Michael Dalali:Makala (A tribute):kwa rafiki yangu Marehemu Regia Mtema

Michael Dalali: Kamanda Umechanua na kunyauka.Pumzika kwa amani!

“Tuache masihara, hakikisha unaninunulia ukiwa unarudi vitabu hivi;
Balance Scorecard na Iron Lady cha Margeth Thatcher maana nimesikia
upo nje ya bongo” aliniambia Regia, name nikamjibu “sawa. usijali
nitakununulia”! Sikufahamu kuwa ndiyo yalikuwa mawasiliano yetu ya
mwisho kati yangu na rafiki yangu Regia tuliyofanya tarehe 12.01.2012
na hata wala hatutoonana name kupata fursa ya kumpatia vitabu kama
ombi lake.

Kwangu ni kama ndoto. Ukishtuka isiwe kweli. Lakini si njozi. Tayari
Regia amefunga kitabu cha maisha yake duniani angali katika umri moto
wa ujana.

Angali akiwa bado na mipango na mikakati mwingi kutelekeleza.

Alikuwa rafiki yangu ambaye tulishazoea sana kiasi cha kutaniana na
kuongea upuuzi upuuzi mwingi sana……maana hata binadamu wa namna gani
kuna watu wake ambao anataniana nao na hata kuongea upuuzi upuuzi.

Niandikapo tanzia hii kwa laptop nayo ni sehemu yenye kuongeza
machungu na simanzi. Kwani nakumbuka aliniomba nimsaidie kupata laptop
kwa kazi zake, nami nilikuwa nataka kubadili kompyuta. Hivyo
nikamwakikishia nitaenda kumchagulia kompyuta nzuri ambayo ataipenda
maana alishachoka kuzunguka madukani bila mafanikio hadi akafikiria
kuagiza nje. Nilikwenda naye, na kumwonyesha kompyuta ambayo alipenda
hivyo tukanunua pamoja aina moja ya kompyuta.

Alikuwa mtu ambaye nilikuwa nimeshibana sana na nilifurahishwa sana
nae mara kwa mara tulipokuwa tukikutana. Tulisoma pamoja kozi ya mwaka
mzima ya uongozi ambayo ilizidi kutuweka karibu zaidi na zaidi. Mengi
tukifundishana na kuelekezana. Kozi tuliyoifanya mwaka 2006/2007.

Nakumbuka ni kipindi hicho na kuendelea ndipo alikuwa mstari wa mbele
katika kazi za kisiasa kupitia chama cha Chadema. Mara kwa mara
nilikuwa namwambia kuwa angalikuwa mbunge baada ya uchaguzi wa mwaka
2010. Jambo ambalo mara nyingi alikuwa akikwepa kulijadili kwa kina na
kuyeyusha kwa mizaha na pale nikimsisitiza kuwa sikuwa katika mizaha
aliishia kuniambia siasa ni safari ndefu lolote linaweza kutokea hivyo
tudumu katika kuombeana na utashi wangu mwema utimie.

Ifahamike, wakati namwambia hayo juu ya uwezekano wake kuwa mbunge
hakuwahi kuniambia juu ya kufikiria kusimama kugombea, na wala hakuwa
ameniambia juu ya jimbo la Kilombero.

Nilishawishika na uwezo, dhamira, jitihada alizokuwa nazo na hakika
kwa yeye kuwa katika siasa na kufanya kazi za chama kwa kujitolea na
kujituma niliona ni miongoni mwa vigezo muhimu sana ambavyo vilimpatia
zaidi na zaidi uwezo na ufahamu wa kisiasa hivyo nilitaraji yeye
kugombea na kushinda mwaka 2010. Maneno yangu kwake daima yalikuwa
msukumu kumuonyesha kuwa anaweza na kama alikuwa akisita kuthubutu
apate ujasiri wa kusonga mbele.

Na mwaka 2010, ndipo aliniambia dhamira yake ya kuingia moja kwa moja
katika siasa. Kusimama katika jimbo na kushindana. Taarifa hiyo kwangu
ilikuwa furaha kuu. Nilimwamini, na kuwa na uhakika angalifanya vizuri
na kuibuka kidedea.

Ukiwa mwaka wa mikiki mikiki mingi kisiasa, licha ya majukumu mengi,
alidumu kuwasiliana nami na kubadilishana mawazo hapa na pale. Na
hatimaye hata dakika za mwisho za kusubiri matokeo nilikuwa na furaha
sana kuona amemudu kufanya vyema. Licha ya kutotangazwa mshindi.
Hakika Regia alikuwa mwakilishi imara wa wanakilombero.

Nilifurahi zaidi nilipoona orodha ya wabunge rasmi wa Chadema kupitia
viti maalumu jina lake likiwamo, nakumbuka nilikutana nae na kwa
furaha niliishia kumwambia; “unakumbuka lakini nilikwambia utakuwa
mbunge?!” yeye hakujibu neno bali kicheko tu na kunirushia matani ya
hapa na pale.

Uwakilishi wa kibunge aliutumikia vyema pasi kuchoka, akijituma licha
ya changamoto nyingi zilizopo katika uendeshaji wa siasa zetu nchini.
Hakukata tamaa na kurudi nyuma. Hakuacha kujifunza, hakuacha kuwa
msikivu!

