Na Tulizo Kilaga
Wizara ya Maliasili na Utalii itawachukulia hatua wale wote
watakaokiuka sheria, kanuni na taratibu zinazotawala utekelezaji wa
mchakato wa kuwapata wawekezaji kwenye vitalu vilivyopo kwenye Maeneo
ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori (WMAs).
Akifungua warsha ya mafunzo kuhusu mchakato wa kufungua maombi ya
uwekezaji kwenye vitalu vya WMAs iliyofanyika katika Ukumbi wa Blue
Peel jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori,
Bw. Paul Sarakikya alisema mchakato husika utahusisha watu wenye uwezo
wa fedha hivyo unaweza kusababisha uwepo wa mazingira ya rushwa.
Alisema mchakato huo ni nyeti na unahitaji uadilifu na umakini mkubwa
katika kuutekeleza. Kushindwa kuzingatia vigezo vitakavyokubalika
katika mchakato huo kutasababisha migogoro isiyo ya lazima hivyo
kudhoofisha maendeleo ya Jumuiya na kukatisha tamaa vijiji
vilivyotenga maeneo kuanzisha WMAs.
“Napenda kusisitiza kuwa, Kanuni za WMAs zinazitaka Jumuiya kufanya
uteuzi wa wawekezaji kwa kutumia vigezo vilevile vilivyotumiwa na
Wizara kuwapata wawekezaji kwa kutumia vigezo vilivile vilivyotumiwa
na Wizara kuwapata wawekezaji kwenye vitalu vyake. Vigezo hivyo viko
kwenye Kanuni za Uwindaji wa Kitalii (2010) kifungu cha 10(2). Hivyo
washiriki watapata fursa ya kuvipitia na kuviwekea alama kwa
kuzingatia mahitaji na hali halisi ya WMAs, alisema Bw. Sarakikya.
Aliongeza kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii itashirikiana na vyombo
vya dola kufuatilia utekelezaji wa mchakato huu na haitasita
kuwachukulia hatua wale wote walioshindwa kuweka mbele maslahi ya
Jumuiya zao na ya Taifa kwa Ujumla,” alisema Bw. Sarakikya.
Bw. Sarakikya alisema kwa kutambua umuhimu wa mchakato wa ugawaji
vitalu hivyo Wizara ya Maliasli na Utalii imetoa Afisa kutoka Kitengo
cha Matumizi Endelevu ya Wanyamapori ili kutoa mafunzo. Hivyo Wizara
inatarajia wajumbe wote watakubalina na kuhitimisha hatua za
kimchakato zitakazotumika, na hatimaye kuwa na mwongozo utakaotumika
na Kamati zitakazo fungua maombi hayo.
Warsha ya Mafunzo kuhusu Mchakato wa Kufungua maombi ya uwekezaji
kwenye vitalu kwenye maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori
imelenga kuwawezesha wajumbe kupata uelewa wa pamoja wa nini cha
kufanya baada ya Jumuiya zilizo nyingi kuwa zimepokea maombi ya
uwekezaji kwanye vitalu vya WMAs kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori
Na. 5 ya mwaka 2009 na Kanuni za WMAs 2012.