waombaji na utaratibu wa ugawaji;
vii.           Kampuni za uwindaji ziliruhusiwa kuwa na idadi ya
vitalu bila ukomo;
viii.           Kampuni za uwindaji, ambazo 95% zilikuwa za wageni
kwa hazikuwa na ulazima wa kuwa na watanzania.
 ix.           Kampuni za uwindaji hazikuwa na ulazima wa kuwa na
wawindaji bingwa watanzania.
    x.           Kulikuwa hakuna upekuzi kujiridhisha kuhusu
utendaji kazi wa kampuni kabla ya kupewa kitalu;
 xi.           Kampuni ziliruhusiwa kuuza hisa zake na vitalu
vilikuwa \’tradeable assets\’ za kampuni. Pia Serikali haikuwa na namna
ya kujua mikataba kati ya kampuni zilizouziana vitalu;
xii.           Hakukuwa na ulazima kwa kampuni za uwindaji kuwa na
watanzania kama wanahisa wake;
xiii.           Hakukwa na ukomo wa idadi ya kampuni za kigeni kumiliki vitalu;
xiv.           Bei ya nyara ilikuwa chini na ilidhibitiwa na
wawindani kupitia chama chao cha TAHOA.;
xv.           Mwombaji wa Kitalu alilazimika kuwa na vifaa kabla ya
kugawiwa kitalu;
xvi.           Waziri au Mkurugenzi alikuwa hana mamlaka ya kuvunja
mkataba kabla ya muda wa mkataba wa miaka 5 kuisha hata pale ambapo
muhusika alifanya mambo kinyume na taratibu;
xvii.           Kampuni za uwindaji hazikulazimika kulipa deposit
yoyote kwa kila mgeni anapokuja kwa kila siku ya safari;
xviii.           Haikuwa dhambi au marufuku kukodisha kitalu kwa mtu
mwingine tofauti na mtu au kampuni iliyoomba na kuingia makubaliano na
serikali;
xix.           Kampuni za uwindaji hazikuwekewa kiasi cha chini cha
kuchangia jamii jirani na vitalu;
xx.           Rekodi ya utii wa sheria, uchangiaji jamii, uchangiaji
wa shughuli za kupambana na ujangili, ulipaji kodi, uwekezaji/utunzaji
wa kitalu husika haikuzingatiwa katika kufikiria maombi ya wawindaji
kabla ya kugawiwa vitalu/kitalu;
xxi.           Hakukuwa na vigezo vya kuhakikisha vitalu vya aina
tofauti tofauti vinatolewa kwa mwombaji.
UTEKELEZAJI WA SHERIA MPYA YA WANYAMAPORI
Tangu mwaka 2008, serikali imefanya mabadiliko makubwa kwenye tasnia
hii ya uwindaji wa kitalii kwa kurekebisha vipengele vyote 21 vya
taratibu za awali kwa lengo la:
 (i)   Kuongeza wigo wa Watanzania kushiriki kwenye tasnina hii;
(ii)Â Â Â Kuongeza mapato ya Serikali;
(iii)Â Â Kuongeza uwazi na uwajibikaji;
Mabadiliko haya, yaliyoanzia kwenye azimio la Bunge na baadaye
kuingizwa kwenye Sheria ya Wanyamapori Na. 5, ya 2009, na Kanuni zake,
sasa yamekamilika na utekelezaji wa sheria kwa kuzingatia mabadiliko
haya unaendelea.
Mabadiliko ya vipengele vyote 21 yamefanyika kwa kuzingatia Sheria ya
Wanyamapori Na. 5, ya mwaka 2009 na Kanuni zake za mwaka 2010.
Kwa mfao, yafuatayo yamefanyika kama sehemu ya utekelezaji wa sheria hii.
      i.     Sheria ya Wanyamapori na 5 ya 2009 ilipitishwa ikiwa na
mabadiliko muhimu katika sekta hii;
    ii.     Tathmini ya vitalu ilifanyika na kuwekwa kwenye madaraja
matano ya ubora.;
 iii.     Serikali iliweka kipindi cha mpito cha mwaka 2009-2012 ili
kuruhusu mabadiliko kufanyika. Ilipangwa kuwa wawindaji wa mwaka 2013
wapatikane mwaka 2010-11, ili waanze maandalizi hadi msimu wa uwindaji
wa Julai 2013;
 iv.     Kanuni za Uwindaji wa Kitalii za 2010 zimekamilika;
    v.     Mwezi February 2011, vitalu 156 vilitangazwa ili viweze
kuombwa na wale ambao wangevihitaji;
 vi.     Kamati ya watu 12 ya kumshauri Waziri juu ya ugawaji wa
vitalu iliteuliwa na kufanya kazi yake. Kamati ilimshauri Waziri
kuhusu Vitalu 156 na waombaji 91 ambao walijitokeza;
vii.     Kamati ilipendekeza kuwa muda uongezwe ili upekuzi wa kina
ufanyike kuhusu dhamana, uraia, ulipaji kodi na uhalali wa kampuni
zilizoomba ukamilike kwa kuhusisha vyombo vyenye mamlaka na uwezo wa
kusemea maeneo hayo, kama vile Idara ya Uhamiaji;
viii.     Aidha, wakati kazi ya upekuzi ikiendelea, kamati ilishauri
kwa vitalu 22 ambavyo havikupata waombaji wenye sifa vitangazwe tena
ili zoezi la upekuzi lihusishe pia waombaji wa vitalu hivi (22) ili
kuokoa fedha na muda. Waziri aliafiki mapendekezo hayo;
 ix.     Muda wa kutangaza waliogawiwa vitalu uliongezwa kwa siku 90
hadi Sept 10, 2011. Aidha, vitalu 22 vilitangazwa tarehe 20 juni 2011
na waombaji kupewa hadi julai 19, 2011 wawe wamefikisha maombi
panapohusika.
