Mhe. Ezekiel M. Maige (Mb)WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, Dar es Salaam:
Ndugu Wadau wa Misitu,
Natumia fursa hii
kuwafahamisha kuwa kuongezeka kwa mahitaji ya mazao ya misitu, kumesababisha
msukumo mkubwa kwa wananchi kutaka kuvuna mazao ya misitu kutoka kwenye
mashamba ya misitu ya serikali. Kutokana na msukumo huo wa mahitaji ni dhahiri
kuwa mabadiliko ya haraka yanahitajika ili kusimamia ipasavyo uzalishaji,
uvunaji na usimamizi wa bei ya mazao ya misitu. Mabadiliko haya yatafanikishwa
na wadau wa mazo ya misitu, hususan Sekta Binafsi na Wakala wa Misitu Tanzania
(Tanzania Forest Service – TFS).
Katika miaka mitatu iliyopita,
uzalishaji wa mbao umeshuka kutoka mita za ujazo 1,500,000 hadi 1,200,000. Kufuatia
kukua kwa uchumi watu wengi sasa wanahitaji kujenga nyumba za kisasa, hivyo mahitaji
halisi ya mbao kwenye soko yameongezeka kutoka mita za ujazo 2,000,000 hadi
5,000,000. Ongezeko hili limetokana pia na kupanuka kwa soko la nje hasa katika nchi za Kenya,
Djibouti, Sudan Kusini, Uarabuni na India.
Pamoja na ongezeko hili
la soko na kushuka kwa uzalishaji, hadi sasa
hakuna mabadiliko katika jitihada za kuongezeka kwa uzalishaji, wala Serikali
haijanufaika na ongezeko hilo la soko kwa sababu bei imeshuka kwa asilimia
thelathini (30%) kutoka bei ya juu ya mwaka 2007. Hali hii imesababisha utitiri
wa waombaji wa mazao ya misitu na malalamiko mengi kuhusu ugawaji wa vibali vya
uvunaji.
Kwa hiyo Serikali
imeamua kufanya mabadiliko ya muda mfupi ya utaratibu wa utoaji vibali kwa kuanzisha
fomu maalum ambayo itajazwa na waombaji.
Hata hivyo, mabadiliko haya
ni ya muda tu. Bado mabadiliko makubwa ya muda mrefu yanahitajika.
Maeneo yanayohitajika
kufanyiwa mabadiliko ni kama ifuatavyo::-
1. Kuongeza mapato ya Serikali
kwa kurekebisha bei ya tozo za Serikali angalau zifikie gharama halisi za
uzalishaji. Kwa sasa, bei ya kuuzia ni 54% ya gharama halisi ya uzalishaji wa miti
ya kutengenezea karatazi (“pulp”) na asilimia 90 kwa miti ya mbao.
2. Kuongeza mapato ya Serikali kwa kurekebisha bei
ya vibali vya kusafirishia nje ya nchi (export permits). Hii ni kwa lengo la
kuifanya nchi ifaidike na soko kubwa la nje na kukatisha tamaa ya kuuza mbao
nje ya nchi, hivyo kupunguza bei za mbao hapa nchini.
Aidha, Wakala wa Hudma
za Misitu Tanzania (TFS) umetakiwa kuimarisha ukaguzi katika mipaka kwa
kuanzisha vituo na kupeleka watumishi katika vituo vyote vya mipakani. Kwa sasa
kazi hiyo ya ukaguzi inafanywa na Maafisa Kodi wa TRA.
3. Kuweka udhibiti wa
bei kwa kuanzisha mfumo wa uzalishaji na usambazaji wa jumla na rejareja kwa
kuanzisha mawakala watakaopatikana kwa tenda ambao watauza mazao ya misitu kwa
bei elekezi itakayowekwa na Serikali.
4. Kuongeza uzalishaji
kwa kuweka mikataba na mawakala ya kuwataka wawe na mashamba yao katika kipindi
cha miaka 15 – 20. Kwa kufanya hivyo baada ya miaka 20 ijayo, angalau asilimia
arobaini (40%) ya malighafi za mbao itakuwa inatoka kwenye mashamba binafsi.
