*TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUFAFANUA KUHUSU MIRADI YA UTAFUTAJI NA
UVUNAJI WA GESI ASILIA NCHINI*
*1.0 UTANGULIZI*
Wizara ya Nishati na Madini inapenda kutoa ufafanuzi wa miradi ya Gesi
Asilia ambayo itatekelezwa kwa kushirikiana na wawekezaji katika Sekta
ndogo ya Gesi Asilia na kueleza manufaa makubwa yatakayopatikana kwa
wananchi wote wa Tanzania wakiwemo wale wa Mikoa ya Mtwara na Lindi.
Siku ya Alhamisi, tarehe 27 Disemba 2012, baadhi ya Vyama vya Siasa vya
Upinzani viliratibu na kuhamasisha baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara,
wengi wao wakitokea Mtwara Mjini kufanya maandamano ya kudai raslimali ya
Gesi Asilia iwanufaishe wakazi wa Mtwara na kupinga mradi mkubwa wa ujenzi
wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Wizara ya Nishati
na Madini inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa Wa-Tanzania wote kwa kupitia
vyombo vya habari.
Tokea Uhuru, uchumi wa Tanzania umetegemea kilimo cha mazao ya biashara
kama vile katani (Tanga na Morogoro), pamba (Mwanza, Mara na Shinyanga),
kahawa (Kilimanjaro, Kagera, Ruvuma na Mara), chai (Iringa) na tumbaku
(Tabora). Fedha za mazao haya zimewanufaisha wakazi wa mikoa yote ya nchi
yetu bila ubaguzi wo wote wala wakulima wa kutoka mikoa hiyo hawajawahi
kufanya maandamano wakidai upendeleo (dhidi ya Wa-Tanzania wengine) wa aina
yo yote ile.
1
Mapato yatokanayo na uchimbaji wa dhahabu (Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga
na Tabora), almasi (Shinyanga) na tanzanite (Manyara) yamewanufaisha
Wa-Tanzania wote bila ubaguzi wo wote ule! Minofu ya samaki wa Ziwa
Victoria (Mara, Mwanza na Kagera) imeliingizia Taifa letu fedha nyingi
ambazo zimetumiwa na wakazi wa nchi nzima bila ubaguzi wo wote.
Aidha kuna mikoa ambayo inazalisha mazao ya chakula kwa wingi kwa manufaa
ya Wa-Tanzania wote. Mahindi kutoka Rukwa, Mbeya, Ruvuma na Iringa
yanasafirishwa kwenda mikoa yote ya nchi yetu bila kujali eneo yanakolimwa
na wakazi wa mikoa hiyo hawajawahi kudai mahindi hayo ni kwa ajili ya watu
wa mikoa hiyo pekee. Sukari ya Kilombero, Mtibwa na Kagera inatumiwa na
wakazi wa mikoa yetu yote bila ya kuwepo madai ya mikoa inayozalisha sukari
hii kupewa upendeleo wa aina yo yote ile. Maji ya Mto Ruvu yanatumiwa na
wakazi wa Dar Es Salaam bila manung’uniko yo yote kutoka kwa wakazi wa eneo
la chanzo cha Mto Ruvu.
Umeme wa kutoka Mtera, Kidatu na Kihansi (Dodoma na Morogoro), Hale
(Tanga), na Nyumba ya Mungu (Kilimanjaro) unatumiwa na wakazi wote wa
Tanzania bila ubaguzi au malalamiko ya wenyeji wa sehemu ambazo umeme huo
unafuliwa na kusafirishwa kwenye Gridi ya Taifa. Kwa hiyo, kutokana na
mifano hii michache, ni wajibu wa wazalendo na wapenda maendeleo wa kweli
na hasa Wa-Tanzania wanaopinga ubaguzi wa aina yo yote ile kujiuliza kwa
kina sababu zilizopelekea Vyama Siasa vya Upinzani kupanga, kuhamasisha,
kushabikia na kuongoza maandamano ya tarehe 27 Disemba 2012 pale Mtwara
Mjini.
