Kushindwa kutambua na kushawishi uwapo wa viwanda vidogo vya kisasa vya chini vya majumbani (home based industries), kumekuwa chanzo cha changamoto ya mwendo goigoi wa ukuaji wa uchumi – Maida Waziri

Presentation CBE, Dodoma

Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nimefurahi sana kualikwa katika hadhara hii kuzungumza kuhusu ujasiriamali. Wakati nazungumza huo ujasiriamali nitaunganisha na Waraka Maalumu wa ushauri wa kisera kuhusu Viwanda vidogo vya chini vya majumbani ambao niliuwasilisha Serikalini. Waraka huu niliuandika kutokana na uzoefu wangu wa miaka 30 ya ujasiriamali na kwa kuangalia kasi ya wenzetu katika kuimarisha uchumi wa viwanda na ujasiriamali na mnyororo wa thamani hasa katika mazao ya kilimo.

Kutokana na muda niliopewa kuwa mdogo, Waraka huo maalumu wa ushauri wa kisera kuhusu viwanda vidogo vya majumbani ambao niliuandaa kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara nchini (TNBC) baada ya kumalizika kwa kikao cha 12 kilichofanyika Juni 25,2021, nitawagawia muusome kwa wakati wenu lakini kikubwa zaidi ni ukweli kuwa tukitaka kuwa na ufanisi wa biashara na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji tunahitaji kubadilika na hasa mabadiliko katika sera ya viwanda vidogo.

Kiukweli Msimamo wa Waraka huou maalumu wa ushauri kisera ni kwamba ipo haja kubwa ya kurejea katika sera, sheria na kanuni kuangalia udhaifu uliopo kuhusu viwanda vidogo vya chini vya majumbani (home based industries-cottage). Aidha kuangalia uhusiano unaostahili kuwapo wa kibiashara, ikiwamo mnyororo wa thamani wa bidhaa, ushirikiano na mahusiano ya kandarasi ili kuwezesha mzunguko sahihi wa kuwezeshana (wa kikongano) kati ya viwanda vidogo vya chini vya majumbani, viwanda vidogo vya chini, viwanda vya kati na viwanda vikubwa.

Ni kweli kwamba kwa kushindwa kutambua na kushawishi uwapo wa viwanda vidogo vya kisasa vya chini vya majumbani (home based industries), kumekuwa chanzo cha changamoto ya mwendo goigoi wa ukuaji wa uchumi hasa mnyororo wa thamani katika kilimo na bidhaa zake ikiwamo raslimali nyingine zilizopo ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi na kuzifanikisha kwa kuzingatia mnyororo husika wa thamani.

Mimi nilifikaje hapa je ni rahisi?

Nilianza kama machinga jijini Dar es Salaam kabla sijaanza kushona nguo kwa kuanzisha kiwanda kidogo nyumbani na cherehani zake mbili; pamoja na kuanzisha kiukweli hali hii haikuwa inatambuliwa kisera wala kisheria na hata kikanuni hivyo shughuli zangu hazikusajiliwa.
Ni baada ya miaka mingi na juhudi kubwa zilizokumbwa na changamoto lukuki niliweza kusajili kiwanda .

Mimi ni muumini wa kuanza kidogo, na kile ulichonacho. Ni ndoto yangu tukibadili mambo tutafika sehemu ambapo mtanzania anaweza akawa billionae kwa kufanya kazi/biashara, na kuwa innovative, hata kama ameanza chini kiasi gani, lakini yote haya yanawezekana kwa kuwa na sera na sheria, kanuni zinazoruhusu na kuwezesha kuanzia chini, viwanda vya majumbani.

Uzuri wa viwanda vidogo vya majumbani vinahitaji vitu vidogo sana kuanza, ambavyo wahusika wanavyo tayari. Mtafiti Stein Kristiansen anasema “Viwanda vidogo vya majumbani nchini Tanzania vina uwezo mkubwa wa kuendelea na kukua” mimi ni Ndoto yangu kama tukikubali kubadilika na kufikia kutambua viwanda vya majumbani kama taifa la India na Bhutan tutafika mahali kila Mtanzania anakuwa na uwezo wa kuanzisha biashara kutoka nyumbani kwake na kuikuza kufikia kiwanda kikubwa.

India wana mfano mzuri kabisa wa viwanda vya majumbani. Viwanda hivi vipo chini ya Wizara ya Viwanda vidogo vya chini, vidogo na vya kati (Ministry of Micro, Small & Medium Enterprises). Pamoja na kuwa na wizara hiyo India pia ina Wizara ya Viwanda na Biashara. Serikali ya India ina Wakala kadhaa wanaosaidia ukuaji wa viwanda vya majumbani na viwanda vidogo,miongoni mwa wakala huo ni Bodi ya Viwanda Vidogo, Kamisheni ya viwanda vijijini, nk.

