HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI MHE. JOHN JOHN MNYI

BAJETI YA MWAKA 2010/2011 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA
NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012 UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika; awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kuniwezesha kuwasilisha maoni haya ya kambi rasmi ya upinzani kuhusu
makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa
fedha 2011/2012 kwa mujibu wa kanuni za Bunge (Toleo la mwaka 2007)
kifungu cha 99 (7) ikiwa ni sehemu ya kuchangia katika wajibu wa bunge
wa kuishauri na kuisimamia serikali.

Mheshimiwa Spika; Nawashukuru wananchi wenzangu wa jimbo la Ubungo kwa
kuniamini bila kujali tofauti zingine na kunituma kuwawakilisha kwa
kunitunuku heshima ya kuwa mtumishi wa umma. Nawashukuru pia kwa
kunipa madiwani wa kufanya nao kazi. Asanteni wazee kwa busara zenu,
wanawake kwa sala zenu na vijana wenzangu tuliokuwa pamoja kipindi cha
kampeni na kukesha wote Loyola katika kulinda ushindi.

Tumeandika historia kwamba hakuna hujuma inayoweza kudhibiti nguvu ya
umma (people’s power) mabadiliko yameanza kuonekana na kwa pamoja
tuendelee kutimiza wajibu kwa kurejea dira yetu: A.M.U.A; Maslahi ya
Umma Kwanza.

Mheshimiwa Spika; Nawashukuru wanafamilia yetu ya Dalali; wazazi wangu
na ndugu zangu kwa upendo wenu ambao umechangia katika furaha yangu na
motisha ya kuendeleza ujasiri na uadilifu katika kusimamia ukweli,
haki na ustawi.

Mheshimiwa Spika; Natambua kwa shukrani mchango wa viongozi wenzangu
wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) makao makuu, Mkoa wa
Kinondoni Kanda Maalum Dar e salaam, Jimbo la Ubungo na wa kambi rasmi
ya upinzani bungeni katika hatua ambayo tumefikia; mahitaji na
matumaini ya watanzania yanatutaka tuendelee kuongoza kwa umoja,
umakini na uwajibikaji mpaka kieleweke dhidi ya ubinafsi, uzembe na
ufisadi ambao unazidi kushamiri katika taifa letu.

Mheshimiwa Spika; Nawashukuru wote katika mamlaka ambao mmenipa
ushirikiano kwenye serikali kuu, manispaa ya Kinondoni, katika kamati
ya nishati na madini na wabunge wengine kwa ujumla katika kutekeleza
majukumu ya kibunge kwa manufaa ya taifa letu na watu wote.

Mheshimiwa Spika; Wizara ya Nishati na Madini ambayo tunatolea maoni
bajeti yake leo ni wizara nyeti sana katika taifa letu nyakati za sasa
na kwa vizazi vijavyo. Sekta ya nishati ni moyo wa taifa wakati madini
ni mtaji wa nchi yetu.

Tanzania imejaliwa rasilimali nyingi watu, ardhi yenye rutuba , maji
(bahari, mito na maziwa), kuwa katika eneo la kimkakati la kijiografia
kwa biashara, mali asili ikiwemo za utalii na madini. Hata hivyo,
tunaelekea kuwa na laana ya rasilimali hali ambayo inafanya wananchi
walio wengi kuendelea kuwa katika lindi la umasikini na wakiendelea
kusukumwa pembezoni nje ya urithi ambao taifa linao.

Mheshimiwa Spika; Tishio la usalama na amani katika taifa letu kwa
sasa sio migomo wala maandamano bali ni migogoro inayoendelea ya
kirasilimali maeneo mbalimbali ya nchi ambayo ni bomu la wakati
litakalolipuka iwapo kasi ya ukuaji wa uchumi wenye kutoa fursa kwa
wengi haitaongezwa. Sekta ya nishati ni moyo wa kurekebisha hali hii
na sekta ya madini ni mtaji wa kufanikisha dhamira hiyo.

Mheshimiwa Spika; tunakutana leo ikiwa ni miezi michache kuelekea
kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru taifa likiwa gizani kutokana na mgawo wa
umeme unaoendelea, idadi ndogo ya watanzania waliounganishwa kwenye
gridi ya taifa na matatizo ya sekta ya nishati kwa ujumla. Tunakutana
wakati ambao urithi wetu mkuu ambao mababu zetu waliupigania wakati wa
kudai uhuru; ardhi na rasilimali zake ikiwemo madini ukiwa mashakani
kutwaliwa na kutawaliwa kwa ubeberu mamboleo.

Mheshimiwa Spika; Mnamo tarehe 21 Juni 2011 Bunge lilipitisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha
2011/2012 ambapo wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani tulipiga kura ya
HAPANA; lakini ikapita kutokana na uwingi wa wabunge wa upande wa pili
bila kuzingatia maslahi ya umma.

Tulipiga Kura ya HAPANA kwa kuwa ilikuwa ni bajeti yenye maneno matupu
bila matendo katika mipango na utekelezaji; athari za bajeti hiyo
zimeshaanza kudhihirika kwenye uchumi wa nchi na maisha ya wananchi wa
kawaida. Bajeti ya mwaka 2011/12 ilielezwa kwa maneno matupu kuwa
imeweka nishati kuwa ni kipaumbele cha kwanza. Hata hivyo vitabu vya
Bajeti ya Serikali iliyopitishwa vinadhibitisha ukweli mchungu kwamba
jumla ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya nishati na madini ni bilioni
539.3 tu.

Kwa mujibu wa Vitabu vya Bajeti ya Serikali 2011/2012 iliyopitishwa,
Wizara ya Nishati na Madini imetengewa jumla ya shilingi 402.4 bilioni
kwenye Fungu 58. Fedha hizo zimegawanywa katika mafungu ya Matumizi
shilingi 76,953,934,000 na bajeti ya Maendeleo zimetengwa shilingi
325,448,137,000 tu. Fedha nyingine kidogo za maendeleo bilioni 126.6
zipo kwenye Fungu la 50 miradi ya MCC kwa kutegemea wahisani.

Hivyo; bajeti hii haijaichukulia kwa uzito unaostahili sekta za
nishati na madini hususani umeme hali ambayo inaibua maswali iwapo
serikali ina dhamira ya dhati ya kukabiliana na changamoto za msingi
zinazolikabili taifa hivi sasa.

Mheshimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani imepitia kitabu cha pili cha
matumizi ya kawaida ya Wizara ya Nishati na Madini ( Volume II Supply
Votes) Fungu la 58 vifungu 1001-1009, 2001-2012 na 3001 na kubaini
kwamba hii ni bajeti ya mgawo mkubwa wa posho na ufujaji. Mathalani
Idara ya Kitengo cha Mawasiliano katika kulipana posho zitatumika Sh.
Milioni 405.62 sawa na asilimia 63% ya fedha yote iliyotengwa Sh.
Milioni 641.99 kwa idara hii.

Idara ya fedha na uhasibu itatumia Sh milioni 598.49 sawa na asilimia
42% ya fedha yote iliyotengwa. Kanda ya Ziwa – Mwanza kulipana posho
inatumia Sh. milioni 389.68 sawa na asilimia 40% ya fedha yote
iliyotengwa. Kuna posho kuwanunulia mavazi wafanyakzi wanao safiri nje
ya nchi, sherehe na maonesho, chakula na vinywaji, huduma kwa wageni,
posho za kukaimu nafasi na posho nyingine.

Kwa ujumla Wizara ya Nishati na Madini inakadiriwa kutumia Sh. Bilioni
7.9 kulipana posho na matumizi mengine ya kawaida ya anasa. Kwani
jumla hii ni nje ya posho za msingi kama vile; posho za uhamisho,
posho za mafunzo, nyumba, maji na umeme.

Kambi Rasmi ya Upinzani inataka serikali ifanye marekebisho kwenye
bajeti ili fedha hizi zipunguzwe ziweze kuongezwa kwenye kuongeza
ujenzi wa miundombinu wa Chuo Cha Madini Dodoma na na kuongeza kiwango
cha fedha katika mfuko wa wachimbaji wadogo wa madini. Aidha yako
matumizi mengine ya ujenzi wa maofisi na gharama kubwa za kisheria
ambayo yanapaswa kuhamishiwa katika miradi muhimu ya maendeleo ikiwemo
ya umeme vijijini.

Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe kwamba tarehe 15 Juni 2011 Kambi ya
upinzani iliwasilisha bajeti mbadala ambayo ilitenga fedha za kutosha
katika kukabiliana na changamoto za sekta za nishati na madini. Bajeti
mbadala ilitenga fedha za maendeleo Sh. Bilioni 977 kwa ajili ya
Wizara ya Nishati na Madini ukilinganisha na ile serikali iliyotenga
Sh. Bilioni 452 kwa maendeleo (Fungu 58 na 50); ambayo ni sawa na
ongezeko la zaidi ya asilimia 100 (100 %).

Kambi rasmi ya upinzani inataka kiwango cha bajeti ya Wizara ya
Nishati na Madini kuongezwa ili vipaumbele vifuatavyo viweze
kuzingatiwa kwa uzito unaostahili: · Kuwekeza fedha za kutosha kwenye
sekta ya umeme na Gesi ili kumaliza kabisa tatizo la nishati ya Umeme
na kupunguza gharama za maisha. Hatua hizo ziambatane kuwekeza katika
Bomba la Gesi kutoka Mtwara, pamoja na ujenzi wa mtambo wa kutengeneza
Gesi (LPG extraction Plant) ili kuwezesha gesi kutumika kwenye magari,
viwandani na majumbani. ·

Kuhakikisha tunazalisha 360MW za umeme kila mwaka ili kufikia malengo
ya Mpango wa Maendeleo wa miaka Mitano na kumaliza tatizo la mgawo wa
umeme. Kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya usafirishaji na
usambazaji wa umeme vijijini ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi
vijijini.

