Maalim Seif alikuwa mtu wa kipekee Zanzibar


*Alikuwa wa pili kuanzia Rais Jumbe alipoachia madaraka, hadi kifo

Na Anil Kija
KIFO cha Seif Sharif Hamad, akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kimebadili sura ya siasa Visiwani humo kuwa ya kawaida zaidi. Kipindi cha siasa Visiwani kuanzia mwaka 1984, mwezi Aprili alipoondolewa madarakani Rais Aboud Jumbe Mwinyi na CCM, Maalim Seif amekuwa na nafasi ya kipekee ambayo hakuna mtu anayeweza kujaza, kwani haiwezekani mazingira ya nafasi hiyo yakaundwa tena. Ni kipindi cha kuinua misingi ya demokrasia Zanzibar, na kuunganisha nchi.

Katika maelezo yake kuhusu maisha ya Maalim Seif na walivyoshirikiana kisiasa, akihojiwa na moja ya redio jijini dira za asubuhi, mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba alisema Maalim Seif alipata shahada ‘first class’ (daraja la kwanza) katika Taaluma ya Siasa na Utawala, daraja ambalo halifikiwi mara nyingi shahada za kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam au kwingineko. Utawala wa idara husika ulitaka abaki kuwa mkufunzi msaidizi na kuendelea na masomo ya juu, lakini Rais Jumbe akasema anamhitaji Zanzibar. Akawa msaidizi maalum Ikulu; hakuwahi kutoka ngazi hiyo.

Sheikh Jumbe alipoondoka madarakani Maalim Seif akawa tena siyo msaidizi ila kupanda kuwa Waziri Kiongozi, baada ya kupitia ngazi kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwa mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango katika Sekretariat ya CCM. Katika nafasi hiyo ikaonekana wazi kuwa anaweza kurithi nafasi ya juu zaidi ya urais Zanzibar siku ikiwa wazi, ila ikawa wazi mapema mno, pale Kamati Kuu ya CCM ilipokataa jina la Balozi Salim Ahmed Salim, wakati huo akiwa Waziri Mkuu, kuwa mgombea urais wakati Rais Julius Nyerere anastaafu. Wajumbe wakauliza ‘nini tatizo la makamu wetu,’ yaani Sheikh Ali Hassan Mwinyi.

Kwa vile Mwalimu alikosa jibu kwa swali hilo, ikabidi akubali na kuelekeza ‘basi aitwe huyo sheikh,’ na wakati huo Maalim Seif, akijua ana uwezo halisi wa kuongoza Zanzibar, na ana nguvu zaidi katika chama kuliko watia nia wengine, akapania kupata nafasi hiyo. Ila haukuwa mwelekeo wa Mwalimu na wengine kama Sheikh Thabit Kombo, kuwa kiongozi wa nchi awe mtu ambaye ameshatoka katika pilikapilika za ujana, anaweza kujituliza madarakani akawa msikivu, siyo (siku hizi tungesema) awe ‘anachati’ na simu. Kwa vile historia ilimtaka kwa jambo tofauti na maisha tulivu ya kiongozi wa juu serikalini, Maalim Seif akawa mkali, hivyo akakosana na wazee CCM, na kuanzia hapo akawa amefika mahali pale alipotakiwa.

Ukitumia mfumo wa fikra wa hekaya za Wayunani (Wagiriki siku hizi) unaweza kusema kuwa Maalim Seif alikuwa amebeba jiwe kama Sisyphus akilipandisha mlimani, na kila anapofika karibu na kileleni nguvu zinapungua, anateleza anaanguka, anaanza upya. Maisha ya Maalim Seif kuanzia mwaka 1987 ugumvi huo ulipozuka ilikuwa ni kupandisha jiwe la dhamira yake mwenyewe kuwa kiongozi, na kupitia kwake, kuwezesha wananchi wanaotokea kisiwa cha Pemba kuondoa ‘uteja’ wao kwa Unguja tangu yatokee mapinduzi mwaka 1964. Haikuwa suala la kuitenga Pemba bali kuwapa nafasi wajisikie vyema.

Kwa upande mmoja jitihada hiyo pia ilisaidia kuibadili CCM kwani suala la mlingano wa kimaendeleo na mgao stahili wa nafasi kiuongozi kati ya wakazi wa visiwa hivyo ulipanda chati kiasi fulani katika chama tawala, ila halikuwa jambo rahisi kuongelea. Hata hivyo kwa wale waliofuata baadaye hatua kwa hatua jambo hilo likaanza kufanyiwa kazi, kwanza kupitia hatua ya kulikataa kuwa halina maana, kuwa wote ni raia wa nchi moja au taifa moja la Zanzibar, halafu kuanza kukiri kuwa haliwezi kupuuziwa. Hivyo CCM ikaanza kuacha ‘ungangari’ wa usimamizi madhubuti wa mapinduzi na ‘Wakuraishi’ wa Unguja, ikaanza kukubali upepo mwanana upite, watu wachanganyike na kugawana madaraka, ndio Katiba Mpya ya 1984.

Hata hivyo wakati CCM inafikia mahali inaanza kushughulikia suala la mgawanyiko na mgongano kati ya wakazi wa visiwa hivyo, sura nyingine ya suala hilo ilishajengeka, ile ya uanaharakati unaounganisha suala hilo kwa upande mmoja, na mengine labda hata makubwa zaidi. La kwanza ni nafasi ya Zanzibar ndani ya Muungano ambako dhambi ile ile ya Upemba ikawa sasa inawatesa Wazanzibari takriban wote kwa suala la Muungano, yaani kama ambavyo Pemba ilikuwa inajusikia vibaya Zanzibar, na Zanzibar kwa jumla ilikuwa inajisikia vibaya katika Muungano. Kwa sababu gani? Jibu la Mwalimu kwa haraka ni lile la mazungumzo yake na waandishi wa habari Machi 1995 hoteli ya Kilimanjaro: ‘..ni ulevi, ulevi tu.’

Unaweza kwa maana hiyo ukasema kuwa maisha ya kisiasa ya Maalim Seif kuanzia mwaka 1984 hadi kifo chake miaka 37 baadaye ilikuwa ni kutawala mazingira ya kisiasa ya huo ‘ulevi,’ na pia kujitoa mhanga ili malengo ya kiitikadi, ya matazamio ya makundi makubwa ya watu kupitia chama ambacho alikiongoza na nafasi yake binafsi katika mfumo wa siasa wa Zanzibar, yasipotee. Jitihada yake haikuwa bure kwani CCM ilichukua hatua za dhati kuondoa kero halisi za maendeleo kwa upande wa wakazi wa Pemba, kwa mfano uonevu katika ununuzi wa karafuu, ambao ulipunguzwa au kuondolewa Maalim Seif akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais kipindi cha kwanza, 2010-2015. Kero hizo zimeendelea kufyekwa na hata bila yeye kuwepo katika awamu hii, ni wazi kuwa jitihada zake na mabadiliko katika CCM kimsingi yameondoa tatizo hilo. Imebaki suala la mipango madhuibuti ya uchumi, hasa ‘Blue Economy,’ kufaulu.
(mwisho)