Pakistan, majirani wa India wao asilimia 80 ya bidhaa na huduma mbalimbali huzalishwa na viwanda vya majumbani. na kwa kuwa kuwa Tanzania ipo katika mapambano makubwa ya kukuza uchumi wa kati unaotegemea viwanda na kwa kuwa uchumi wetu kwa sehemu kubwa unategemea kilimo kwa kuwa na sera na sheria hii kuhusu viwanda vya majumbani tutaneemeka.

Tuna mambo mengi tunaweza kufanya kwenye cottage industry hapa nyumbani kama ufumaji wa nguo, mafuta ya nazi, tomato source, clips, misumari, furnitures, majembe, usanii wa vinyago, uhunzi, utengenezaji wa viatu, vyungu, mashua, misumari, sabuni, batiki, mikate, maandazi, vitumbua na kadhalika. Sheria zilizopo, utaratibu wa kodi unafanya viwanda vya majumbani kuwa ni uhalifu.

Nataka kusema kwamba katika mazingira ya Tanzania ni muhimu kutofautisha viwanda vya majumbani kwa mfumo wa viwanda vidogovidogo vinavyotambulika kisheria na vya kati kama ilivyo kwenye sera ya viwanda vidogo na vya kati ya mwaka 2002/3.

Ukiangalia nilivyofanya shughuli za umachinga, kutumia kampuni za watu wengine kufanya shughuli ambayo naimudu utaona kwamba kama ingelikuwepo sera, sheria na kanuni za kunitambua na kunikiza ningemaliza kila kitu. Nimefanya masimulizi yangu kwa kina nilivyokua kibiashara kwa kuthubutu katika kitabu cha kesho yako ni uthubutu na changamoto zote hizo zimetokana na kukosekana kwa msaada wa kupambana na hali yangu.

Simulizi langu katika kitabu hicho ni miongoni mwa masimulizi ya watanzania wengi ambao hawana fedha za mtaji ambao wanajaribu kujiingiza kwenye biashara mbalimbali ili kujikimu. Juhudi zao zinakwamisha mara zote kutokana na sera, sheria na kanuni zilizopo ambazo hazitambui uwapo wa viwanda vidogo vya majumbani na wala kutoa njia ya kuvihudumia ili vikue. Na ndio maana ipo haja ya kurekebisha mazingira yanayoambatana na ufanisi wa viwanda vya aina hii katika sera, sheria na kanuni ili kuleta unafuu wa watu kuibua fursa za kuwa na viwanda majumbani.

Kwa mfano:
(i) Katika uchakataji wa chakula mahitaji na sheria kuhusiana na biashara hizo zinataka jengo lisajiliwe kama ilivyo katika kiwanda kidogo (SMEs). Mtu anatakiwa kutekeleza matakwa ya wakala wa Tanzania Chakula Dawa na Vipondozi kuhusu kanuni za usalama wa chakula za mwaka 2006 .
Hii ni adha kubwa kwa viwanda vya majumbani ambayo vinahitaji tu malighafi kutoka katika mazingira ya pale nyumbani au jirani. Kuna msururu wa sheria ambazo mtu anatakiwa kutekeleza kabla ya kuanza shughuli hiyo na taratibu zote hizo zinahitaji fedha za kutosha huku akitakiwa meneja aliyetoka chuoni. Ili kuweza kutekeleza masharti yote hayo mtu atahitajika kusafiri maeneo mbalimbali katika ofisi za tawala za mikoa na serikali za mitaa kwa vibali pamoja na wakala wengine wanaohusika na shughuli anayodhamiria kuifanya ambayo itamgharimu fedha na mtaji mkubwa.
(ii) Kutokana na haja ya kutaka kutambuliwa rasmi ( ili kuweza kupata misaada ya kifedha na masoko), biashara hiyo ni lazima iwe na utambulisho wa namba ya mlipa kodi ( Tax Identification Number- TIN). Zaidi ya hapo mhusika ni lazima aoneshe ni kiasi gani cha fedha za kodi atalipa kwa mwaka wa kwanza na kuanza kulipa kiasi cha mwanzo cha asilimia 25 ya makadirio ya mwaka katika kipindi cha miezi mitatu.
Utambulisho wa mlipa kodi kwa kawaida hufanywa bure katika ofisi iliyokaribu na Mamlaka ya Mapato (TRA). Lakini mpaka umepata utambulisho huo utakuwa umeshahangaika katika ofisi nyingi na hii inagharimu fedha na muda huku kukiwa na ukweli wa wazi kwamba wengi wanaoanzisha viwanda majumbani huwa hawana fedha au wakiwa wanazo ni kidogo sana.
(iii) Kwa uhakika viwanda vidogo vya majumbani hutegemea zaidi nguvu kazi ya familia (kaya) ambayo huenda isilipwe au inalipwa kwa mtindo wa familia kuweza kuendelea kupata mahitaji yake ya lazima, lakini sheria zilizopo zinamhitaji mwendeshaji wa kiwanda hiki kufuata sheria zote za kazi zikiwemo utoaji wa kiwango cha chini cha mshahara, ulipaji wa kodi, michango katika mifuko ya hifadhi na kadhalika.
(iv) Biashara ya viwanda vya majumbani huenda kwa kipindi kirefu isitengeneze faida lakini mwenye kiwanda hiki anatakiwa kufanya makadirio ya kodi na kulipa kodi hiyo mara tu atakapokuwa amepata namba ya utambulisho wa ulipaji kodi katika kipindi cha miezi mitatu tangu kusajiliwa kwake.
(v) Gharama ya kupata leseni ya biashara pekee kwa sasa ni Sh 50,000 inaweza kirahisi kabisa kuzidi mtaji wa anayetaka kuanzisha kiwanda cha majumbani, ambao mara nyingi hutegemea utaalamu wake, matumizi ya wanafamilia katika utengenezaji wa kitu husika, matumizi ya vifaa vya nyumbani na hata vifaa vya kuazima kutoka kwa ndugu au majirani.