*2.0 RASLIMALI YA GESI ASILIA TANZANIA*
Gesi Asilia ilianza kugundulika hapa nchini tangu mwaka 1974 kwenye Kisiwa
cha Songo Songo, Mkoani Lindi. Baada ya hapo Gesi Asilia imegundulika
maeneo ya Mtwara Vijijini, yaani Mnazi Bay (1982) na Ntorya (2012),
Mkuranga (Pwani, 2007), Kiliwani (Lindi, 2008). Kiasi cha Gesi Asilia
iliyogunduliwa katika maeneo haya inakadiriwa kuwa *Futi za*
2
*Ujazo Trilioni 4.5 – 8. *Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita,* *kumekuwa
na kasi kubwa ya utafutaji Mafuta na Gesi Asilia uliojikita zaidi kwenye
maji ya kina kirefu cha bahari. Kiasi cha Gesi Asilia iliyogundulika katika
kina kirefu cha maji inafikia takribani *Futi za* *Ujazo Trilioni 27. *Kiasi
cha wingi wa Gesi Asilia yote iliyogunduliwa* *nchi kavu na baharini
inafikia takribani *Futi za Ujazo Trilioni 35.*
Kufuatana na Sheria za nchi yetu zinazotumiwa kugawa mipaka ya mikoa
iliyopo kando kando mwa bahari (isivuke 12 nautical miles au 22.22 km
kuingia baharini), Gesi Asilia iliyogunduliwa hadi sasa katika
*Mkoa wa Mtwara pekee ni asilimia 14 tu *ya gesi yote iliyogundulika* *nchini.
Kwa kutumia kigezo hicho cha Sheria za mipaka ya ki-utawala ya mikoa
yetu, *Lindi
inayo 7%* ya gesi yote, *Pwani 1%* na huku Kina Kirefu cha Bahari *(Deep
Sea) ndicho chenye gesi nyingi (78%)* kuliko mikoa yote ikiwekwa pamoja!
Kwa hiyo, hakukuwa na haja ya kufanya maandamano kwa sababu Gesi Asilia
nyingi inapatikana kwenye bahari ya kina kirefu ambayo iko ndani ya mipaka
ya nchi yetu bila kujali mipaka ya mikoa yetu. Isitoshe Gesi Asilia
imegundiliwa kwenye miamba tabaka (sedimentary rocks) yenye umri wa *Miaka
kati ya Milioni 199.6* *hadi 23.03. *Mipaka ya Bara la Afrika, ya nchi yetu
na ile ya mikoa yetu* *haikuwepo wakati huo!
Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia pia unaendelea tukiwa wa mategemeo
makubwa ya upatikanaji wa raslimali hizi katika Mikoa ya Arusha,
Kilimanjaro, Tanga, Manyara, Kigoma, Mbeya, Njombe, Rukwa, Katavi, Morogoro
na Tabora pamoja na kwenye kina kirefu cha maji baharini kuanzia mpaka wetu
na Msumbiji hadi mpaka wetu na Kenya. Hatutarajii mikoa hii nayo ifanye
maandamano ya kutaka kuhodhi raslimali za Gesi Asilia na Mafuta
zitakapogunduliwa mikoani mwao.
*3.0 **MATUMIZI YA GESI ASILIA YA MNAZI BAY (MTWARA) NA SONGO SONGO
(LINDI) *
Mpaka hivi sasa Gesi Asilia inayozalishwa na kutumika nchini ni kutoka
Mnazi Bay (Mtwara Vijijini) na Songo Songo (Kilwa, Lindi). Gesi ya Mnazi
3
Bay kwa sasa huzalisha umeme kwa ajili ya Mikoa ya Mtwara na Lindi tu.
Mitambo ya kufua umeme kutokana na Gesi Asilia iliyopo Mtwara Mjini inao
uwezo wa *kuzalisha MW 18* lakini matumizi ya umeme ya Mikoa ya Mtwara na
Lindi *haijavuka MW 12.* Umeme huo wa Mtwara unafuliwa na TANESCO huku
Kampuni za Wentworth na Maurel & Prom zikizalisha Gesi Asilia (inayotumiwa
na TANESCO) kiasi cha *Futi za* *Ujazo Milioni 2 kwa siku*. Ikumbukwe
kwamba ufuaji wa umeme wa* *hapo Mtwara Mjini ulikuwa mikononi mwa Kampuni
ya Artumas iliyofilisika. *Tangu Desemba 2006 hadi leo hii* kiasi cha gesi
kilichotumika kufua umeme kwa ajili ya mikoa hiyo miwili *ni chini ya*
*asilimia
1 ya gesi yote iliyogundulika Mnazi Bay (Mtwara Vijijini)*.* *Vilevile
ikumbukwe kwamba kuna visima vinne vya Gesi Asilia pale Mnazi Bay (Mtwara
Vijijini) na kinachotumika kwa sasa na tena kwa kiwango cha chini kabisa ni
kimoja tu!
