MATOKEO YA KIDATO CHA PILI YATANGAZWA LEO.

MATOKEO YA KIDATO CHA PILI YATANGAZWA LEO.
Na Veronica Kazimoto – MAELEZO
Dar es Salaam
11/01/2013.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Philipo Mulugo
ametangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Elimu ya Sekondari Kidato
cha Pili mwaka 2012, ambapo kiwango cha ufaulu kimepanda kutoka
asilimia 45.40 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 64.55 mwaka 2012.

Matokeo hayo yametangazwa mbele ya waandishi wa habari leo jijini
Dar es Salaam ambapo idadi ya watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani
walikuwa 430,327, kati yao wasichana walikuwa 205,476 na wavulana
224,851, ikiwa ni upungufu wa watahiniwa 36,240 ikilinganishwa na
mwaka 2011 ambao walikuwa 466,567.

“Watahiniwa 386,271 sawa na asilimia 89.76 ya waliosajiliwa, walifanya
mtihani wakiwemo wasichana 187,244 na wavulana 199,027, watahiniwa
44,056 sawa na asilimia 10.24 hawakufanya mtihani, kati yao wasichana
ni 18,231 na wavulana 25,825” amesema Mulugo.

Aidha Waziri Mulugo amefafanua kuwa watahiniwa 136,946 ambao
wameshindwa kupata wastani wa ufaulu wa alama 30 na wale waliofutiwa
matokeo yao kutokana na udanganyifu watalazimika kukariri kidato cha
pili mwaka 2013.

“Ni vema ikaeleweka kuwa kukariri kidato si adhabu bali ni kutoa fursa
nyingine kwa mwanafunzi kuweza kupata maarifa, stadi na ujuzi wa elimu
ya sekondari, hivyo ni matumaini yangu kuwa wanafunzi hawa watafanya
bidii katika kujifunza na kuzingatia masomo ili waweze kufaulu masomo
yao katika kiwango kinachotakiwa” amesisitiza Mulugo.

Mtihani wa Taifa wa Elimu ya Sekondari Kidato cha Pili ulifanyika
nchini kote kuanzia tarehe 05 Novemba, 2012 na kumalizika tarehe 16
Novemba, 2012 kukiwa na jumla ya vituo 4,304 vilivyosajili watahiniwa,
sawa na ongezeko la vituo 117 ikilinganishwa na ile ya mwaka 2011.

MWISHO.