Mheshimiwa Spika; Tunatambua kwamba wakati wote serikali imekuwa
ikitoa visingizio kuwa kiasi cha fedha kilichopo ni kidogo na hivyo
kutegemea zaidi fedha za wahisani. Hivyo, kambi rasmi ya upinzani
imewasilisha vyanzo vya mapato ambavyo vinaweza kutumika kuongeza
kiwango cha bajeti kwa ajili ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.
Baadhi ya misingi muhimu ya mapato ambayo tumeiwasilisha ni pamoja na:
· Kupunguza misamaha ya Kodi ikiwemo kuondoa msamaha wa ushuru wa
mafuta Kampuni za Madini peke yake kutaongeza mapato ya shilingi
bilioni 59. ·

Kutoka Vyanzo vipya vya mapato tulivyovianisha; kwa upande wa sekta ya
madini kwa Kurekebisha Kodi Sekta ya Madini peke yake tunaweza
kukusanya shilingi bilioni 240 katika mwaka wa fedha 2011/2012. ·
Kupunguza fedha kwenye Wizara zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya
kawaida yasiyokuwa ya lazima na kuelekeza fedha katika miradi ya
maendeleo hususani ya umeme na gesi.

Mheshimiwa Spika; katika muktadha huo pamoja na kifungu cha 106 cha
Kanuni za Bunge kutenguliwa kuruhusu sheria ya fedha 2011 kupitishwa
tarehe 22 Juni 2011; ni muhimu mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati
na Madini uhusishe pia kupitia kitabu cha kwanza cha mapato (Volume 1-
Revenue Estimates) ili kuongeza wigo wa mapato.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuzingatia maoni na
mapendekezo yanayoendelea kutolewa na kuwasilisha marekebisho
(amendments) ya sheria ya fedha ili kuongeza wigo wa mapato. Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka kuwasilisha bajeti ya Nyongeza
(Supplimentary budget) kwa ajili ya Wizara ya Nishati na Madini ili
kuwa na makadirio ya nyongeza ya matumizi kwa mujibu wa kanuni 107 kwa
ajili ya miradi ya umeme na gesi asilia.

Umeme Mheshimiwa Spika; Tatizo sugu la mgawo wa umeme ambalo sasa
limekomaa na kuwa janga la taifa limetokana na ufisadi na udhaifu wa
kiuongozi na kiutendaji ambao umeikabili sekta ya nishati nchini
kuanzia awamu ya pili, likaongezeka katika awamu ya tatu na kukomaa
katika awamu ya nne ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ufisadi na udhaifu huo wa kiutendaji unajidhihirisha zaidi katika
maamuzi mbalimbali yaliyofanyika awamu ya pili hususani 1990 mpaka
1995; awamu ya tatu hususani 1996 mpaka 2004 na awamu ya hususani 2006
mpaka 2011 kwenye maamuzi na mikataba mbalimbali mathalani kashfa ya
IPTL, hasara ya mchakato wa ubinafsishaji wa TANESCO, uzembe wa Net
Group Solution, ufisadi wa Kiwira, kashfa ya Alstorm Power Rentals,
sakata la Songas/Pan African Energy, ufisadi wa Richmond, madhara ya
Dowans (ambayo sasa mitambo yake iko chini ya Symbions bila serikali
kutoa kauli, kashfa kuhusu mitambo hiyo zimekwisha baada ya umiliki
kuhamia kwa kampuni ya Marekani na iwapo taratibu za zabuni
zilifuatwa) ambapo mkazo haukuwekwa katika mipango ya muda mrefu ya
kuondokana na tatizo la mgawo wa umeme nchini ambayo imetajwa bayana
katika nyaraka mbalimbali za mipango ya kiserikali.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na maamuzi ya Bunge la tisa ya kuhusu masuala
hayo bado kambi ya upinzani inataka hatua kamili kuchukuliwa kwa
wahusika wa kashfa hizo kama walivyotajwa kwenye orodha ya mafisadi
ili kujenga msingi wa kuepusha hali kama hiyo kujirudia katika
uwekezaji unaondelea hivi sasa.

Mheshimiwa Spika,athari za upungufu wa umeme kwenye uchumi wa nchi na
maisha ya wananchi ni makubwa sana. Taarifa za Serikali zinaonyesha
kwamba Mamlaka ya Mapato inapoteza mapato ya Bilioni 840 kwa mwaka
kutokana na mgawo wa umeme na ripoti za wadau wengine zimeeleza bayana
upungufu wa ajira unaosababishwa na mgawo wa umeme.

Mheshimiwa Spika; Ikumbukwe kwamba katika mkutano wa pili wa Bunge
kikao cha sita tarehe 15 Februari 2011 Waziri wa Nishati na Madini
alitoa kauli bungeni kuhusu mipango ya dharura ya serikali kupunguza
tatizo la mgawo wa umeme. Kati ya hatua ambazo zilielezwa ni
ukodishaji wa mitambo ya dharura ya MW 260 na kuongeza matumizi katika
mitambo ya IPTL.

Kambi rasmi ya upinzani imefadhaishwa na taarifa iliyotolewa kwa umma
na TANESCO wakati wa kuanza kwa mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa
kuwa umechangiwa na mitambo ya IPTL kuzalisha chini ya kiwango
kutokana na upungufu wa mafuta mazito (HFO) suala ambalo linatosha kwa
serikali kuwajibika kutokana na uzembe wenye kulitia hasara taifa kwa
sababu suala hili lilikuwa likijulikana kwa miezi mingi bila hatua
stahili kuchukuliwa.

Mheshimiwa Spika; Tarehe 1 Aprili 2011 Rais Jakaya Kikwete alitoa
ahadi kupitia hotuba yake kwa taifa kwamba mitambo ya MW 260
ingekodishwa na kuanza kufanya kazi mwezi Julai kukabiliana na mgawo
wa umeme.

Kambi ya Upinzani haijaridhika na visingizio ambavyo vimekuwa
vikitolewa na serikali kwa kutumia sababu za matatizo ya nje ya nchi
kuelezea uzembe wa kiutendaji wa kushindwa kusimamia maamuzi ya ndani
na inaitaka Wizara ya Nishati na Madini ieleze kwa uwazi na ukweli
sababu za kuchelewa kwa mpango huo na hivyo kuongeza kwa kiwango
kikubwa muda na kiwango cha mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa.

Mheshimiwa Spika; kwa upande mwingine mgawo wa umeme unaoendelea hivi
sasa ni matokeo ya serikali kushindwa kutekeleza kwa wakati mpango wa
kuweka mitambo ya MW 100 Ubungo (Dar es salaam) na MW 60 Nyakato
(Mwanza) ambayo iliwekwa kwenye mpango wa umeme wa mwaka 2009 ambao
ulicheleweshwa na hatimaye wakati wa Bajeti ya mwaka fedha 2010/2011
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na Madini wote waliahidi kukamilisha
uwekaji wa mitambo hiyo mapema mwaka 2011. Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka serikali ieleze sababu za kuchelewa kutekelezwa kwa mpango
huo na hatua za uwajibikaji zilizochukuliwa kutokana na udhaifu huo.

Mheshimiwa Spika; Ni aibu kwa taifa kuendelea kutegemea vyanzo ambavyo
vilianzishwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Hayati
Mwalimu Nyerere na awamu zilizofuata sio tu kushindwa kuongeza kasi ya
kuzalisha umeme bali pia kushindwa kukarabati mitambo hiyo na hivyo
kuzalisha chini ya kiwango. Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2010
inaonyesha kuwa vituo vyetu vya umeme vinazalisha 3694.74 jigawati kwa
saa yaani MW 421.8 sawa na asilimia 53.5 ya uwezo wa vituo hivyo MW
788.68.

(Rejea Kielelezo cha Pili). Sababu zinazotolewa za uzalishaji kidogo
ni uchakavu wa mitambo na ukame unaoliathiri taifa. Kambi ya Upinzani
inaishauri serikali kuacha kuwalaghai wananchi kwa sababu zisizo za
msingi kwani ikumbukwe kwamba zipo nchi zilizo katika hali ya jangwa
lakini vituo vya kuzalisha umeme vina uwezo wa kuzalisha umeme wa
wastani wa zaidi ya asilimia 90.

Mheshimiwa Spika; Mwaka 2010 Serikali ilieleza kupitia taarifa ya hali
ya uchumi kwamba mahitaji ya umeme yalifikia MW 791 na Waziri wa
Nishati na Madini akatoa matumaini hewa kwa wananchi kupitia bajeti ya
mwaka 2010/2011 kuelekea uchaguzi kwa kutaja miradi ambayo jumla yake
iliahidi uzalishaji wa MW 2,960; hata hivyo serikali haikutenga fedha
za kutosha kufanikisha mipango husika au walau kuweka mazingira
wezeshi kwa taasisi zingine na sekta binafsi kwa ujumla kufanikisha
utekelezaji hali ambayo imejirudia tena katika bajeti ya mwaka wa
fedha 2011/2012.