MAAMUZI YAMEZINGATIA SHERIA
Kufuatia sheria na kanuni mpya zilizopo, msimamo wa Wizara ni kama ifuatavyo:
      i.     Wizara inaamini kuwa vielelezo vilivyowasilishwa na
waombaji na taarifa ya ukaguzi na upekuzi uliofanywa na kamati ya
ushauri kwa waombaji wote kwa zaidi ya siku 180 ni sahihi na
zilifanyika kwa mujibu wa sheria;
    ii.     Maamuzi ya Waziri yamezingatia sheria na mipaka ya
madaraka yake kama Waziri mwenye dhamana ya sekta husika. Wizara
inawasihi wahusika wote wafuate utaratibu wa kisheria katika
kuwasilisha malalamiko na vielelezo vyao;
 iii.     Mabadiliko yaliyofanyika ni sahihi. Wizara inawasihi wadau
wote wa tasnia ya uwindaji wa kitalii, kuunga mkono mabadiliko
yaliyofanyika maana yamefanyika kwa kuzingatia sheria;
Baada ya matokeo ya mchakato wa ugawaji kutangazwa, kampuni
zikizofanikiwa kupata vitalu ziliandikiwa barua kuarifiwa kuhusu
uamuzi huo na vitalu walivyopewa kwa mujibu wa sheria;
Matokeo hayo yalipokelewa kwa furaha na waombaji watanzania ambao
walipata fursa ya kutumia utajiri wa nchi yao kama mtaji wao;
Maamuzi haya pia yalipongezwa kwa kuzingatia azimio la Bunge kuhusu
hoja Binafsi ya Mzindakaya ya 2008 na baadaye sheria ya Wanyamapori
Na. 5, 2009;
Vilevile, matokeo hayo yalipongezwa na kuungwa mkono na Chama cha
wawindaji TAHOA maana yalizingatia sheria.
HITIMISHO
Wizara inasisitiza kuwa wadau wote watapaswa kuzingatia sheria katika
kuvitumia vitalu walivyopewa kwa kuwa sheria inatambua kuwa vitalu ni
mali ya serikali kwa dhamana ya Waziri. Kama kuna malalamiko yoyote ni
vema yafuate taratibui za kisheria.
Hadi sasa Kampuni kadhaa zimetumia fursa za kisheria kuomba mapitio ya
maamuzi ya Waziri (administrative review). Kwa mujibu wa sheria,
maombi haya ya administrative review hupelekwa kwa Kamati ya Ushauri
kuhusu Vitalu kwa maoni kabla ya Waziri kutoa uamuzi wa mwisho. Sheria
haijaweka ukomo wa kupokea malalamiko wala ukomo wa muda wa
kushughulikia malalamiko hayo. Kazi ya kupitia malalamiko hayo
inaendelea.
Hata hivyo, zoezi la administrative review ni la kawaida na husaidia
kufanyika marekebisho madogo kadiri ushahidi utakavyowasilishwa wala
halilengi KUBATILISHA MAAMUZI YOTE ya awali.
Pia, kama itaonekana kuwa Wizara imetafsiri vibaya sheria, hivyo
kutomtendea haki mwombaji ni vema mhusika aende Mahakamani.
Wizara anakumbusha pia kuwa mtumiaji wa kitalu ni kama mpangaji tu,
hivyo dhana kwamba kampuni fulani imekuwa na kitalu fulani kwa muda
mrefu hivyo kujijengea imani kwamba kitalu husika ni cha kampuni hiyo
siyo sahihi. Vitalu vyote ni mali ya Serikali.
Vilevile, kumekuwepo tuhuma kupitia vyombo vya habari kwamba baadhi ya
waombaji waliokosa vitalu wanafanya njama za kughushi baadhi ya
nyaraka ili kubadili sura za maombi yao ya awali.
Wizara inatahadharisha kuwa vitendo hivyo, kama vinafanyika ni kinyume
na sheria, na Wizara ikijiridhisha kwamba nyaraka zozote
zilizowasilishwa siyo sahihi au ni za kugushi, itawachukulia hatua za
kisheria wahusika. Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kuwafutia
watuhumiwa ugawaji waliokwishapata, hata kwenye vitalu vingine kama
wanavyo na kuwashitaki mahakamani.
Mwisho, Waziri wa Maliasili na Utalii ataunda Kamati ya Kutathmini
Matumizi ya Vitalu \’blocks utilization monitoring comittee\’. Kamati
hii itakuwa inafanya ukaguzi na uperembaji wa matumizi ya vitalu
vilivyokodishwa kwa kuzingatia sheria kwa muda wote wa ukodishaji na
kumshauri Waziri kuhusu hatua za kuchukua kwa waombaji watakaovunja
sheria.
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
12 Januari 2012