Kilimo cha chikichi kikiendelezwa jibu kwa umaskini wa wakulima

Na Fadhili Abdallah:
CHIKICHI ni moja ya mazao yenye soko kubwa hapa duniani na kama
litatumiwa na kuendelezwa vizuri linaweza kuwa moja ya njia nzuri za
kuwaondoa wakulima wadogo katika lindi la umasikini.

Ipo mifano mingi ambayo inaonyesha kwamba nchi zilizotumia zao la
chikichi ambalo hutumika kuzalisha mawese zimeweza kufanikiwa katika kuinua
kipato cha wananchi wake na kusaidia kuingia taifa mapato
makubwa.

Malaysia moja ya nchi zilizo katika bara la Asia ni mfano wa kuigwa
katika hilo kwani nchi hiyo imeweza kutumia zao la chikichi katika
kusaidia wakulima wake na sasa ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kuuza
mafuta ya mawese kwa wingi duniani.

Zitto Kabwe Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini mkoani Kigoma
anaandika katika mtandao wake kuwa chikichi ni zao la ukombozi kwa
wananchi wa kipato cha chini kama serikali ya nchi husika itaweka
kipaumbele na mkakati madhubuti katika kutumia zao hilo kama moja ya
mazao ya biashara ya na mazao ya kiuchumi kwa nchi.

Nakubaliana na Zitto kuhusiana na hali hiyo, kwani hivi karibuni
nimefanya ziara kwa wakulima wa zao la chikichi katika vijiji
mbalimbali vya mkoa Kigoma na nimethibitisha kwamba serikali haijaweka
mkakati madhubuti wa kuinua zao hilo na kulifanya zao ambalo linaweza
kuwakomboa wakulima.

Katika mahojiano na wakulima na wazalishaji wa zao hilo wanaeleza
kilio chao kwa serikali na Halmashauri kwa namna ambavyo hawapati
msaada wowote katika kuwafanya kuliendeleza zao hilo.

Kiza Kassim mzalishaji wa mawese katika kijiji cha Mahembe Halmashauri
ya wilaya Kigoma anasema kuwa amefanya kazi hiyo kwa miaka 25 sasa
lakini kikubwa anachopata ni pesa ya kula bila kuwa na ziada ya
kufanya maendeleo.

Anasema kuwa kwa mfano akinunua ngazi za shilingi 150,000 ambazo ni
pipa 4 na nusu za lita 200 huzalisha mafuta ya mawese lita 120 ambazo
huuza dumu moja la lita 20 kwa kiasi cha kati ya shilingi 3,000 na
shilingi 40,000 ambapo kwa mwezi huweza kuzalisha mara tatu.

Anaeleza sababu kubwa ya kuendelea kuzalisha kidogo na kupata kiasi
kidogo namna hiyo ni kutokana na kutokuwa na zana bora za uzalishaji
na wamekuwa wakizalisha kienyeji kwa muda wote.

Kiiza anasema kuwa serikali imekuwa kimya katika kuona namna gani
inawasaidia wakulima kwa kuwapa ushauri mbalimbali wa kuimarisha zao
la chikichi na ndiyo maana wameamua kufanya namna wanavyoona inafaa
ili kuingiza hata hicho kiasi kidogo wanachopata.

Mzalishaji mwingine wa Mawese katika kijiji cha Mahembe, Mamisho Seif
Ruyange anasema kuwa uwezeshaji umekuwa tatizo kubwa kwao na kwa
upande wake amefanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka saba lakini hakuna
mahali popote ambapo ameweza kupata mkopo au ruzuku ya kuimarisha
uzalishaji wa mawese.

Anasema kuwa mahali pekee ambako pamekuwa na msaada kwao nio katika
vyama vya kuweka na kukopa ambapo wamekuwa wakichangishana na
kukopeshana wenyewe hapo kijijini kwao.

Mamisho anaeleza kuwa amekuwa akitumia pesa zake kwa ajili ya kufanya
kazi hiyo lakini faida imekuwa siyo kubwa ya kuweza kumfanya aione
kazi hiyo ndiyo mkombozi pekee na ndiyo maana pamoja na uzalishaji wa
mawese inabidi wajiingize pia kwenye kilimo cha mazao mengine.

Anasema kuwa anaweza kukodi shamba la michikichi kwa kiasi cha
shilingi milioni 2 kwa mwaka ambapo anaweza kuzalisha dumu 100 za lita
20 ambazo bei hutegemea na hali ya soko kwani huweza kufikia hadi
shilingi 45,000 kwa dumu na wakati mwingine hushuka hadi shilingi
25,000 kwa dumu la lita 20.

Naye Jasmin Hassan mkulima wa michikichi katika kijiji cha
Chankabwimba, Kigoma Vijijini anasema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa
wakitegemea kuvuna ngazi (matunda ya chikichi yanayotumika kuzalisha
mawese) kutoka katika mashamba ambayo wamerithi kutoka kwa Baba na
babu zao.

“Mashamba ni yale yale ya tangu enzi za babu zetu hakuna mbegu mpya
ambazo tumeweza kupanda, kila tukiuliza Halmashauri tunaambiwa
halmashauri inatengeneza vitalu vya mbegu bora lakini miaka inakatika
na hakuna jipya,”anasema Jasmin.

Mkulima mwingine wa kijiji cha Msimba anasema kuwa enzi za Mkuu wa
mkoa aliyemaliza muda wake katika utumishi wa umma, Elmon Mahawa
serikali ilianza kuonyesha njia katika kuimarisha zao hilo lakini
tangu aondoke na hilo limekufa.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mahembe anasema kuwa tatizo kubwa ni mashine
za kusindika mawese kwani kwa muda mrefu wananchi wamekuwa
wakihangaika na uzalishaji wa kienyeji ambao hutumia nguvu nyingi
lakini tija yake ni ndogo.

Anatoa mfano wa kijiji kwao kwamba zilisimikwa mashine za kusindikia
mawese lakini uzalishaji unaofanyika na gharama zake umewakatisha tama
wananchi na ndiyo maana kwa sasa mashine hiyo imefungwa na wanaendelea
kuzalisha kienyeji.

Diwani wa kata ya Mahembe eneo ambalo limekuwa na uzalishaji mkubwa wa
mawese mkoani Kigoma, Habibu Ramadhani Hebeye anailaumu serikali kwa
kushindwa kuchukua nafasi yake kuliwekea mkazo zao hilo.

Hebeye anasema kuwa mambo matatu yamelifanya zao hilo kutoweza kuwa na
thamani kwa wakulima ambapo ameanza na uzalishaji wa mbegu bora
limekuwa tatizo kubwa licha ya yeye kama diwani kukutana na watendaji
wa halmashauri mara nyingi kuzungumzia jambo hilo.

Jambo la pili ambalo diwani huyo analizungumzia ni mashine za
kuzalisha (kusindika) mafuta ya mawese ambapo katika zao la michikichi
bila kuwepo kwa mashine hizo uzalishaji wa mawese hauwezi kuwa na
tija.

Katika wilaya nzima ya Kigoma anasema kuwa hakuna mashinde ya
kuzalisha mawese hivyo kufanya wazalishaji wa mawese kubaki katika
kutumia mtindo wao wa kuzalisha kienyeji.

Aidha anazungumzia suala la masoko ambapo anasema kuwa kwa sasa
mkulima wa michikichi na mzalishaji wa mawese hawafaidi kwa chochote
na zao hilo zaidi wanaofaidika ni wanunuzi ambao hupita nyumba kwa
nyumba na kununua mawese na mwisho wa siku huyasafirisha kuuza nje ya
mkoa.