Mheshimiwa Spika; Kutokana na hali hiyo ya mgawo wa umeme unaoendelea
na kasi ndogo ya usambazaji wa umeme vijijini na majibu yaliyotolewa
na Serikali kupitia kwa maswali ya papo kwa papo ya Waziri Mkuu tarehe
14 Julai 2011 yameonyesha kwamba serikali halichukulii tatizo la umeme
kwa udharura na uzito unaostahili. Hivyo, kambi rasmi ya upinzani
inatoa hoja kwa bunge kupitisha azimio la kutangaza kwamba ukosefu wa
nishati ni janga la taifa na kupitisha maamuzi ya hatua za haraka
ambazo serikali inapaswa kuzichukua kwa uwajibikaji wa pamoja.

Bunge lichukue nafasi yake kwa niaba ya wananchi kwa mujibu wa katiba
ibara ya 63 (2) (3) ili kuisimamia serikali kuondoa janga hili la
taifa; maazimio ya bunge yatawezesha taarifa za mara kwa mara kutolewa
bungeni kuhusu hatua za utekelezaji na adhabu kutolewa kwa mawaziri wa
serikali watakaozembea katika kuchukua hatua za haraka.

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Taifa wa miaka mitano
(2011/2012-2015/2016) umelenga kuongeza uzalishaji wa umeme mpaka
kufikia MW 2780 kwa kuongeza MW 1788 kwa mujibu wa miradi iliyotajwa
kwenye mpango. Lengo hili ni dogo ukilinganisha na rasilimali ambazo
zipo katika taifa letu; hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
serikali kufanya mapitio ya mpango huo na kuongeza miradi mingine
mikubwa ukiwemo wa Stiggler Gorge ambao una uwezo wa kuzalisha MW 2100
na kuingiza pia makadirio ya ujumla ya MW zinazotokana na miradi
midogo midogo itakayoanzishwa katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani imebaini kwamba hata lengo
hili dogo la MW 1788, ambalo ni sawa na ongezeko la wastani wa MW 360
kila mwaka; halijaanza kutekelezwa kwa ukamilifu. Hii ni kwa sababu
katika mwaka wa fedha 2011/2012 serikali imepanga katika bajeti
kuongeza MW 160 ambazo kimsingi zilipaswa ziwe zimekamilika mwaka wa
fedha 2010/2011.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kueleza mradi mwingine wa MW
200 ambao unapaswa kukamilika katika mwaka huu wa fedha na rasilimali
zilizotengwa kwa ajili ya kufanikisha mradi husika. Kambi Rasmi ya
Upinzani inasisitiza kwamba mradi wa Kiwira wa MW 200 awamu ya kwanza
upewe kipaumbele maalum katika mwaka huu wa fedha ili kuweza kuziba
pengo lililopo. Kambi rasmi ya Upinzani inataka kauli ya serikali
kuhusu pendekezo letu la kutenga fedha za ndani kutekeleza mradi wa
njia za kusafirisha umeme huo kutoka Kiwira mpaka Mbeya katika mwaka
wa fedha 2011/2012 .

Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza miradi iliyosalia kwa wakati Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara ya Nishati na Madini kueleza
mazingira wezeshi ambayo yanakusudiwa kuandaliwa ili miradi ifuatayo
iweze kupata rasilimali kwa wakati na makubaliano kukamilishwa mapema:
Dar es salaam-Kinyerezi (Gesi Asilia MW 240), Iringa-Mchuchuma na
Ngaka (Makaa ya Mawe-300), Mtwara – Somanga Fungu (Gesi Asilia-MW 300)
na Morogoro/Iringa- Ruhudji (Maji- MW 358).

Mheshimiwa Spika, Uchambuzi wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Taarifa
ya Utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2010/2012 na makadirio ya bajeti ya
mwaka wa fedha 2011/2012 unaonyesha uwezo mdogo na kasi ndogo ya
kufikisha umeme vijijini. Mathalani katika bajeti yake ya mwaka huu
Wizara imetenga Sh Bilioni 1.1 kupeleka umeme katika vijijini 4 tu
( Kijiji cha Magindi, kijiji cha Mbwewe, Kijiji cha Mgwashi, kijiji
cha Kiwanga) kati ya vijiji 12,176 vilivyosajiliwa kutokana na taarifa
ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Kwa hali hiyo itachukua karibu miaka elfu mia mbili sawa na karne
mbili kufikisha umeme katika vijiji vyote; kama ambavyo tumetumia
miaka 50 ya uhuru kuunganisha umeme kwa 14% tu kwenye gridi ya taifa.
Kasi ndogo ya kusambaza umeme inadhihirishwa na idadi kubwa ya maombi
ya wananchi wanaotaka kufungiwa umeme huku Shirika la Umeme (TANESCO)
likiwajibu kuwa halina uwezo kwa sasa mpaka lipate miradi.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2010/2011 Serikali
iliahidi kutekeleza Mradi wa MCC (Millenium Challenge Cooperation) wa
kuvipatia umeme vijiji 289 katika mikoa 6. Mwanza (42), Tanga (129),
Dodoma (45), Mbeya (18), Iringa (17) na Morogoro (38). Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka serikali kutoa taarifa ya kina ya utekelezaji
kutokana na malalamiko ya kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi kwa
kulinganisha na kiwango cha fedha kilichotumika. Aidha tathmini
ifanyike kuhusu utekelezaji wa mradi husika ili kuwezesha umeme kuweza
kufika vijijini kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani tulieleza kwenye bajeti
mbadala 2011/2012 kwamba Kipaumbele chetu cha muhimu ni Kuwezesha
Ukuaji wa Sekta za Uzalishaji na hasa ukuaji wa uchumi vijijini ili
kuboresha kilimo, kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani
za bidhaa, kuongeza ajira na kupunguza umasikini kwa wananchi walio
wengi.

Mkakati huu ambao utapunguza vijana wengi kukimbilia mijini na
kuliokoa Tanzania kuwa taifa la wachuuzi unahitaji uwekezaji wa
kutosha kwenye miundombinu ya vijijini ikiwemo ya umeme. Mheshimiwa
Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutenga bilioni 150
kwa ajili ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kwa kushirikiana na
Halmashauri za Wilaya kwa ajili ya uzalishaji wa umeme toka vyanzo
vidogo vya maeneo mbalimbali pamoja na usambazaji wa umeme katika
maeneo ya vijijini.

Chanzo cha nyongeza ikiwa ni fedha ambazo zinaendelea kutozwa hivi
sasa kutokana na ongezeko katika kodi ya mafuta ya taa ambayo
ikiendelea kwa mwaka mzima serikali kukusanya kiasi kisichopungua
bilioni 70. Mheshimiwa Spika; tunatambua kwamba utekelezaji wa mradi
kabambe wa kusambaza umeme katika mikoa 16 unasuasua kutokana na
serikali kutokupeleka fedha kwa REA kwa mujibu wa bajeti
zinazopitishwa na serikali.

Mpaka mwezi Mei mwaka 2011 serikali ilikuwa imepeleka bilioni 23.3 tu
kwa ajili ya malipo ya wakandarasi wakati ambapo fedha zinazohitajika
ni shilingi bilioni 78.3. Kwa mwaka wa fedha 2008/2009 fedha ambazo
hazikutolewa na hazina ni bilioni 25.3 huku mwaka wa fedha 2010/2011
mpaka mwezi Mei zikiwa zimetolewa bilioni 13.6 tu ambazo ni sawa na
chini ya robo (23%) ya bajeti iliyopangwa.

Aidha kambi ya upinzani inashauri mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu
za serikali (CAG) afanye ukaguzi wa ufanisi wa miradi inayoendelea
kutekelezwa ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa mapema kuwezesha
wananchi wa vijijini kupata umeme.

Mheshimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani hairidhiki na kasi ya
kuboresha utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) na tunataka serikali
ieleze hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mpango maalum wa
kurekebisha hali ya kifedha ya shirika (2006-2010). Kambi rasmi ya
upinzani inaitaka serikali iwaeleze watanzania ni lini mapitio ya
mikataba ambayo inaipa mzigo mkubwa wa kifedha TANESCO na kusababisha
bei ya umeme kupanda itafanyiwa mapitio.

Aidha, serikali imekuwa ikiidhamini TANESCO kupata mikopo ambayo kwa
sehemu kubwa imekuwa ikitumika kwenye kukodi mitambo ya dharura; hivyo
kambi rasmi ya upinzani inashauri kuwe na udhibiti wa kutosha ili
mikopo hiyo isigeuke kuwa mzigo kwa taifa baadaye. Kwa upande
mwingine, TANESCO imekuwa ikizidai wizara, idara na taasisi za
serikali Ankara za umeme zinazofikia bilioni 76; hivyo serikali
inapaswa ionyeshe mfano kwa kufanya malipo kwa wakati.

Mheshimiwa Spika; Pia pamekuwepo malalamiko mbalimbali kuhusu
mazingira ya kupitishwa kwa zabuni za ununuzi wa nguzo, transforma na
nyaya za umeme kwa kiwango kikubwa toka nje ya nchi huku viwanda vya
ndani mathalani TANALEC ABB, East African Cables (hususani kampuni
tanzu ya Tanzania Cables) na vingine vikididimia.

Hali hii imesababisha pia kukwama kwa utekelezwaji wa miradi
mbalimbali ya kusambaza umeme kutokana kwa kile kinachoelezwa kuwa ni
vifaa kutokupatikana kwa wakati toka nje ya nchi. Kambi ya Upinzani
inaitaka Serikali kuandaa mkakati wa kupunguza gharama za manunuzi na
pia kupunguza kiwango cha uagizaji wa nguzo na vifaa vingine kutoka
nje ili kutumia rasilimali za ndani ili kuchangia katika kukuza
uzalishaji na uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani hairidhiki na hatua ambazo
serikali inachukua katika kupunguza gharama wanazotozwa wananchi za
kuunganishiwa huduma ya umeme suala ambalo linapunguza kasi ya
uunganishwaji wa umeme. Tumepokea malalamiko toka kwa wananchi
wanaotakiwa na TANESCO kulipia nguzo na gharama nyingine za
kuunganishwa umeme kwa kiasi kinachozidi milioni moja ambacho ni
vigumu kwa wananchi wa kawaida kumudu.

Hivyo, serikali itoe kauli ya hatua inazopanga kuchukua ikiwemo za
kubadili mfumo wa Ankara ili kuruhusu kuingiza kwa mteja gharama hizo
kidogo kidogo katika kipindi hiki cha mpito. Aidha, TANESCO inahimizwa
kutangaza kwa umma Kanuni za Sheria ya Umeme zilizotolewa kwenye
gazeti la Serikali tarehe 4 Februari 2011 (GN 63) ambazo kifungu cha
nne kinaeleza namna mteja atakavyofidiwa na kampuni ya usambazaji pale
ambapo mteja anajigharamia mwenyewe kuvutiwa umeme ili fursa hiyo
iweze kutumika ipasavyo.

Mheshimiwa Spika; kutokana na kasi ndogo ya usambazaji wa umeme,
pamoja na kuondoa kodi katika vifaa vya umeme wa jua; serikali ieleze
hatua ilizochukua katika kuweka mazingira wezeshi kwa vifaa vya umeme
wa dharura kuweza kupatikana kwa urahisi mathalani vifaa vya
kuhifadhia umeme (invetors). Aidha, serikali iongeze kasi ya
kutekeleza miradi ya kuhamasisha nishati mbadala hususani vijijini kwa
kufanya marekebisho ya msingi katika sheria ya fedha na sheria ya
umeme.

Gesi Asilia Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imejaliwa utajiri wa gesi
asilia katikati ya lindi la umasikini wa wananchi. Gesi asili
iligunduliwa nchini mwaka 1974, ikaanza kutumika kuzalisha umeme
viwandani 2004 mpaka sasa inatumika kuzalisha MW 440 sawa na 60% ya
matumizi yote ya umeme kila siku na inatumiwa na takribani viwanda 25
kwa uzalishaji.

Kwa mujibu wa tafiti tuna zaidi ya 12 tr cf za gesi na uko uwezekano
wa kugundua zaidi kutokana na utafutaji unaoendelea. Taifa letu lina
fursa ya kuwa nchi kiongozi katika gesi Afrika na kushindana kimataifa
ikiwa tutaweka mstari wa mbele upeo, umakini na uadilifu katika sekta
ya nishati kuepusha laana ya rasilimali. Hata hivyo kwa mwelekeo wa
ufisadi na udhaifu wa kiuongozi unaoendelea hivi sasa rasilimali hii
inaweza kuwa chanzo cha migogoro na kuhatarisha pia usalama wa nchi.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba mradi wa
Bomba la Gesi kutoka Mtwara kupitia Dar es salaam mpaka Tanga uwekwe
kipaumbele katika Bajeti ya nyongeza ya Wizara ya Nishati na Madini
kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Hivyo, serikali itenge bilioni 200 kwa
ajili ya kuchangia kwenye mradi wa Bomba la Gesi na kuchangia katika
ujenzi wa Kiwanda cha Gesi kama sehemu ya mkakati wa kushughulikia
upungufu wa nishati kama janga la taifa.

Aidha usiri katika majadiliano ya mradi wa bomba la gesi ni muhimu
ukaondolewa kwa wakati nyaraka rasmi za kiserikali zinaonyesha
majadiliano yanayoendelea kati ya Tanzania na China kuhusu mradi
husika; kambi rasmi ya upinzani inayo mawasiliano baina ya watendaji
wakuu wa kampuni ya Orca Exploration Limited na baadhi ya maofisa wa
ikulu kutaka kupatiwa mradi husika; wakati kampuni yao tanzu ya Pan
African Energy Tanzania (PAT) imekuwa ikilalamikiwa kuhusu mradi
mwingine wa gesi.

Mheshimiwa Spika; kambi ya rasmi ya upinzani inasisitiza mradi kwa
kujenga kiwanda cha kujaza gesi kwenye mitungi (LPG) na mradi wa
usambazaji wa gesi Dar es salaam pamoja na mradi matumizi ya gesi
kwenye magari inayotekelezwa na Shirika la Petroli Nchini (TPDC)
inapaswa kuongezewa rasilimali katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Hatua hii itapunguza pia matumizi ya umeme katika maeneo yenye kuweza
kutumia gesi na kubakiza umeme mwingine utakaoweza kutumika kwenye
maeneo ikiwemo ya viwandani yenye upungufu wa nishati mbadala. Uamuzi
huu utawezesha pia kupunguza gharama za uzalishaji na za maisha
zinazotokana na kupanda kwa bei ya mafuta ambayo pamoja na mizigo ya
kodi na gharama zinazotokana na mfumo mbovu wa uingizaji inasababishwa
pia na kupanda kwa bei katika soko la dunia.

Aidha ili kuongeza mapato kwa serikali na TPDC kambi rasmi ya upinzani
inataka mrabaha wa asilimia 12 kwenye gesi uanze kutozwa kwa mujibu wa
sheria na isitishe mara moja utaratibu wa baadhi kuachiwa kutokulipa
malipo husika kwa mujibu wa wa sheria. Mapitio ya kitabu cha mapato
yameonyesha kwamba wakati kwenye kifungu cha 2001 cha madini kuna
mrabaha hakuna kasma hiyo kwenye kifungu 3001 kinachohusika na gesi na
mafuta.

Mheshimiwa Spika; ili kujiandaa kitaaalumu kama taifa kwa mipango
kabambe ya gesi, kambi rasmi ya upinzani itekeleze mkakati wa
kuwaambatanisha wataalamu wazawa na makampuni makubwa yenye uzoefu wa
sekta husika. Aidha, kambi rasmi ya upinzani inataka Wizara ya Nishati
na Madini iharakishe kukamilisha mtaala wa uhandisi wa gesi na mafuta
ili fani hizo ziweze kutolewa kwenye Chuo Cha Madini Dodoma. Aidha,
kwa kuwa serikali wakati wa kuhitimisha mjadala wa mpango wa mpango wa
taifa wa miaka mitano; serikali ilikubali pendekezo la kuanzisha Chuo
Kikuu cha Mtwara.

Kambi rasmi ya upinzani inaitaka Wizara ya Nishati na Madini kueleza
maandalizi ambayo inakusudia kuyafanya kwa kushirikiana na mamlaka
zingine husika ili kuwezesha uanzishwaji wa chuo kikuu hicho muhimu
ambacho kitatoa mchango mkubwa kwa taifa katika masuala ya gesi na
bidhaa zitokanazo na gesi.

Mheshimiwa Spika; kwa muda mrefu sasa taifa letu limekuwa likitegemea
mradi mkubwa wa Songo Songo kwa shughuli za uendelezaji, uzalishaji,
usafishaji na usafirishaji ambao uko chini ya Kampuni ya Songas. Hata
hivyo, kampuni ya Songos imeiajiri Kampuni ya PanAfrican Energy
Tanzania (PAT), ambayo ni mshirika wa TPDC katika uzalishaji,
usambazaji na ugavi wa gesi asili. PAT imepewa pia Mradi wa Kusambaza
Gesi Asili (Ring Main and CNG Project) jijini Dar es Salaam. Taarifa
mbalimbali zinaonyesha kuwa Kampuni ya PAT ililipwa kiasi kikubwa cha
fedha zaidi gharama ilizoingia wakati wa kujenga mtandao wa usambazaji
wa gesi asili.

Mheshimiwa spika, Aidha upo mwenendo usioridhisha wa kampuni hii ambao
unapelekea upungufu wa gesi unaosababisha mgawo wa umeme, mfumo wa bei
kubwa unaoongeza mzigo wa watumiaji na pia upotevu wa mapato ya
serikali. Hivi karibuni kampuni hii ilipewa na TPDC mabilioni ya fedha
kinyume cha taratibu mpaka sasa serikali inadai; ni muhimu serikali
ikawaeleza watanzania ni viongozi gani walinufaika na malipo hayo na
kiasi gani mpaka sasa hakijarejeswa.

Kutokana na uzito wa tuhuma na usiri katika mikataba; Kambi Rasmi ya
Upinzani inashauri kuundwe kamati teule ya bunge itayofanya mapitio ya
mikataba, sheria, kanuni pamoja na tuhuma za upungufu wa mgawo wa
mapato na ufisadi kutokana na mauzo ya gesi kuanzia mwaka 2004 mpaka
2010.

Mafuta Mheshimiwa Spika; Taarifa za Hali ya Uchumi nchini zinaeleza
kuwa mfumuko wa bei unaombatana na kupanda kwa gharama za maisha
unazidi kuongezeka katika taifa letu kutoka asilimia 4.2% Oktoba mpaka
6.4% Aprili, na kama utaendelea kupanda hivi kwa ari, nguvu na kasi
zaidi kwa miezi michache ijayo utakuwa zaidi ya tarakimu moja.

Kambi rasmi ya upinzani inatambua kwamba ukiondoa kupanda kwa bei ya
chakula kunakutokana na kushuka kwa uzalishaji, chanzo kikuu cha hali
hii ni ongezeko la bei ya nishati hususani mafuta, umeme na gesi hali
ambayo isipodhibitiwa kwa mikakati makini ni tishio kwa utulivu wa
taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Juni 2011 kambi rasmi ya upinzani
iliishukuru serikali kwa kutoa kauli ya kukubali matakwa ya umma na
pendekezo la kambi rasmi ya upinzani la kupunguza kodi na tozo kwenye
bidhaa za mafuta ili kupunguza bei na mzigo mkubwa wa gharama za
wananchi na kuonyesha mashaka kuhusu kiwango ambacho kitaondolewa na
serikali.