Aidha ni vizuri ndugu zangu Wa-Tanzania wakaelewa kuwa Gesi Asilia hii
inatafutwa na kuchimbwa na wawekezaji wenye mitaji mikubwa, wataalamu na
teknolojia ya utafutaji na uchimbaji wa Gesi Asilia ambao wanapaswa
kurejesha mitaji yao. Uchorangaji wa kisima kimoja cha utafutaji wa Gesi
Asilia nchi kavu unahitaji *Dola za Marekani Milioni* *40, *na kwenye kina
kirefu cha maji baharini zinahitajika zaidi ya* Dola za Marekani Milioni 100
*. Ikumbukwe kwamba, Serikali kwa* *kushirikiana na Shirika la Mafuta la
Tanzania (TPDC), inatumia fedha za walipa kodi wa nchi nzima kwa shughuli
za kuvutia, kuratibu na kusimamia utafutaji na uendelezaji wa Gesi Asilia
nchini kote ikiwemo Mikoa ya Mtwara na Lindi. Walipa kodi Wa-Tanzania bado
hawajalalamika wala hawajafanya maandamano ya kudai fedha zao za kodi
zisitumike huko Mtwara!
Ni muhimu pia tukaelewa kwamba Gesi Asilia iliyopo Mnazi Bay (Mtwara
Vijijini) inazalisha umeme peke yake kwa ajili ya Mikoa ya Mtwara na Lindi.
Gesi Asilia ya Songo Songo (Kilwa, Lindi) *ndiyo* inayotumika kuzalisha
umeme kwa ajili ya Gridi ya Taifa, na pia kwa ajili ya wananchi wa Kisiwa
cha Songo Songo (Lindi), maeneo ya Somanga
4
Fungu (Lindi) na viwandani (Dar Es Salaam). Tangu Oktoba 2004 ambapo
mitambo ya kufua umeme ilipoanza kazi hadi leo hii, kiasi cha Gesi Asilia
ya Songo Songo kilichotumika ni *asilimia 7 tu* ya Gesi Asilia yote
iliyogunduliwa huko. Kwa hiyo, takwimu zinaonyesha kwamba hata uchumi wa
Jiji la Dar Es Salaam unatumia kiasi kidogo sana cha Gesi Asilia
*(7%)*iliyopo Songo Songo (Kilwa, Lindi). Ikumbukwe kwamba waajiriwa
kwenye
viwanda vya Dar Es Salaam wamo wanyeji wa kutoka Mtwara Mjini ambako
maandamano yalifanyika na vilevile wamo wafanyakazi ambao ni wanachama wa
Vyama vya Siasa vya Upinzani vilivyopanga, ratibu na kushabikia maandamano
ya Mtwara Mjini ya tarehe 27 Disemba 2012.
*4.0 **MIPANGO YA MATUMIZI YA GESI ASILIA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA 5
HADI 10 *
* *
*(a) **Ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia hadi Dar Es Salaam: *
* *
Kuuza Gesi Asilia Jijini Dar es Salaam, kitovu cha uchumi wa Tanzania (80%
ya mapato ya nchi yetu yanazalishwa Dar Es Salaam) ni uamuzi mzuri wa
ki-uchumi. Tayari kuna viwanda **
34 vinatumia Gesi Asilia ambavyo vinahitaji kupanua shughuli zao endapo
gesi zaidi itapatikana. Soko kubwa la Gesi Asilia lipo tayari Dar es Salaam
(na siyo Mtwara), ambapo ipo mitambo ya kufua umeme kwa kutumia mafuta.
Serikali inatumia fedha nyingi za kigeni kununulia mafuta ya kufua umeme
tunaoutumia kila siku. Takribani Dola za Marekani Bilioni Moja *(sawa na
Shilingi Trilioni 1.6)* kwa mwaka zitaokolewa kutokana na mitambo iliyopo
nchini ikifua umeme kwa kutumia Gesi Asilia na kuachana na mafuta ambayo ni
ya bei kubwa sana. Bei ya umeme kwa uniti moja (KWh) ya umeme unaofuliwa
kutumia dizeli na mafuta ya aina nyingine ni kati ya *Senti za Marekani 30
hadi 45* na huku bei ya uniti moja hiyo hiyo *ni Senti za Marekani 6-8* kwa
umeme utokanao na Gesi Asilia na zinapungua na wakati wa matumizi.