Ni mapambano haya ya kuleta mabadiliko katika jimbo la Kilombero ndiyo
pia yalimsukuma Regia kuja na wazo la kuwa na vuguvugu “movement” ya
maendeleo ndani ya Kilombero. Katika mwaka wa kiuchaguzi alikuwa
tayari akitumia kauli ya; “Kilombero for Change” (Kilombero kwa
Mabadiliko). Nakumbuka tulikutana na kujadiliana juu ya umuhimu wa
kupiga hatua ya kutoka kuwa “movement” na chombo rasmi, kuwa taasisi
kwa jina la Kilombero for Change. Jambo ambalo baada ya siku kadhaa
aliniomba nilisimamie mwanzo mpaka mwisho kuhakikisha chombo
kinasajiliwa na kuanza kujiendesha. Kazi ambayo niliipokea na kuitenda
kwa uaminifu mkubwa nikijua nasaidia mabadiliko kwa wanakilombero na
zaidi namsaidia rafiki yangu katika kutekeleza ndoto aliyonayo.

Ingawa bado shirika halikufikia hatua ya kusajiliwa, lakini tulimudu
kukamilisha taratibu zote zilizostahili katika usajili kama Katiba,
nembo, jina na vingine vingi tuliweza kuvikamilisha nikisaidiwa na
marafiki wa karibu katika harakati. Tukiwa tunasubiri jambo moja tu,
orodha ya majina ya watu ambao aliwaamini walikuwa imara kuanza
kutenda kazi katika ngazi ya wajumbe wa bodi. Mara kwa mara nikiwa
namkumbusha juu ya kukamilisha mchakato wa kuanzisha taasisi, alikuwa
msikivu na kunikumbusha pia umuhimu wa kuhakikisha anapata watu wazuri
katika bodi na si bora watu tu kutimiza hitaji la uanzishwaji wa
taasisi.

Licha ya majukumu mazito ya kibunge, daima alikuwa mwepesi katika
mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii na hata simu yake. Alikuwa
mshirika imara na mwepesi kushughulikia jambo hasa upatikanaji wa
taarifa au nyaraka kwa wakati. Nilimtegemea sana kwa hili na yeye
hakuniangusha daima.

Kwangu daima aliendelea kuwa rafiki wa karibu zaidi hata ya nyadhifa yake!

Najaribu kutafakari maneno ya Jim Reeves katika wimbo wake wa; “This
world is not my home”! Siamini maneno haya sasa yanarindima kwa rafiki
yangu Regia.

Licha ya majonzi nafarijika sana kwa Regia kumudu kufanya mengi katika
umri wake mbichi wa ujana.

Amemudu hata kuthubutu kuingia katika siasa tena kupitia upinzani na
zaidi kugombea kiti cha ubunge kupitia jimbo! Wengi sana wamekuwa
wakiahirisha uamuzi na kusubiri miaka ipite kwanza. Wengi kwa kuwa
wanawake wamekuwa wakirudi nyuma na kuacha kugombea kupitia majimboni.
Amemudu kuishi na kuitumikia nchi, si tu  katika harakati kupitia
mashirikia ya watu wenye ulemavu bali katika kutunga sheria na
kuisimamia serikali. Amejitahidi kurejesha matumaini na fikra mbadala
kwa wanakilombero, kwa vijana,  kwa wanawake na zaidi kwa watu wenye
ulemavu. Amedhihirisha inawezekana!

Licha ya nafsi zetu binadamu kutokumudu kuhimili majonzi na simanzi
zito na kuishia kuanguka katika kilio, naamini Regia huhitaji machozi
yetu sana sasa kama unavyohitaji sala zetu. Daima nitakuweka katika
sala zangu. Daima tumuweke katika sala zetu!

Pole sana kwa Remija natambua uchungu ulio nao kwa kupoteza pacha
mwenzako. Pole sana baba na mama, najua mpo katika simanzi na majonzi
makuu ya kumpoteza kijana wenu. Ni uchungu gani kumlaza kijana mbichi
kama Regia!Mungu awape faraja na moyo wa saburi. Pole kwa familia
nzima ya Regia, ndugu, jamaa na marafiki. Naamini ni kipindi kigumu
sana, tuweka tumaini letu kwa MUNGU.

Makamanda wote wa CHADEMA poleni sana. Kwa namna ya kipekee John
Mnyika (MB) ambaye amekuwa  chachu, taa na muongozo mkubwa kisiasa kwa
Regia,pole sana. Mwenyekiti Mbowe na Katibu Mkuu Dr.Slaa, Makamu
Katibu Mkuu Zitto na viongozi  wengine wote pamoja na maafisa na
watendaji wa chama Makao Makuu poleni sana. Kamanda alisimama kidete,
alipambana, hivyo daima tunu kubwa itakuwa kuendeleza mapambano;
Hakuna Kulala Mpaka Kieleweke!

Poleni sana wananchi wa jimbo la Kilombero!

Poleni sana wabunge na bunge zima kwa ujumla!

Zaidi poleni sana wananchi wote wa Tanzania.

“Even though crying is a human act that helps in healing our pains in
our souls…now Regia needs much our prayers than tears”!! (Hata kama
kulia nikitendo cha kibinadamu kinachosaidia kutuliza maumivu katika
roho…sasa Regia anahitaji zaidi sala zetu zaidi ya machozi!)

Kwa kheri Kamanda! Ulale mahala pema peponi.

© Michael Dalali, 14.01.2012

__._,_.___