“ukusanyaji wa mawese nao ni wa kienyeji mno na ili Halmashauri ipate
mapato kutokana na zao hilo imebidi kuweka mawakala ambao imebid
kufanya kazi wakati wote kuzuia utoroshaji wa mafuta hayo usiku ili
waweze kupata mapato kutokana na zao hilo,”anasema kuwa Diwani huyo.

Zitto Kabwe mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini ambaye alitembelea
Malaysia kuona na kujifunza namna nchi hiyo ilivyoweza kufaidika na
kilimo cha Michikichi na kuweza kuwa moja ya nchi zinazoongoza kwa
kusafirisha nje ya nchi yao kiasi kikubwa cha mawese na hivyo
kuiingizia nchi hiyo fedha za kigeni.

“Malaysia iliunda Shirika la Umma linaloitwa Federal Land Development
Authority (FELDA) likiwa na wajibu mmoja mkubwa wa kuhakikisha
wananchi masikini wanapata ardhi, wanalima kisasa na kuongeza
uzlishaji kisha kufuta umasikini,”anasema Zitto.

Anaongeza kuwa kila mwananchi masikini aligawiwa ardhi hekta 4.1,
ardhi ikasafishwa na kuwekwa miundo mbinu yote muhimu, ikapandwa
michikichi na Mwananchi akapata huduma za ugani ili kukuza michikichi
hiyo.

Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini anasema kuwa Shughuli zote hizi
zilifanywa kwa gharama za Serikali na wananchi wale wakapewa kama
mkopo ambao walikuwa wanaulipa kidogo kidogo kila wanapovuna na kuuza
ngazi/ mawese kwa Shirika hili la Serikali.

“Hivi sasa Shirika hili ni kubwa sana, lina thamani ya dola za
kimarekani bilioni 3.5 na kupitia Ushirika wao wananchi hawa waliopewa
ardhi ya kulima michikichi sasa wanamiliki asilimia 20 yaShirika
hili,”Zitto anasema aliyoyaona huko.

Zitto alisema kuwa Malaysia iliweza kuondoa umasikini kutoka asilimia
57 ya wananchi wanaoishi kwenye dimbwi la umasikini mwaka 1965 mpaka
chini ya asilimia 3 mwaka 2012.

Mbunge huyo anasema kuwa serikali inapaswa kuweka mipango ambayo
itasaidia wakulima wadogo kutumia mashamba yao kuendelezwa na
kuzalisha kwa tija kuanzia uzalishaji wa mazao ya chikichi shambani
hadi kuwekewa mashine za kuzalisha mawese wakakopeshwa na baadaye
kulipa taratibu.

Katika utafiti wangu mdogo nilioufanya kuhusu kudumaa kwa zao la
michikichi kuwamboa wakulima na lindi la umasikini nimegundua kuwa
mashine ni moja ya vikwazo vikubwa kwa wakulima katika kufikia
mafanikio kutumia zao hilo.

Meneja wa shirika la viwanda vidogo (SIDO) mkoa Kigoma, Gervas
Ntahamba anasema kuwa shirika lake limekuwa likihangaika kwa muda
mrefu kuona nanna gani linapata teknolojia rahisi ya bei nafuu ambayo
wazalishaji wa mawese wataitumia katika kuzalisha mawese mkoani
Kigoma.

Ntahamba anasema kuwa baada ya kuhangaika kwa muda mrefu mwaka huu
wamefanikiwa kuzindua mashine moja ya kuzalisha mawese ambayo ina seti
ya mashine tatu kwa ajili ya zao la Michikichi.

Anasema kuwa mashine hizo tatu kwa pamoja zinauzwa shilingi milioni 15
na tayari mashine ya kwanza imefungwa katika kijiji cha Ilagala wilaya
ya Uvinza ambayo ilinunuliwa na mradi wa maendeleo ya bonde la ziwa
Tanganyika (PRODAP) kwa ajili ya wazalishaji mawese katika eneo hilo.