Vilevile, takribani *Dola za Marekani millioni 202* kwa mwaka zitaokolewa
iwapo Jiji la Dar Es Salaam litatumia Gesi Asilia badala ya mafuta katika
magari, taasisi na majumbani. Fedha
5
hizi zikiokolewa zitatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa letu kwa
manufaa ya Wa-Tanzania wote wakiwemo wale waliondamana na wale walioratibu
maandamo ya Mtwara Mjini ya tarehe 27 Disemba 2012.
*(b) Umeme mwingi zaidi kutokana na Gesi Asilia:*
Bomba la Gesi Asilia linalojengwa litasafirisha gesi nyingi zaidi ambayo
itawezesha mitambo mipya itakayojengwa Kinyerezi (Dar Es Salaam) kufua
umeme wa zaidi ya MW 990. Umeme mwingine utafulia Somanga Fungu (Lindi) wa
kiasi kisichopungua MW 520.
*(c) Usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini mwetu*:
Dar es Salaam ndiko kuna miundombinu mikubwa ya usafirishaji na usambazaji
wa umeme kuliko mikoa mingine yote, hivyo ni uamuzi wa ki-uchumi
unaotulazimisha kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara na
kuipeleka Dar Es Salaam ambako itatumika kufua umeme, na kutumika moja kwa
moja viwandani, majumbani na kwenye magari.
*(d) Kwa kuzingatia mahitaji ya Gesi Asilia yatakayojitokeza:*
Bomba la kusafirisha gesi litawekewa matoleo ya kuchukulia gesi (*tie-off*)
katika maeneo ya Mtwara, Lindi, Kilwa na Mkuranga ili kuhakikisha kuwa miji
hii inakuwa na Gesi Asilia ya uhakika wakati wowote itakapohitajika. Kwa
hiyo kuweka mitandao ya usambazaji wa gesi kutoka kwenye Bomba la Gesi
Asilia linalojengwa kutarahisisha matumizi ya Gesi Asilia viwandani na
majumbani katika Mikoa ya Mtwara na Lindi, na kwenye mikoa mingine kwa siku
za baadae.
*(e)Serikali imetenga maeneo katika pwani ya Mikoa ya Kusini*
(Lindi na Mtwara) kwa ajili ya uanzishwaji wa maeneo ya viwanda *(Industrial
Parks/Estates)* vikiwemo viwanda vya mbolea, *Liquefied Natural Gas (LNG) na
* *Petrochemicals**.*
Ujenzi wa kiwanja cha sementi uko katika hatua za mwisho za maandalizi.
*(f) *Ili kutengeneza mazingira mazuri ya biashara ya Gesi Asilia na
Mafuta kwa kampuni za huduma, malighafi na vitendea kazi, Serikali imetenga
*eneo maalumu Mtwara,* ambalo litawekewa **
6
miundombinu ya msingi ili kutoa vivutio mbalimbali kwa makampuni hayo. Eneo
hilo litapewa hadhi ya *Ukanda Huru wa*
*Bandari (Freeport Zone).*
Ni lazima shughuli za kusafisha na kusafirisha Gesi Asilia zitatoa ajira
katika maeneo husika. Kwa mfano kwa mitambo ya kusafishia gesi inayojengwa
Madimba (Mtwara Vijijini) na SongoSongo (Kilwa, Lindi), kila mtambo
utahitaji wafanyakazi na wengine watatoka Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Watanzania wanakumbushwa kuwa raslimali zilizopo nchini ikiwemo gesi
asilia, madini, makaa ya mawe, wanyama pori, misitu, milima ya utalii,
mito, maziwa, bahari n.k ni za Wa-Tanzania wote kwa mujibu wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Raslimali hizi zinapatikana, zinatunzwa na
kuzalishwa maeneo mbalimbali nchini mwetu na mapato yake yanatumika
kwa *maendeleo
ya Wa-Tanzania* *wote bila kujali maeneo raslimali hizo zilipo.*
*Tusikubali kuvunja nchi yetu vipande vipade kwa kisingizio cha raslimali
zilizopo mikoani mwetu. Tusikubali kuvunjavunja mikoa yetu kwa kisingizio
cha raslimali zilipo kwenye wilaya zetu. Tusikubali kuvunjavunja wilaya
zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye tarafa zetu. Tusikubali
kuvunjavunja tarafa zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye kata
zetu. Tusikubali kuvunjavunja kata zetu kwa kisingizio cha raslimali
zilizopo kwenye vijiji vyetu na mitaa yetu.*
*MUNGU IBARIKI TANZANIA, DUMISHA UHURU NA UMOJA WETU*
*Prof Dr Sospeter Muhongo (Mb)*
*WAZIRI YA NISHATI NA MADINI*
*JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA*