Tanzania:
ALIYEWAHI kuwa mkuu wa wilaya tofauti hapa nchini wakati wa serikali ya awamu ya kwanza na baadaye kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ,Waziri Juma Waziri amefariki dunia akitibiwa hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es salaam Juzi na anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao Sungwi baada ya swala adhuhuri.
Kwa mujibu wa watu wa karibu na mzee Waziri, msiba upo nyumbani kwake Tandika Berege Nyumba namba tatu.
Mzee Waziri ambaye mwaka huu anatimiza miaka 89 alikufa siku chache tu baada ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.
Akiwa amehudumu katika wilaya mbalimbali zikiwamo Ngara, Pangani , Morogoro, Dodoma, Singida ni mmoja wa watumishi wa serikali waliofanyakazi kubwa ya kupambana na Nyarubanja, mfumo wa umiliki uliokuwa ukiendeshwa Mkoa wa Ziwa Magharibi.
Akiwa amesoma shule ya Msingi Pugu na kisha kusoma sekondari ya Minaki ni mmoja wa watanzania wa mwanzo waliokuwa na kazi kubwa ya kuonesha njia katika siasa za ujamaa na kujitegemea wakifuata maelekezo ya mwalimu.
Katika mahojiano yake ya Mwisho na wandishi wa habari waliokuwa wanatengeneza dokumentari, alisema kwamba wakati wa utawala wa mwalimu Nyerere, rushwa na matumizi amabaya ya ofisi yalikuwa ni mambo yasiyovumilika.
Aidha alisema kwamba viongozi walikuwa na kazi kubwa ya kuelimisha watu kuelewa utawala maana yake nini na kushiriki katika kazi za kujenga taifa kwa uhuru na kujituma zaidi.
Mzee Waziri ameacha watoto kadhaa, wajukuu na vitukuu.
Miongoni mwa watoto wake ni Maida Waziri ambaye ni mjasiriamali na mhamasishaji maarufu wa ujasiriamali nchini na barani Afrika.
Aidha Maida Waziri ni mmoja wa wanawake wanaojulikana sana katika sekta ya ujenzi nchini Tanzania akimiliki kampuni ya ujenzi ya Ibra Contractors.