Mheshimiwa Spika, Mashaka hayo yalidhihirisha kwenye kupitishwa kwa
muswada wa sheria ya fedha tarehe 22 Juni 2011 ambapo serikali
haikuonyesha kivitendo dhamira ya kupunguza kodi kwenye mafuta kwa
kiwango cha kuwapunguzia ugumu wa maisha badala yake ikajikita kwenye
kupunguza tatizo la uchakachuaji pekee ambalo limedumu kwa sababu ya
serikali kushindwa kusimamia utawala wa sheria. Ushahidi ni kwamba
katika marekebisho ya kodi; serikali haikupunguza hata senti moja
katika mzigo wa kodi kwenye petrol. Aidha, serikali ilipunguza kodi ya
dizeli kwa shilingi 99 tu huku ikiongeza kodi ya mafuta ya taa kwa
shilingi 358.

Mheshimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani ilikuwa na dhamira ya
kuwianisha bei ya mafuta ya taa na dizeli ili kupunguza tatizo la
uchakachuaji; lakini si kwa kuongeza kwa kiwango kikubwa kodi ya
mafuta kama ilivyofanya serikali. Matokeo ya uamuzi huu ni kwamba
wakati bei ya petroli na dizeli zikibaki bila kupungua au zikipanda
katika maeneo mengi ya nchi; bei ya mafuta ya taa imepanda kwa ari,
nguvu na kasi zaidi.

Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuleta marekebisho ya sheria
ya fedha ili kurekebisha hali hiyo na kueleza mkakati wa kweli wa
kupunguza gharama za maisha kwa wananchi. Aidha, serikali ijieleze
bungeni kutokana na udhaifu ulionyeswa na taasisi zake ikiwemo Mamlaka
ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) katika kusimamia bei elekezi na
kupunguza bei za mafuta ambazo serikali iliahidi bungeni kuwa
zingepungua kuanzia Julai 2011.

Aidha kama sehemu ya mchakato wa kupunguza gharama za mafuta
kufuatilia mabadiliko ya kodi, tozo na mfumo wa uingizaji wa mafuta
serikali ifanye mapitio ya mkataba baina ya EWURA na kampuni ya Global
Fluids International (T) Ltd kuhusu ufanisi na gharama za kuweka
vinasaba na kuleta vifaa maalum vya kupima ubora (XRF).

Mheshimiwa Spika, ukiondoa kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la
dunia na ukubwa wa kodi zinazotozwa na serikali bei ya mafuta inakuwa
juu kutokana na mfumo mzima wa uagizaji, usafirishaji, uingizaji na
usambazaji. Mfumo uliopo sasa unanufaisha makampuni makubwa mengi
yakiwa ya kigeni na wafanyabiashara wachache wa ndani pamoja na baadhi
ya viongozi wa serikali wasiokuwa waadilifu kwa kulinyonya taifa na
kuongeza gharama za maisha kwa watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Spika; Hali hii ndiyo iliyokwamisha kwa muda mrefu kuanza
kwa mfumo wa uagizaji na uingizaji wa mafuta ya pamoja (Bulk
Procurement System) ili kupunguza gharama; suala ambalo Julai 2010
serikali ilisema liko katika hatua za mwisho na Julai 2011 mwaka mmoja
baadaye bado serikali bado inatumia lugha ile ile. Aidha Serikali
iwajibike kwa kutoanzisha hifadhi ya mafuta mpaka hivi sasa wakati
mwaka 2010 ilitoa kauli ya kufufua kampuni ya taifa ya mafuta (COPEC);
kwa ujumla kupanda kwa gharama ya mafuta kumechangiwa kwa kiasi
kikubwa na udhaifu wa serikali wa kutochukua hatua zinazostahili kwa
wakati.

Kama imeshindwa kufufua kampuni ya taifa ya mafuta itekeleze pendekezo
lililotolewa na kambi rasmi ya upinzani la kuchukua hisa 100% katika
kampuni ya BP ambayo serikali ina hisa na kuigeuza kuwa chombo cha
kutimiza azma husika. Aidha Wizara ya Nishati na Madini ieleze hatua
mahususi za kulinda maslahi ya nchi katika kampuni ya TIPER ambayo
serikali ina hisa 50% katika hatua za uingizaji na uhifadhi wa mafuta.

Mheshimiwa Spika; Ili kuongeza tija na ufanisi wa TPDC, kambi rasmi ya
upinzani inaitaka Serikali itoe maelezo kuhusu hatua iliyofikiwa
katika kutekeleza ushauri wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma wa
kulifanyia marekebisho shirika hilo ili kuwa na mamlaka itakayohusika
na kutoa vibali kwenye leseni na kusimamia uchimbaji wa mafuta na gesi
na kampuni itakayoshiriki katika biashara ya mafuta na gesi.

Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upizani Bungeni inaendelea
kusikitishwa na uamuzi uliofanywa wa tarehe 22 Juni 2011 wa kuondoa
msamaha wa kodi ya mafuta kwa kampuni za utafutaji ya mafuta na Gesi.
Uzoefu kutokana na misamaha ambayo imekuwa ikitolewa kwa makampuni ya
madini unadhihirisha kwamba makampuni mengi yanatumia mwanya huo
kuleta mafuta yasiyo na kodi na kuyaingiza kwenye soko la ndani la
reja reja. Mathalani takwimimu zimedhihirisha kuwa kupitia misamaha
iliyotolewa kwa makampuni matano tu ya madini ni karibu robo ya mafuta
yote ya Dizeli yaliyoingia nchini na kampuni hizi zililipa dola laki
mbili tu.

Mheshimiwa Spika; Misamaha hii haina maslahi ya taifa na ni mianya
mingine ya uhujumu uchumi; hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
serikali kufikiria upya uamuzi huo na kuleta marekebisho ya sheria ya
fedha ili kuufuta msamaha hiyo kwa kuwa kampuni za utafutaji mafuta na
gesi zinayofursa kwa mujibu wa mikataba (PSA) kurejeshewa gharama zao
mara baada ya mafuta kupatikana. Aidha, uamuzi huu uhusishe pia
kampuni za madini bila kujali mikataba (MDA) kwa kuwa imethibitika
kampuni hizi zote hutengeneza faida nono bila kulipa kodi
inavyostahili.

Madini

Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa sekta ya madini mwaka 2010/2011
kumekuwa na ongezeko la uzalishaji huku mauzo ya nje ya madini yakiwa
yameongezeka; dhahabu pekee ikifikia thamani ya dola 1,516.6. Hata
hivyo mchango kwenye mauzo ya nje umeendelea kuwa ule ule wa asilimia
3.3 wa mwaka 2009/2010 na mchango kwenye pato la taifa ni asilimia 7.1
tu licha ya maelezo matamu ya serikali kuwa mapato yameongezeka
kutokana na kutungwa kwa sheria mpya ya madini.

Mheshimiwa Spika, Nyaraka ambazo kambi rasmi ya upinzani inazo toka
vyanzo vya kiserikali yanaonyesha kwamba sehemu kubwa ya makampuni
yenye mikataba yamekataa kukubaliana na serikali. Hatua za haraka
zinahitajika kulinusuru taifa na hali hii ambapo utajiri wetu
unaendelea kuondoka huku watanzania wakiendelea kuwa masikini; hatua
ambazo zitahusisha mwingiliano baina ya sekta ya madini na sekta
nyingine.

Mheshimiwa Spika; Ukirejea kitabu cha kwanza cha mapato ya serikali
kwa mwaka 2011/2012, nchi yetu itakusanya bilioni 99.5 tu; hii ni aibu
ya taifa ukilinganisha na mauzo ambayo sekta hii inauza nje hasa kwa
kuzingatia sehemu kubwa ya kampuni hizo hazilipi kodi inavyostahili.

Kambi ya Rasmi ya Upinzani inaishauri Wizara ya Nishati na Madini
kuwasiliana na Wizara ya Fedha ili kuboresha mfumo wa utoaji wa
taarifa za malipo ya kodi kwa kampuni za madini ili malipo ya kila
kampuni na mchangunuo wake yafahamike kwa umma badala ya mfumo wa sasa
ambapo hurundikwa pamoja katika takwimu za idara ya walipa kodi
wakubwa. Aidha, Wakala wa Madini (TMAA) ufanye ufuatiliaji maalum wa
madini ya Tanzanite; ambapo bei katika soko iko kati ya dola 250-400
na zaidi kwa kwa karati wakati viwango vinavyotumiwa na mamlaka husika
kukadirani vidogo hali inayosababisha upotevu wa mapato.

Mheshimiwa Spika; Ili kuongeza kiwango cha mapato ikiwemo ya kodi
kutokana na uchimbaji wa madini; kambi rasmi ya upinzani inaitaka
serikali kutekeleza mikakati ya kupenya kuta za umiliki na mitaji
(capital and ownership structures) zilizojengwa kwa muda mrefu na
makampuni ya kimataifa kwa kutumia mianya ya udhaifu wa kisheria na
ushawishi wa kifisadi uliosababisha mikataba mibovu katika sekta ya
madini nchini.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kueleza
bayana hatua ambazo imechukua kufuatia ripoti ya tume/kamati
mbalimbali ambazo ziliundwa na serikali kwa nyakati mbalimbali kwa
kutumia fedha nyingi za walipa kodi lakini mapendekezo yake bado
hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake. Mathalani ripoti za karibuni za
Kamati ya Masha na ile ya Bomani (2008) zilieleza bayana namna ambavyo
makampuni makubwa ya madini yamekuwa yakitumia sehemu kubwa ya
uwekazaji wao kama mkopo (debt financing).