Meneja huyo wa SIDO Kigoma anaeleza kuwa ni wazi bado wakulima wadogo
hawana uwezo wa kumudu kununua mashine hizo na kwamba serikali kupitia
Halmashauri za wilaya zinazo kazi za kuona inaweka mkakati wa
kuhakikisha mashine hizo zinafika kwa wakulima.

Nilipata nafasi ya kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
wilaya ya kigoma, Miriam Mbaga ambaye anakiri kuwa bado serikali
haijaweka mkakati wa makusudi katika kuinua kilimo cha michikichi na
uzalishaji wa mawese mkoani Kigoma.

Mbaga anasema kuwa wakati mwingine hiyo inatokana na vipaumbele vya
watawala waliokuwepo kipindi hicho hasa Wakurugenzi wa halmashauri
katika kuweka vyanzo vya mapato kwa halmashauri zao.

Mkakati wa uboreshaji wa zao la michikichi hadi kufikia uzalishaji wa
mawese kwa mbegu bora kama ukianza sasa unaweza kuchukua miaka mitano
kuja kuanza kuvuna kutoka katika mbegu hizo baadhi ya viongozi kwao
wanaona inachukua muda mrefu kuweza kupata mapato kwa halmashauri zao.

Kwake yeye akiwa ndiyo amemaliza mwaka mmoja na nusu tangu aweze
mkurugenzi katika halmashauri hiyo ameshaweka mikakati mbalimbali ya
kuinua zao la michikicha na uzalishaji wa mawese.

Anataja moja ya mipango hiyo ni kuanzisha uzalishaji wa mbegu bora kwa
kushirikia na chama cha wakulima wa michikichi (KIPAFADA) ambao
amewapatia kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kutekeleza
mkakati huo.

Sambamba na hilo Mbaga anasema kuwa Halmashauri imetenga kiasi cha
shilingi milioni 50 kwa ajili ya ununuzi wa mashine za kukamulia
mawese ambazo zitafungwa katika eneo la Mahembe.

Mkurugenzi huyo anakiri kuwa kwa sasa hakuna soko rasmi la mawese na
Halmashauri ili iweze kupata mapato yake imebidi kuweka mawakala ambao
hukusanya ushuru kutoka kwa wanunuzi kwenye baadhi ya vizuizi ambavyo
vimewekwa.

Tunazo historia kwamba Malaysia ilitoa mbegu za Michikichi kutoka
kijiji cha Ilagala wilaya ya Uvinza na sasa imekuwa tajiri kutokana na
kuweka mkakati na kutumia zao hilo kama moja ya njia zake kuu za
kiuchumi za kuingizia nchi mapato.

Ni dhahiri kwamba umefika wakati sasa serikali ione umuhimu wa kuinua
zao la chikichi ambalo mawese yanaozalishwa yanayosoko kubwa ndani na
nje ya nchi.

Miaka mitano nyuma kampuni ya Murzah Oil Mills iliwahi kuja mkoani
Kigoma kwa ajili ya kununua mawese badala ya kununua mawese nje lakini
imeondoka kutokana na hali halisi ya upatikanaji wa mawese ulivyo.

Moja ya mambo makubwa ambayo yaliwakimbiza ni kiwango kidogo cha
mawese kinachokusanywa kutokana na wao kuhitaji zaidi ya behewa 10 kwa
wakati mmoja na ili mzalishaji awe na mzigo mkubwa suala la ubora
likaanza kuchakachuliwa.

Inaelezwa kuwa moja ya mambo ambayo wauzaji wa mafuta ya mawese
waliyokuwa wakifanya ni kutia maji au kuweka mafuta ambayo
hajakamuliwa vizuri na mwisho wa siku kampuni hiyo ikaona jambo hilo
ni hasara kwao na kuendelea kuagiza mafuta nje yenye ubora ambao
wanaoutaka.

Mwisho.