Kwa sasa asilimia tisini na nane (98%) ya mbao zinatoka kwenye mashamba ya miti
na hifadhi za misitu ya serikali.
Ili kufikia hatua hii,
mikataba iliyopo kati ya Serikali na wawekezaji itabidi irekebishwe au ivunjwe.
Majadiliano kuhusu suala hili, yanatakiwa yaanze sasa na mikataba mipya iwekwe kati
ya sasa na mwaka 2014.
5. Mapungufu ya
kimkataba na kiusimamizi yanayofanya wawekezaji wakubwa kuuziwa malighafi kwa
bei ya chini, huku wavunaji wadogo wakiuziwa malighafi hizo hizo kwa bei ya juu
yatarekebishwa kuanzia msimu ujao, Julai 2012. Aidha, ili kufikia lengo la
kuzalisha karatasi kamili hapa nchini, ruhusa ya kusafirisha karatasi ambazo
hazijafikia kiwango cha mwisho cha etengenezaji (“semi-processed papers”) itaangaliwa upya.
6. Ili kuimarisha
matumizi ya malighafi kidogo zilizopo, Wakala wa Misitu Tanzania – TFS unatakiwa
kuanza utaratibu wa kugawa malighafi kwa kutazama matumizi ambapo wavunaji
watakuwa wanapewa malighafi kwa kipindi kifupi, yaani kwa mwezi. Baada ya kuvuna
na na kumaliza kutumia, mvunaji ataandaa
taarifa itakayoonyesha malighafi hiyo ilivyotumika ndipo aweze kupewa mgao mwingine unaofuata.
Mabadiliko hayo ni badala
ya kupewa mgao wa mwaka mzima ambao wahusika huwa hawana uwezo wa kuutumia wote,
badala yake wanawauzia watu wengine kwa ulanguzi. Aidha, TFS ianzishe utaratibu
wa kugawa malighafi za “chips” kwa kiwanda cha karatasi cha Mufindi Paper Mill
(MPM), badala ya kugawa malighafi ya miti iliyokomaa kama inavyofanyika hivi
sasa.
7. Ili kuongeza motisha
na uzalishaji kwa wananchi waishio jirani na mashamba ya miti, TFS ianzishe
utaratibu wa kuwasaidia walimaji wadogo wa miti. Kadiri itakavyowezekana,
misaada ya ujirani mwema itakayotolewa na TFS kwa wananchi ilenge katika kuimarisha
sekta ya misitu.
Aidha, Mfuko wa Misitu
Tanzania (Tanzania Forest Fund – TFF)
uimarishwe kwa kuongezewa vyanzo vya mapato kwa kushirikisha wadau wa maendeleo.
Pia mfuko huo uimarishwe kiutendaji kwa kuwa na menejimenti yake ambayo itakuwa
inatoa mikopo ya muda mrefu na ruzuku
kwa wakulima wadogo wa miti.
8.
Ili kuongeza ulinzi kwenye mashamba ya Serikali, Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) uweke mkakati maalum wa kubainisha mipaka na kuilinda. Pia, TFS iandae
mkakati maalum wa kupanda miti kwa maeneo yasiyo na miti, ama, kwa kupanda
wenyewe au kutumia sekta binafsi kwa mikataba maalum ya muda mrefu (long term
concessations).
Kwa
mfano, Shamba la Miti la Sao Hill linaweza kuingia mikataba ya muda mrefu na
wadau maana ukubwa wa shamba hilo ni hekta 130,000, lakini zilizopandwa miti
hadi sasa ni takriban hekta 50,000 tu.
Yapo
maeneo mengi yanayoweza kuwekewa mikataba ya kupanda miti, kama vile mashamba
ya Serikali ya Buhindi mkoani Mwanza na Rubare mkoani Kagera.
9.
Ili kukabiliana na changamoto ya uvamizi wa maeneo ya hifadhi na mashamba ya
miti, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) uanzishe dawati maalum la
kusimamia migogoro kwa majadiliano na kwa kutumia taratibu za kisheria. ***** Ujumbe huu Ulitolewa kwa mara ya kwanza na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Ezekiel Maige kwa Wavunaji wakubwa wa misitu, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na wadau wengine wa misituSao Hill Mafinga tarehe 19 Machi 2012