Inakuhusu sana uwe kwenye ndoa au unaelekea, soma

From Jamii Forums, Dar es Salaam:
Inahuzunisha lakini kuna fundisho kuu kwetu sote.
“Nilipofika nyumbani usiku ule, mke wangu aliponitayarishia chakula,
nilimshika mkono na kumwambia, Kuna kitu nataka nikwambie. Mke wangu
alikaa chini na kula chakula kimya akiwa tayari kunisikiliza. Tena
nikagundua macho yake yalionyesha anaumizwa. Nilishindwa hata namna ya
kuanza kufumbua kinywa changu. Lakini ilibidi nimwambie ili ajue
nilikuwa nikifikiri nini juu yake.

Nataka kukupa talaka. Nilianza kusema kwa utulivu. Alionekana
kutokereka na maneno yangu badala yake aliniuliza kwa sauti ya upole
‘kwa nini?’ Sikumjibu swali lake. Kutojibu kulimfanya akasirike.
Akatupa kijiko na akanikaripia, ‘wewe si mwanamume!’ Usiku ule,
hakukuwa na maongezi kati yetu. Alikuwa akilia kwa kwikwi. Nilifahamu
kwamba alitaka kujua ni nini kimetokea kwenye ndoa yetu. Lakini kwa
hakika nisingeweza kumpa jibu wala sababu ya kuridhisha; alionekana si
mali kitu kwangu penzi langu lilihamia kwa Jane. Sikumpenda tena mke
wangu mawazo yote yalikuwa kwa Jane. Kwa kweli nilimdharau mke wangu!

Huku moyo wangu ukijua wazi kwamba nafanya kosa, niliandika talaka
ambayo ilionyesha kwamba yeye (mke wangu) angepata nyumba yetu, gari
na atakuwa na hisa 30% ya kampuni yetu. Aliangalia talaka ile na
kuichana vipande vipande.

Mke ambaye tumeishi nami kwa miaka 10 alionekana mgeni machoni mwangu.
Nilimuonea huruma kwa muda, rasilimali na nguvu alizopoteza lakini
sikuweza kurudi nyuma kwa sababu Jane aliuteka moyo wangu kisawasawa.
Hatimaye mke wangu alilia kwa sauti mbele yangu, jambo ambalo kwa
hakika nilitarajia. Kwangu mimi kilio chake kilinipa nafuu.

Wazo la kuachana na mke wangu limenisumbua kwa majuma kadhaa na sasa
limeendelea kuimarika na kuwa jambo la hakika zaidi.

Siku iliyofuata nilikuja nyumbani kwa kuchelewa sana nikakuta mke
wangu akiandika jambo mezani. Sikutamani hata kula chakula
alichonipikia nilikwenda moja kwa moja chumbani na usingizi
ulinichukua mara moja kwa sababu nilikuwa nimechoka baada ya kula raha
za kufa mtu na Jane.

Usiku nilishtuka usingizini mke wangu alikuwa bado akiandika. Sikujali
kabisa nikajifunika vyema shuka na kulala tena. Asubuhi yake
alinikabidhi masharti ya talaka yake: hakutaka kitu chochote kutoka
kwangu lakini alihitaji apate angalau mwezi mmoja wa kujiandaa kabla
hajaachika. Akaomba kwamba katika kipindi hicho cha mwezi mmoja sote
mimi na yeye tujitahidi kuishi maisha ya upendo au kawaida kwa kadiri
itakavyowezekana. Sababu yake ilikuwa ndogo lakini muhimu: mwanetu wa
kiume alikuwa akikaribia kufanya mtihani katika mwezi uliofuata kwa
hiyo hakupenda mtoto aathirike kisaikolojia kwa sababu ya kuachana
kwetu. Hili halikuwa tatizo kwangu, nilikubali mpango wake. Lakini
alikuwa na sharti la ziada, aliniomba nikumbuke jinsi nilivyombeba
siku za fungate yetu hasa siku ya harusi yetu. Akaniomba na kunisihi
kwamba katika kipindi hicho cha mwezi mmoja niwe nambeba kutoka
kitandani kwetu mpaka mlango wa kutokea kila asubuhi. Nilidhani
anakaribia kuwa kichaa. Ili kufanya siku zetu za mwisho zisiwe na
migogoro nilikubaliana na masharti yake ya ajabu.

Nilimsimulia Jane kuhusu masharti ya kuachana na mke wangu. Jane
alicheka sana, aliona ni ujinga. ‘Hata akitumia ujanja wa namna gani
talaka ni lazima’, alisema Jane tena kwa dharau. Mimi na mke wangu
hatukuwahi kugusana tangu nilipomweleza dhamira ya kumtaliki. Kwa hiyo
nilipombeba kwa mara ya kwanza sote tulinuniana. Mwanetu alifurahi
sana na kupiga makofi nyuma yetu, ‘aah baba kambeba mama mikononi
mwake’. Maneno yake yalinichoma moyoni moja kwa moja. Kutoka chumbani
kwetu hadi sebuleni, halafu tena mpaka mlangoni, ni zaidi ya mita kumi
nimembeba mke wangu. Alifumba macho na kusema kwa sauti laini na ya
upole; usimwambie mwanetu juu ya talaka. Nilikubali kwa kichwa, ingawa
nilijisikia vibaya. Nilimuweka chini nje ya nyumba.

Alienda kituoni kusubiri basi la kazini kwake nami nikaendesha gari
kwenda ofisini kwangu. Siku ya pili, zoezi lilikuwa rahisi kwetu sote.
Aliegemea kifuani pangu. Nilisikia harufu nzuri ya uturi aliofukiza
kwenye blauzi yake. Nikagundua kwamba sijamuangalia kwa makini mke
wangu kwa kipindi kirefu sana. Nikagundua hakuwa binti tena. Kulikuwa
na mikunjo usoni na nywele zake zilianza kuwa nyeupe! Ndoa yetu
imekula urembo wake. Kwa dakika moja nikafikiri kwa nini namfanyia
hivi.
Siku ya nne nilipombeba hisia za mapenzi kati yetu zilirejea. Huyu ni
mwanamke aliyejitoa kuishi nami na tumeishi kwa miaka kumi sasa. Siku
ya tano na ya sita ilikuwa wazi kwamba mapenzi yetu yalikuwa yakimea
upya. Sikumwambia Jane kuhusu jambo hili. Kadiri mwezi ulivyokaribia
kwisha niliona raha kumbeba mke wangu na zoezi likawa rahisi zaidi.
Pengine kufanya kazi hii kila siku kuliniimarisha zaidi.

Alikuwa akichagua nini cha kuvaa asubuhi. Alichagua mavazi kadhaa
hakupata linalomfaa. Kisha akaguna, ‘nguo zangu zote zimekuwa kubwa’.
Nikagundua kwamba mke wangu amepungua sana, nadhani ndiyo maana
niliweza kumbeba kirahisi. Ghafla jambo likanichoma… mke wangu ana
uchungu na maumivu makuu moyoni mwake. Bila kujitambua nikamgusa
kichwa chake. Mara mtoto wetu akatokeza na kusema ‘baba ni wakati wa
kumbeba mama muende kazini’. Kwake kumuona baba akimbeba mama likawa
ni jambo la furaha sana. Mke wangu alimuonyesha ishara mwanetu asogee
karibu na akamkumbatia kwa upendo mkuu. Niligeuza uso wangu nisije
nikabadili mawazo katika dakika ya mwisho. Kisha nikambeba mikononi
mwangu kutoka chumbani, sebuleni halafu mpaka mlangoni. Mkono wake
laini ulikuwa umeizunguka shingo yangu kwa upendo. Nilimkumbatia mwili
wake; ilikuwa ni mithili ya siku ya ndoa yetu. Lakini wepesi wake
ulinitia mashaka.
Siku ya mwisho nilipombeba nilipata shida hata kupiga hatua moja.
Mtoto wetu alishakwenda shuleni. Nilimshika kwa karibu na kumwambia
sikubaini kwamba maisha yetu yalikosa upendo. Nikaenda zangu ofisini….
Nikashuka garini hata bila kufunga mlango. Maana nilihisi nikichelewa
tu ninaweza kubadili nilichoamua…. nikapand ngazi. Jane alifungua
mlango nikamwambia, ‘Samahani, Jane, sihitaji tena kumtaliki mke
wangu’. Akaniangalia kwa kustaajabu, halafu akagusa kichwa changu.
Akaniuliza ‘Unaumwa?’ Nikaondoa mkono wake kichwani kwangu. ‘Samahani,
Jane, nimesema sitaki kumtaliki mke wangu. Nadhani ndoa yangu haikuwa
na furaha kwa sababu sikuthamini undani wa maisha yetu, mimi na mke
wangu, si kwamba hatupendani. Nimetambua hilo tangu nilipombeba siku
ya ndoa yetu nilitakiwa kumbeba siku zote za maisha yetu, nampenda mke
wangu sitamuacha mpaka kifo kitakapotutenganisha.’

Ikawa kama Jane alizinduka usingizini. Akanizaba kibao cha nguvu,
akajiegemeza mlangoni na kuanza kulia. Nikashuka ngazi na kuondoka
zangu. Nikaingia kwenye duka la maua nikaagiza maua mengi mazuri kwa
ajili ya mke wangu. Muuzaji akaniuliza aandike nini kwenye kadi.
Nikatabasamu na kuandika “Nitakubeba kila asubuhi mke wangu mpaka kifo
kitakapotutenganisha”. Jioni ile nilifika nyumbani na maua mikononi
mwangu, tabasamu kubwa usoni nikakimbia mpaka chumbani, nikapokelewa
na maiti ya mke wangu kitandani.
Kumbe mke wangu alikuwa akisumbuliwa na saratani kwa miezi kadhaa nami
nilishindwa kubaini kwa sababu nilihamishia akili yangu kwa Jane.
Alijua kwamba angekufa karibuni na alitaka asiniingize katika chuki na
mwanetu kama ningelazimisha talaka mapema.
Angalau machoni mwa mwanangu naonekana ni mume mwema…

Jamani vitu vidogo vidogo vizuri ni vya msingi sana katika mahusiano
yetu… Siyo majumba au magari au fedha zilizoko kwenye benki. Hivi
vitakupa tu mazingira ya kufurahi lakini vyenyewe siyo furaha. Kwa
hiyo jitahidi kuwa na muda mzuri na mazingira rafiki ya kuwa na mwenzi
wako, kuwa rafiki wa mwenzi wako. Fanya vitu mlivyofanya wakati wa
uchumba na wa ndoa yenue ambavyo vitawaweka karibu siku zote. Muwe na
ndoa yenye furaha. Mara nyingi watu hushindwa katika ndoa kwa
kutotambua ni kwa kiasi gani walikuwa karibu wakati wa kujenga
uhusiano wao
Mungu awabariki nyote mliosoma na kujifunza hapa