Kilimo cha umwagiliaji salama ya familia maskini

Na Mariam Juma:

“Nilishindwa kuendelea na masomo baada ya baba kufariki, mama akasema
kilimo kitatusaidia nirudi shuleni, mama amelima na mvua hakuna na mazao
yamenyauka nahisi ndoto za kurudi shuleni zimekatika,’’ alisema mtoto
Fikiri Joachimu(9) mkazi wa kijiji cha Kibombo kata ya Nyakasana wilayani
Karagwe mkoani Kagera.

Ni mtoto mdogo, lakini unaona kwamba pamoja na udogo wake anafahamu kabisa
kwamba uwezo utatokana na kupatikana kwa mazao.

Kwa wakazi wa karagwe ambao wengi wao hufanya kilimo cha kutegemea mvua za
msimu wa vuli na masika kunapotokea mabadiliko huathiri sana familia hasa
zile maskini wa kipato.

Ni kutokana na kuwapo kwa athari za aina hiyo ipo haja ya kuanzisha na
kuimarisha kilimo cha umwagiliaji.

Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 ambayo katika ibara ya 34 kifungu
kidogo cha (a) hadi (f) imesisitizwa kutumia kilimo cha umwagiliaji kwa
ajili ya kukuza uchumi wa taifa na wananchi katika kipindi hiki kwa
kuongeza uhakika wa upatikanaji wa chakula nchini, inaweza kuwa dira ya
msukumo kwa viongozi wa mkoa wa kagera na wilaya zake zenye kutindikiwa na
mvua na kusabisha usalama wa chakula kuwa shakani.

Mpango mkakati wa miaka mitano wa Sekretariet ya Mkoa wa Kagera ambao
ulisisitiza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara utokane na Kilimo
cha Umwagiliaji utaweza kuokoa familia kama za akina Joachimu.

Sekretarieti ya Mkoa wa Kagera inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera
(Mh.Col RTD Fabian Massawe) pamoja na Katibu Tawala Mkoa (Bw.Nassor
Mnambila) umeamua kusimamia utekelezaji wa Sera, Miongozo na Maelekezo yote
ya Serikali Kuu kuhusu sekta ya kilimo cha umwagiliaji.

Pamoja na kutekeleza usimamizi kuna changamoto zilizojitokeza katika
utekelezaji wa mikakati ya kilimo cha umwagiliaji kwa msimu wa mwaka
2010/2011 kwa 2012/2013

Moja ya changamoto kubwa ni bajeti ndogo ya uwekezaji katika kilimo cha
umwagiliaji, Uwezo na ushiriki mdogo wa taasisi binafsi katika maendeleo ya
kilimo cha umwagiliaji, Ujuzi na uwezo mdogo kwa wakulima na Halmashauri za
wilaya kuhusu kilimo cha umwagiliaji.

Mambo mengine ni ukosefu wa mifumo bora ya kuendeleza kilimo cha
umwagiliaji, kukauka kwa vyanzo vya maji kunakosababishwa na mabadiliko ya
tabia nchi na upungufu wa wataalamu wa umwagiliaji katika Halmashauri za
wilaya.

Mmoja wa wakulima ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kigarama kata ya Igurwa
katika wilaya ya Karagwe Bw. Katabaro Byalimpa alieleza kuwa, Kilimo cha
umwagiliaji kimekuwa ni Changamoto kutokana na jiografia iliyopo katika
wilaya hizo, hivyo kushindwa kuanzisha kilimo hicho ambacho alikiri kuwa ni
muhimu.

“Kilimo cha Umwagiliaji katika wilaya yetu kimekuwa ni gumzo tu kwani
ukiangalia jiografia ya wilaya zetu ni milima hivyo kwa nguvu za wananchi
tu itakuwa vigumu kumudu kilimo hicho,’’ alisema Byalimpa.

Alieleza kuwa, kuna suala la wakulima kuridhika na kidogo wanachokipata na
kutopenda kujihusisha zaidi kupata kipato zaidi katika kilimo ni tatizo pia.

Naye Mwalimu mstaafu Dominic Rugaikamu mkazi wa kijiji cha Rwanyango
ambaye pia ni mkulima, alisema kuwa suala la kuanzisha kilimo cha
umwagiliaji kinawezekana kutokana na uwepo wa vyanzo vya maji kwa baadhi ya
maeneo.

“Mathalani kijiji cha Kakanja kuna bwawa ambalo lina maji kwa muda mrefu na
halitumiki na wananchi hawaelewi matumizi sahihi ya maji hayo, ikiwa
litatengenezwa kwaajili ya kilimo cha umwagiliaji maji hayo yataweza
kusaidia vijiji vya Rwanyango, Kimuli, Kakanja na Rwele,’’ alisema
Rugaikamu.

Aidha alisema:,“kilimo hicho kinaweza kunyanyua uchumi wa wakazi wa wilaya
ya Kyerwa kwa sababu sasa wanakwenda kwenye ushindani wa kibiashara
kutokana na kujengwa soko la kimataifa katika kijiji cha Nkwenda’’.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kata ya Mabira, Daud Serestin alisema kuwa,
wanaweza kuwa na kilimo cha umwagiliaji kwani maji yapo ya kutosha ikiwa
yatadhibitiwa.

Aliongeza kuwa:“msimu uliopita tulishindwa kuvuna ipasavyo kutokana na
uhaba wa mvua na sasa kama unavyoona mazao yamekauka kwa kukosa mvua, kwani
hata Raisi Jakaya Kikwete alipotembelea hapa alihamasisha kilimo cha
umwagiliaji’’.

Mhandisi kilimo na mratibu wa DASIP mkoani Kagera, Msafiri Magugu katika
taarifa yake alisema maeneo ya Bukoba-Kyabalamba, Missenyi-Kyakakera na
Ngono, Karagwe-Mwisa na Karazi, Ngara-Rulenge, Biharamulo-Mwiluzi,
Muleba-Kyamyorwa, Buyaga, Buhangaza na Kyota yamefanyiwa utaratibu wa
miradi ya kilimo cha umwagiliaji.

Wachambuzi wa mambo wanasema Sheria ya Umwagiliaji ya mwaka 2013
iliyopitishwa mwishoni mwa mwezi Agosti itaipa sekta ya kilimo nguvu mpya
katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Waziri wa Kilimo na chakula wa Tanzania, Christopher Chiza, aliliambia
bunge kwamba sheria mpya italeta fikra mpya kwa nchi katika kutumia shamba
kama rasilimali katika kilimo endelevu cha umwagiliaji.

“Tutatumia kila tone la maji lililopo nchini mwetu kuendeleza kilimo cha
umwagiliaji hadi kufikia mwaka 2015 angalau asilimia 25 ya chakula lazima
itoke katika kilimo cha umwagiliaji,” alisema.

Waziri alisema, serikali kwa sasa inatekeleza miradi 39 ya umwagiliaji
kwenye ekari 16,710 ikitumia teknolojia ya umwagiliaji ya dondoka kwa
gharama ya Tsh 677.5 billion (Zaidi ya dola za kimarekani million $400).

Wakulima wa Mkoa wa Kagera wanajishughulisha na kilimo kwa asilimia 70
katika msimu wa kilimo cha vuli na asilimia 30 kwa kilimo cha msimu wa
masika; katika msimu wa kilimo 2012/2013 mvua za Vuli 2012 zimechelewa
kuanza katika maeneo mengi ya Mkoa na sasa hali ya jua imeendelea kuutafuna
mkoa huo.

Hata hivyo Mkoa umejiwekea lengo la kulima na kutunza jumla ya hekta
712,890 za mazao mbalimbali ya chakula zinazotarajiwa kuzalisha jumla ya
tani 1,495,550 za ndizi, tani 337,540 za nafaka, tani 139,760 za mikunde,
na tani 1,135,680 za mazao ya mizizi.

mwisho