MAONI YANGU

Tanzania ipo katika mapambano makubwa ya kuwa katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda. Kwa sasa uchumi wetu kwa sehemu kubwa unategemea kilimo. Uwapo wa viwanda vidogo vya majumbani ni msaada mkubwa wa kwanza kuongeza thamani ya bidhaa mbalimbali za kilimo hapa nchini na pia kuwa chachu ya kuwapo kwa mapinduzi ya viwanda na kuongeza fursa za ajira.

Sehemu kubwa ya bidhaa zinazozalishwa mashambani nchini Tanzania zinafaa kuwa malighafi kwa ajili ya viwanda vya majumbani. Hapa pia tunastahili kujiuliza ni tani ngapi za matunda huwa tunazitupa kwa kuharibika wakati wa msimu wa matunda. Kuwapo kwa viwanda vya majumbani kuna maana kwamba wakulima wanaweza kusindika matunda hayo katika hali mbalimbali na kuuza rojo lake kwa viwanda vya kati au hata vya chini. Mtu anaweza kuwa na friji nyumbani na mtambo wa kukaushia matunda na kutumia fursa zote hizo kibiashara, hata katika kiwango kidogo lakini hawawezi kufanya chochote kwa kuwa sheria zina masharti mengi ambayo wakulima wa kawaida na wanakaya hawawezi kumudu, hasa gharama zake.

Ili kuwapo na viwanda vya majumbani kuna haja katika sera ijayo ya maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati ( SME) kuingiza ndani yake viwanda vidogo vya majumbani. Mpaka naandika waraka huu kwa mujibu wa rasimu iliyotengenezwa Novemba 2020 , hakuna eneo lolote lililoonesha uwapo wa viwanda vidogo vya majumbani na mahitaji ya sheria mpya yatakayowezesha kutimia kwa ndoto za viwanda kwa mwananchi wa kawaida.

Hakika kuna haja ya sera ijayo ya MSME kuhakikisha kwamba inatamka waziwazi kuhusu maendeleo ya viwanda vya majumbani na kuweka sheria zake na kanuni zake ili kusaidia kuanzishwa kwa viwanda hivyo na kuboreshwa viwe vipo vijijini au mijini. Mengine katika sera na sheria ni kuundwa kwa Tume au Bodi ambayo itashughulika na viwanda vidogo vya chini vya majumbani. Tume au bodi hii itashughulika na kuweka mazingira bora na yenye muafaka kwa wananchi kuanzisha viwanda hivi vya majumbani ambapo pia vitawezesha kukua kwa viwanda vidogo. Kwa kuwa na Tume serikali itatambua kila mwaka ni viwanda vingapi vya majumbani vinaweza kupanda hadhi kuwa viwanda vidogo katika mfumo wa SMEs.

Kunatakiwa sheria inayoruhusu na kuhalalisha uwapo wa viwanda vidogo majumbani. Hii maana yake ni kuondokana na sheria zote zikiwemo za kikoloni zinazopiga marufuku uwapo wa viwanda vidogo vya majumbani ambazo vinafanya uzalishaji na uchakataji.

SIDO , ambayo ilianzishwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge na kuwajibika kuwawezesha wahitaji wa viwanda vidogo na vya yanatakiwa kuongeza maelezo kuhusu viwanda vya majumbani ili kuwezesha viwanda vya majumbani kupata huduma wanazohitaji katika kuanza na kuviendeleza. Ni muhimu kwa taasisi hii kupewa fursa na serikali kutoa huduma kwa viwanda vidogo vya majumbani nchini kote. Na hili linatakiwa kuelezwa kinaga ubaga katika sera mpya inayotengenezwa kuhusu viwanda vidogo vikiwemo vya majumbani.

Tusione aibu kuazima sera ya viwanda vidogo na vya majumbani ya taifa la Bhutan ya mwaka 2019 , ikisimama yenyewe kama sera ya Wizara ya Uchumi ya Falme ya Bhutan. Kuna haja kubwa ya kusahihisha makosa yetu ambayo tumekuwa tukiyafanya tangu kupata uhuru hadi sasa kuhusiana na suala la uwezeshaji wa fursa za viwanda vya majumbani kisera, kisheria na kikanuni.

mwisho