Kambi Rasmi ya Upinzani, inatambua kwamba makampuni hayo yamekuwa
yakitumia mianya hiyo ya kisheria na kimikataba kuwezesha wamiliki na
wanahisa kupata faida mapema kuliko kuweka mtaji kwa kuwa riba ya
mikopo huondolewa katika kukokotoa kodi.

Kambi Rasmi ya Upinzani inataka serikali iwaeleze watanzania ni
trilioni ngapi za mapato tumezikosa kati ya mwaka 1995 mpaka 2010
katika kipindi cha miaka 15 ya kuachia mianya ya upotevu wa mapato kwa
kuruhusu asilimia kubwa ya mikopo kuwa mitaji. Aidha, ni hatua gani
zimechukuliwa kwa waliohusika kuliingiza taifa katika mikataba mibovu
iliyoruhusu makampuni hayo kujitangazia hasara kila mwaka huku
yakipata faida kubwa.

Mheshimiwa Spika; ukipitia kitabu cha mapato serikali imeweka malengo
madogo ya mapato kwa upande wa Wizara ya Nishati na Madini hali ambayo
inadhihirisha kwamba inakusudia kuendelea kutoza mrabaha wa asilimia
3; tofauti na mapendekezo ya Kamati ya Bomani ya asilimia 5 na Sheria
ya Madini ya mwaka 2010 ambayo inaitaka serikali kutoza asilimia 4.
Kwa upande mwingine bado serikali inaachia mianya kwa makampuni ya
madini kutotoa mrabaha baada ya kuondoa gharama za usafiri (net back
value) badala ya kutoa kwenye mahesabu ya ujumla (gross); Hatua hizi
zikichukuliwa zinaweza kuongeza mapato ya serikali kufikia zaidi ya
bilioni 200.

Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti hali hii ya ukwepaji kodi na kuongeza
mapato ya serikali katika mwaka wa fedha 2011/2012 kambi Rasmi ya
Upinzaniinaitaka Wizara ya Nishati na Madini ieleze hatua mahususi
ambazo itazichukua kutekeleza mapendekezo yafuatayo yaliyotolewa
kwenye bajeti mbadala:

Kutunga Sheria ya kuhakikisha kwamba mikopo kwenye makampuni ya
uwekezaji wa madini katika mahesabu ya kodi isizidi 70% ya mtaji;
Kutunga Sheria kuhakikisha kwamba riba ya mikopo kwenye makampuni
yanayohusiana haitaondolewa kwenye mahesabu ya kodi; Kufanya
marekebisho ya sheria kuhakikisha kwamba kodi ya mtaji (capital gains)
inatozwa katika mauziano ya makampuni yote ya madini ambayo mali zake
au uwekezaji wake uko nchini hata kama mauziano hayo yamefanyika nje
ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kuendelea kuporomoka kwa thamani ya
shilingi ya Tanzania; kambi rasmi ya upinzani inaishauri Wizara ya
Nishati na Madini kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Fedha katika
kuweka mikakati na usimamizi wa kuhusisha sekta ya madini katika
kuimarisha fedha yetu. Kwa kuwa mauzo ya madini yetu yanaongezeka huku
shilingi ikishuka;

Kambi Rasmi ya Upinzani, inaitaka Wizara ieleze hatua ilizochukua za
kushirikiana na Wizara ya Fedha katika kuwezesha Benki kuu kutunza
sehemu ya hifadhi yetu ya fedha za kigeni katika mfumo wa madini ya
dhahabu. Wizara ya Nishati na Madini ishirikiane na benki kuu kuweka
mfumo wa kununua dhahabu kwa wachimbaji wadogo na pia kutoza sehemu ya
mrabaha wa dhahabu kwa ajili ya uhifadhi kama ilivyoshauriwa na Kamati
ya Hesabu za Mashirika ya Umma. Taratibu hizi ziende sambamba na
kusimamia mfumo wa kuhakikisha kwamba makampuni hayo yanatunza sehemu
kubwa ya fedha za nje (walau 60%) kwenye benki za ndani ili kusaidia
kudhibiti kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika; Sheria ya Madini ya mwaka 2010 imeipa majukumu
muhimu STAMICO ya kuwa mwakilishi na msimamizi wa rasilimali za madini
nchini kwa niaba ya serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani hairidhishwi na
kasi ya kuliwezesha shirika hili muhimu kutekeleza wajibu wake. Mwaka
mmoja umepita bila ya serikali kukamilisha mchakato wa marekebisho ya
STAMICO kuweza kukidhi haja. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali
ieleze ni kwa nini marekebisho ya sheria ndogo iliyoanzisha STAMICO
(Establishment order) katika mwaka wa fedha 2010/2011 kama
ilivyoahidiwa na kurejesha fedha za nyumba nne za STAMICO ambazo
ziliuzwa na wakala wa majengo Tanzania (TBA)?

Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Msingi katika sekta ya madini ni
kuhakikisha watanzania wanaumiliki katika miradi mikubwa ya madini ama
kupitia hisa za makampuni hayo kuwekwa katika soko la ndani (DSE) au
kwa kampuni ya umma kushikilia sehemu kubwa ya uwekezaji hasa katika
madini nyeti ikiwemo urani. Hivyo, ni lazima mtaji wa STAMICO uongezwe
haraka kwa kurekebisha sheria na kanuni lakini pia kuongeza mtaji wa
shirika. Ukiondoa albaki ya bilioni 5.25 bilioni Serikali ieleze hatua
ambazo inakusudia kuongeza mtaji wa STAMICO katika mwaka wa fedha
2011/2012.

Mheshimiwa Spika; tunatambua kwamba Wakala Jiolojia (GST) anaendelea
na utekelaji wa mradi wa kutambua maeneo ya madini. Kambi ya upinzani
inataka mradi huu uende sambamba na kufanya tathmini ya kina (mineral
appraisal) ya madini yetu na kupendekeza mabadiliko ya kisheria na
kimikataba ambayo yatawezesha utajiri wa madini yetu kutumika kama
mtaji na dhamana katika hatua ya kuhakikisha taifa letu linanufaika na
rasilimali zake.

Pia; ili kuongeza uwezo wa GST kutimiza wajibu wake malipo yote
yanayopaswa kutolewa kwa mujibu wa sheria ndogo iliyounda wakala
husika (Establishment Order) yafanyike kwa mujibu wa taratibu kuanzia
mwaka wa fedha 2011/2012. Aidha; ramani na ripoti zinazotokana na
utafiti na uchunguzi huo zitolewe kwa uangalifu ili kuhakikisha
maslahi ya taifa yanalindwa katika hatua zote.

Mheshimiwa Spika; tunasikitishwa na maamuzi ya serikali ya kuendelea
na hatua za mbele katika utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani
bila kukamilisha maandalizi ya kisera, kisheria, kikanuni na kitaasisi
yanayohitajika suala ambalo litaachia mianya ya upotevu wa mapato kwa
taifa kama ilivyokuwa kwenye madini mengine na pia itahatarisha
usalama.

Kambi ya Rasmi ya Upinzani inataka maelezo ya kina kuhusu mauzo na
mabadilishano ya umiliki yaliyofanyika baina ya kampuni ya Australia
(Mantra Resources) na Kampuni ya Urusi ya ARMZ Uranium Holding kampuni
tanzu ya Rosato. Mauzo hayo ambayo yanaelezwa kimataifa kuwa
yamefanyika kwa bei ya dola 1.16 bilioni ambayo ni zaidi ya shilingi
trilioni 2. Mauzo hayo yamehusisha kuhamishiana umiliki wa maeneo ya
Tanzania Mkuju River (Namtumbo) na Bahi Kaskazini (Dodoma).

Mheshimiwa Spika, Iwapo tungepata asilimia 30 tu ya mauzo hayo kama
kodi taifa letu lingepata 600 bilioni ambayo ni fedha nyingi kuliko
bajeti nzima ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka. Izingatiwe
kwamba eneo husika lina madini ya urani takribani paundi 108 milioni
sawa na asilimia 77 ya uchimbaji wote wa urani kwa mwaka jana. Hii ni
aibu kwa taifa linalokwenda nje kuomba huku ikiachia bwerere fursa za
rasilimali za ndani na kufikia hatua hata ya mbuga za wanyama kuvamiwa
kwa uchimbaji usio kuwa na tija ya moja kwa moja kwa watanzania walio
wengi.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kusimamisha kwa muda
taratibu zinazoendelea za uchimbaji wa urani mpaka maandalizi ya
msingi yafanyike yatakayohakikisha umiliki, manufaa na usalama.

Mheshimiwa Spika; pamoja na ahadi ya serikali kumaliza migogoro katika
sekta ya madini baina ya wachimbaji wakubwa na wachimbaji wadogo
pamoja na kuepusha migogoro ya leseni mathalani mgogoro wa wachimbaji
wadogo eneo la Winza wilaya ya Mpwapwa ambao serikali iliahidi bungeni
tarehe 9 Julai 2010 kuumaliza.

Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kauli ya serikali kuhusu mgogoro huo
kwa kuwa tayari wachimbaji wadogo wameanza kuhamishwa kwa nguvu toka
maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, pia migogoro ya wafanyakazi katika makampuni ya
madini. Wizara ya Nishati na Madini ilieleze taifa hatua ilizochukua
kushirikiana na Wizara nyingine husika kutatua malalamiko ya
wafanyakazi wa Tanzanite kuhusu ongezeko la wafanyakazi wageni;
Wafanyakazi walioachishwa katika kampuni ya Bulyankulu; kampuni ya
Caspiani katika mgodi wa Mwadui Shinyanga ambayo yapo Wizarani kwa
muda mrefu bila hatua za msingi kuchukuliwa.

Mheshimiwa Spika, Mnamo tarehe 25 Mei 1946 kampuni iitwayo Alamasi
Limited ilipewa leseni ya kuchimba madini ya almasi kaskazini ya
kijiji cha Luhumbo katika eneo la Mwadui, Wilaya ya Shinyanga. Leseni
hiyo ijulikanayo kama Hati ya Uchimbaji (Mining Lease) Na. 224
ilitolewa chini ya Sheria ya Madini ya mwaka 1929 iliyokuwa inatumika
wakati huo na ilihusu eneo la ukubwa wa ekari 3007. Ili kuchimba
almasi katika eneo hilo, Alamasi Ltd. ilipewa Hati Milki ya ardhi Na.
5954. Muda wa leseni hiyo ulikuwa miaka ishirini na moja kuanzia
tarehe 14 Juni 1944 na ulitakiwa kwisha tarehe 31 Mei 1965.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa leseni hiyo, Alamasi Limited ilitakiwa
kulipa kodi ya ardhi ya senti hamsini kwa ekari moja kwa nusu ya mwaka
1944 iliyokuwa imebakia, na baadae kodi ilitakiwa kupanda hadi
shilingi moja kwa ekari kwa mwaka 1945; shilingi moja na thumni kwa
mwaka 1946; shilingi mbili kwa mwaka 1947 na baada ya hapo kodi
ilitakiwa kuwa shilingi mbili na thumni kwa ekari kwa kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, Ilipofika Januari Mosi 1963, Alamasi Ltd. ilihamisha
umiliki wa leseni hiyo kwa muda uliobakia kwa kampuni mpya iitwayo New
Alamasi (1963) Limited. Uhamisho wa milki hiyo ulithibitishwa na
Msajili wa Hati Msaidizi mnamo tarehe 23 Mei 1963 baada ya taratibu
zote za kisheria za uhamisho kukamilika. Kwa mujibu wa taarifa ya
Msajili wa Hati Mkuu Msaidizi Mary J. Mziray iliyotolewa tarehe 30
Januari 2006, milki ya leseni ya New Alamasi (1963) Ltd. ilikwisha
muda wake tarehe 31 Mei 1965, na eneo la leseni hiyo lilirudishwa
katika milki ya Rais.

Kwa sababu hiyo, kwa mujibu wa barua ya Kamishna wa Madini ya tarehe
27 Machi 2006, Leseni Na. 224 Hati Milki Na. 5954 ilifutwa katika
rejesta ya leseni za madini.

Mheshimiwa Spika, Licha ya muda wa leseni Na. 224 kwisha na leseni
yenyewe kufutwa katika rejesta ya leseni za madini, New Alamasi (1963)
Ltd. iliendelea kuchimba madini ya almasi katika eneo hilo na kuyauza
nchi za nje bila ya kuwa na leseni yoyote ile kwa miaka thelathini na
tano! Aidha, kwa kipindi chote hicho, hakuna takwimu zozote
zinazoonyesha kiasi cha almasi iliyochimbwa kinyume cha sheria na wala
fedha zilizopatikana kutokana na mauzo ya almasi hiyo na zilikoenda
fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, tunaitaka Serikali itoe kauli rasmi juu ya shughuli
za New Alamasi Ltd., uhalali wa shughuli zake za uchimbaji almasi
katika eneo la Luhumbo, kiasi cha almasi iliyochimbwa kwa kipindi
chote tokea tarehe 1 Juni 1965 hadi tarehe 8 Mei 2000 na zilizokoenda
fedha zilizotokana na mauzo ya almasi hiyo! Aidha, Serikali ieleze ni
kwa nini kampuni iliruhusiwa au iliachwa kuendesha shughuli za
uchimbaji haramu wa almasi kwa miaka thelathini na tano na hatua
ambazo zimechukuliwa au zinatarajiwa kuchukuliwa dhidi ya wale wote
waliohusika na ukiukaji huu mkubwa wa sheria za Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Mnamo tarehe 9 Mei 2000, Waziri wa Nishati na Madini
wakati huo Mh. Dr. Abdallah Omari Kigoda aliipatia New Alamasi (1963)
Ltd. leseni Na. ML. 71/2000 kwa ajili ya kuchimba almasi katika eneo
hilo hilo kwa kipindi cha miaka ishirini na tano. Kwa mujibu wa
Kamishna wa Madini kwa barua yake ya tarehe 21 Machi 2006, tarehe 25
Mei 2005, “eneo lililokuwa na leseni hiyo liliunganishwa pamoja na
maeneo mengine na kuwa leseni ya uchimbaji Na. SML 216/2005 ya
Williamson Diamond Ltd. kwa maombi ya wamiliki wa leseni hiyo ya
awali.”

Hii ina maana kwamba wamiliki wa New Alamasi (1963) Ltd. waliomba
leseni yao iunganishwe na maeneo mengine na leseni hiyo mpya
kukabidhiwa kampuni ya Williamson Diamond Ltd. ambayo imekuwa
ikichimba almasi katika eneo la Mwadui kwa zaidi ya miaka sitini.

Mheshimiwa Spika, Kuna shaka kubwa na ya kimsingi juu ya uhalali wa
milki hii mpya ya leseni ya uchimbaji almasi katika eneo la Luhumbo.
Kwanza, kwa mujibu wa kifungu cha Sheria ya Madini ya mwaka 1998
iliyokuwa inatumika wakati huo, leseni pekee inayoweza kutolewa
kisheria kwa ajili ya uchimbaji almasi ni Leseni ya Uchimbaji wa Mawe
ya Vito (Gemstone Mining Licence). Leseni ya Uchimbaji (Mining
Licence) hutolewa tu kwa madini yasiyokuwa mawe ya vito au dhahabu.
Hii ndio kusema kwamba ML. 71/2000 isingeweza kuwa leseni halali kwa
uchimbaji wa almasi katika eneo la Luhumbo au eneo lingine lolote
nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa barua ya Kamishna wa Madini ya tarehe
27 Machi, 2006, ML. 71/2000 iligeuzwa na kuwa Leseni Maalum ya
Uchimbaji (Special Mining Licence) Na. 216/2005 mnamo tarehe 25 Mei
2005. Hii ndio inayosemekana kuwa leseni ya Williamson Diamond Ltd. na
ina ukubwa wa kilometa za mraba 29.73. Hata hivyo, kwa mujibu wa
Sheria ya Madini ya 1998, madini ya almasi hayawezi kuchimbwa kihalali
kwa kutumia Leseni Maalum ya Uchimbaji kwani leseni ya aina hii
hutumika tu kwa uchimbaji wa madini ya vyuma (metals) kama vile
dhahabu na sio kwa mawe ya vito.

Mheshimiwa Spika, madai yaliyotolewa kwa maandishi na Kamishna wa
Madini kwamba ML. 71/2000 iliunganishwa na leseni nyingine na kugeuzwa
kuwa SML. 216/2005 yanaelekea kutokuwa na ukweli wowote. Hii ni kwa
sababu, kwa mujibu wa barua ya Kamishna wa Madini ya tarehe 19Aprili
2008, leseni pekee ambayo Williamson Diamond Ltd. wanayo katika eneo
la Mwadui ni Leseni ya Uchimbaji namba ML 02/92 iliyotolewa tarehe 20
Mei 1992 na aliyekuwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Luteni Kanali
Jakaya Mrisho Kikwete.

Eneo la leseni hiyo ni kilometa za mraba 12.33. Kwa mujibu wa barua
nyingine ya Kamishna wa Madini ya tarehe 21 Aprili 2008, ML 02/92 bado
‘iko hai’ na “haijaunganishwa na eneo au maeneo ya mining licence
nyingine”!

Mheshimiwa Spika, Miezi mitatu baadae, Kamishna wa Madini alipigilia
msumari wa mwisho katika madai haya alipoandika ifuatavyo mnamo tarehe
24 Julai 2008: “Hapakuwa na leseni ya uchimbaji madini ya Williamson
Diamond Limited iliyotumika kuunganishwa na leseni namba ML 71/2000 na
kuwa moja Special Mining Licence SML 216/2005”! Ni wazi, kwa nyaraka
hizi za Serikali, kwamba kuna jambo ambalo limefichwa kuhusiana na
shughuli za uchimbaji almasi za New Alamasi (1963) Ltd. na uhalali wa
shughuli hizo.

Kambi ya Upinzani ,Tunaitaka Serikali itoe kauli rasmi ya kufafanua
mustakabali wa sasa wa eneo la iliyokuwa Hati ya Madini Na. 224.
Tunaitaka Serikali ifafanue utaratibu wa kisheria ambao umeiruhusu
Williamson Diamond Ltd. kuendelea kuchimba almasi katika eneo la
Luhumbo wakati haina leseni halali katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika; Ni nani hasa walikuwa wamiliki na wakurugenzi wa New
Alamasi Ltd? Kwa mujibu wa waraka wa Msajili Msaidizi wa Makampuni
katika Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) juu ya kampuni
hiyo, wamiliki wa New Alamasi Ltd. walikuwa ni mabwana Sylvanus Mipawa
aliyekuwa na hisa tatu na Phares Kitanzi Songo aliyekuwa na hisa na
Williamson Diamonds Ltd. iliyokuwa na hisa 96!

Aidha, kampuni hiyo ilikuwa na mtaji wa shilingi za Tanzania 2000
ikiwa na maana kwamba kila hisa ilikuwa na thamani ya shilingi
ishirini tu! Waraka huu wa BRELA uliandikwa tarehe 22 Septemba, 2006.
Kufuatana na waraka huu, kuanzia mwaka 2002 New Alamasi (1963) Ltd.
ilipeleka fomu za annual returns ambazo hazikukamilika. Aidha, “…
wenye hisa wawili Sylvanus Mipawa na Phares Kitanzi Songo hawaonekani
katika returns na maelezo na utaratibu wa kutoka katika kampuni
haukuzingatiwa.”

Mheshimiwa Spika, Vile vile, kwa mujibu wa waraka wa Msajili Msaidizi
Mwandamizi wa Makampuni wa BRELA wa tarehe 13 Julai 2007, kati ya
mwaka 1965 na 1970, wakurugenzi wa kampuni hiyo walikuwa mabwana
George Faulkner Hunt, Gabriel Jacobus Du Toit na Ian David
Livingstone. Kati ya mwaka 1970 na 1972, wakurugenzi walikuwa George
Faulkner Hunt, Gabriel Jacobus Do Toit na Alexander John Prescott.

Aidha, kati ya mwaka 1973 na mwaka 1983 watu waliopata kuwa
wakurugenzi wa kampuni hiyo ni pamoja na Samuel Lweyemamu Lwakatare,
Robert Macbain Bisset, Ignace Herack Marandu, Jeremias Norbert
Rweyemamu, William Henry Manning, John Robert Dawson Kiwia na Phares
Kintazi Songo. Kwa mujibu wa waraka wa BRELA wa Septemba 2006,
wakurugenzi wa kampuni hii wanaonekana tofauti “… lakini utaratibu
wa mabadiliko haukufuatwa.” Tunaitaka Serikali itoe maelezo sahihi ya
kuhusu wamiliki na wakurugenzi wa kampuni hii na kwa nini taratibu za
kisheria hazijafuatwa kwa miaka mingi. Aidha, tunaitaka Serikali itoe
maelezo iliwezekanaje kwa kampuni yenye mtaji wa shilingi 2000 imeweza
kuchimba almasi kwa zaidi ya miaka arobaini!

Mheshimiwa Spika, Uhusiano kati ya New Alamasi (1963) Ltd. na
Williamson Diamonds Ltd. umegubikwa na utata mkubwa. Hii ni kwa sababu
mnamo tarehe 21 Machi, 2006, wakati akijibu swali la mwandishi wa
habari wa gazeti la Uhuru aliyetaka kujua uhusiano wa makampuni haya
mawili, Kamishna wa Madini alidai kwamba yeye hatunzi kumbu kumbu za
makampuni hivyo “… siwezi kujua uhusiano wa New Alamasi (1963) Ltd.
na Williamson Diamonds Ltd. Na kama tulivyoona, taarifa zilizotolewa
na BRELA Septemba 2006 zinaonyesha kwamba Williamson Diamonds Ltd. ina
96% ya hisa zote za New Alamasi (1963) Ltd.

Hata hivyo, katika tarehe isiyojulikana ya mwaka 1992, New Alamasi
(1963) Ltd. iliingia mkataba na Williamson Diamonds Ltd. ambao kwayo
New Alamasi (1963) Ltd. ilifutwa kwa hiari na kuhamisha hisa na mali
zake zote “zilizoko kwenye Hati ya Madini Na. 224 Hati Milki Na. 5954”
kwa Williamson Diamonds Ltd. Mkataba huu unaelekea ulisainiwa na
Sylvanus Mipawa kwa upande wa New Alamasi na watu watatu wasiojulikana
kwa niaba ya Williamson Diamonds Ltd.

Mheshimiwa Spika; Mkataba huu kati ya New Alamasi (1963) Ltd. na
Williamson Diamonds Ltd. umezua maswali mengi ambayo yanahitaji majibu
kutoka kwa Serikali. Kwanza, mkataba huu unatamka kwamba
kinachohamishwa ni Hati ya Madini Na. 224 na mali zilizoko kwenye eneo
hilo ambavyo kama tulivyoonyesha ilikwisha muda wake tarehe 31 Mei
1965.

Pili, mkataba huu unataja Hati Milki ya Ardhi Na. 5954 ambayo nayo
ilikwisha kurudi kwenye milki ya Rais tangu mwaka 1965 leseni ya
uchimbaji ilipokwisha muda wake! Tatu, mkataba huu unaonyesha
ulifanyika chini ya Mining Ordinance ya mwaka 1929 ambayo ilikwisha
kufutwa tangu mwaka 1979 wakati Sheria ya Madini ya mwaka huo
ilipotungwa! Nne, makubaliano haya yanataja makubaliano mengine ya
kuhamisha haki za New Alamasi (1963) Ltd. yanayodaiwa kufanyika tarehe
31 Januari 1967, 17 Januari 1972 na 14 Februari 1978.

Mheshimiwa Spika, Hata hivyo, hakuna ushahidi wowote wa makubaliano ya
aina hiyo kati ya makampuni haya mawili kwa vipindi vilivyotajwa.
Aidha, makubaliano yanadai kwamba New Alamasi (1963) Ltd. walipewa
leseni ya eneo hilo tarehe 25 Mei 1965 kwa kipindi cha miaka kumi na
sita kuanzia tarehe 13 Juni 1965 “ambayo ilisajiliwa na Idara ya
Madini.” Hata hivyo, kama tulivyoona, Idara ya Madini yenyewe
imekanusha madai hayo kwa kuonyesha kwamba Hati ya Madini Na. 224
ilikwisha muda wake tangu tarehe 31 Mei 1965!

Mheshimiwa Spika; Taarifa tulizonazo zinaonyesha kwamba mkataba kati
ya New Alamasi (1963) Ltd. sio halali bali uligushiwa kwa lengo la
kuwezesha uchimbaji wa almasi kuendelea katika eneo hilo kinyume cha
sheria na ili kuendeleza wizi wa rasilimali ya nchi yetu ambao
umeendelea kwa miaka zaidi ya arobaini! Tunaitaka Serikali itoe kauli
rasmi na sahihi juu ya uhusiano huu kati ya makampuni haya mawili.

Mheshimiwa Spika, Mamia ya wananchi waishio maeneo jirani na eneo la
New Almas wamekuwa wakinyanyaswa kwa miaka mingi na vyombo vya dola
kama vile polisi, mahakama na vyombo vya utawala kwa madai kwamba ni
wavamizi wa eneo la leseni ya New Alamasi. Watu kadhaa wameuawa na
askari polisi na mgambo baada ya kukutwa ndani ya eneo hilo.

Wengi wengine wamepigwa na kuteswa katika vituo vya polisi na wengine
wengi wamefungwa kwa tuhuma za uongo za kuvamia eneo la Mgodi wa New
Alamasi (1963) Ltd. na kwa kutumia hati za kugushi za kuonyesha
umiliki wa eneo hilo. Wote hawa walioteswa namna hiyo na/au ndugu zao
wanastahili sio tu kuombwa msamaha kwa mateso ya miaka mingi na ya
bure, bali pia wanastahili kulipwa fidia kwa madhara yote waliyoyapata
katika muda huo.

Kambi ya Upinzania , Tunaitaka Serikali itoe kauli kama iko tayari
kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanapata haki zao kutokana na uovu
waliotendewa na vyombo vya serikali. Aidha, Serikali itoe taarifa
rasmi juu ya hatua inazotarajia kuzichukua dhidi ya Williamson
Diamonds Ltd. kwa kushiriki katika kugushi nyaraka za kuiwezesha
kuchimba almasi kinyume cha sheria.

HITIMISHO Mheshimimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani inapenda
kuhitimisha kwa kusisiza kwamba kwa sehemu kubwa matatizo katika sekta
za nishati na madini yamechangiwa na sababu za kibinadamu za
kutowajibika ipasavyo kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji kwa
viongozi wa kiserikali kuanzia kwa viongozi wakuu wa nchi, Waziri
mwenye dhamana na watendaji wengine na hivyo kusababisha ugumu wa
maisha kwa wananchi na kuathiri uchumi wa nchi; wahusika wanapaswa
kuwajibika.

Mheshimiwa Spika; uwajibikaji huo unapaswa kufuatiwa na hatua za
haraka za kusimamia sera sahihi, uongozi makini na taasisi thabiti
zenye kuelewa kwamba sekta ya nishati ni moyo wa taifa na sekta ya
madini ni mtaji wetu kwa sasa na kuchukua hatua kali dhidi ya ufisadi
uliofanyika katika sekta husika, kufanya mapitio ya mikataba,
kuharakisha utekelezaji wa mipango kwa ushirikiano kati ya serikali na
sekta binafsi na kwa ujumla kuwajibika.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba bunge lako lijadili
makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa kuzingatia
maoni tuliyoyatoa ya kuongeza bajeti ya wizara husika; kupokea
mapendekezo yatayopelekea kufanyika kwa mabadiliko katika sheria ya
fedha na kupitisha maazimio mahususi ikiwemo ya kukabiliana na
upungufu wa nishatia mbao sasa ni janga la taifa pamoja na kuhakikisha
taifa letu linanufaika na madini; aidha iwapo Serikali haitakubali
hoja hizi za msingi za kuinusuru nchi yetu kuzifanyia kazi, basi
tutaunganisha nguvu ya umma kupitia maandamano na kitaeleweka. Kwa
niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha,

John Mnyika (Mb)

Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani

Wizara ya Nishati na Madini

15/07/2011