Na Grace Mkojera :
Nchini Tanzania kuna watu zaidi ya milioni mbili ambao
wanaishi na virusi vya ukimwi huku wengine wakiwa bado hawajajitokeza kupima
ili kutambua afya zao.
Aidha, Takwimu mbalimbali za mwaka 2003 zinaeleza kuwa watu
wapatao milioni 25 waliokufa kwa Ukimwi katika Afrika, zaidi ya asilimia 90
wanatoka katika familia maskini sana.
Pia, zinaeleza kuwa vijana wa Afrika wapatao asilimia 62 wa
umri wa kati ya miaka 15 na 24 wanaishi na VVU na zaidi ya asilimia 60 wanatoka
katika familia maskini sana.
Miongoni mwa maeneo ambayo yameathirika hapa nchini kwa
ugonjwa wa ukimwi ni pamoja na wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani, ambayo
nilibahatika kutembelea siku za karibuni kuandika habari za kiutafiti juu ya
huduma kwa wagonjwa wa ukimwi ikiwa ni pamoja na kuangalia lishe na dawa na
jinsi mfumuko wa bei za bidhaa ulivyowaathiri ambapo niliwezeshwa na shirika
lisilo la kiselikari la Panos.
Wilaya hii ambayo ni moja kati ya wilaya sita zinazounda
mkoa wa Pwani, ambapo wilaya nyingine ni Rufiji, Mafia, Bagamoyo, Kibaha na
Mkuranga, wilaya hii kiutawala imewgawanywa katika tarafa nne, kata 15 na
vijiji 78.
Katika Wilaya ya Kisarawe kuna baadhi ya maeneo yanayoongoza
kwa kuwa na wagonjwa wengi wa ukimwi. Maeneo hayo ni pamoja na Maneromango na
Kisarawe ikiwa inaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa wa wagonjwa ukilinganisha na
sehemu nyingine.
Kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na Baraza la Misikiti
Tanzania katika eneo la Kisarawe inaonyesha kuwa ManeroMango ina wagonjwa 190,
wakati Kisarawe ina wagonjwa 127, Masaki ina wagonjwa 77, Kibuta inawagonjwa
101, Msanga ina wagonjwa 81 na sehemu nyingine zina wagonjwa wachache.
Watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wanahitaji kupata lishe
bora itakayowawezesha dawa wanazotumia kufanya kazi mwilini. Lakini wengi
hukabiliwa na hali ngumu ya maisha inayowafanya baadhi yao kutumia dawa kwa
muda mfupi na kisha kuziacha kwa kukosa lishe.
Dawa wanazotumia ni kali wakati mahitaji yake ni magumu kupatikana
kirahisi hasa ikizingatiwa kwamba wagonjwa wengi wanaishi kwa ndugu, jamaa na
marafiki. Jamii ya Kisarawe imekuwa ikitegemea zaidi kilimo cha Muhogo katika
kuwakomboa na umaskini na pia kutumika kama chakula.
Licha ya kutegemea muhogo kwa chakula na kukuza kipato chao
lakini bado wananchi wengi ni maskini wa kipato, wanaishi katika mazingira
ambayo ni hatarishi kwa maana kwamba hata baadhi ya nyumba wanazoishi ziko
katika hali mbaya. Kwa maana kwamba bado kilimo hakijawasaidia kujikomboa na
umaskini unaowakabili.
Watu wengi ambao wamekuwa wakikumbwa na ugonjwa huu kwa
asilimia kubwa wanaishi katika mazingira magumu, wamekuwa wakirudi karibu na
ndugu zao ili kupata msaada wa chakula na mahitaji mengine muhimu.
Nilipata nafasi ya kuzungumza na dada ambaye anaitwa Kurwa
Shomari mwenye umri wa miaka 34 ambaye pia ni mama wa mtoto mmoja. Kabla ya
kujitambua kama ni mgonjwa alikuwa akifanya shughuli za biashara ndogondogo na
mara baada ya kuumwa alilazimika kuwa karibu na ndugu zake na kuacha kazi alizokuwa
akifanya.
Kurwa anaishi na ndugu hadi sasa na amekuwa akimtegemea kaka
yake ampe fedha kidogo kwa ajili ya kutumia nauli kufuata dawa katika Hospitali
ya Kisarawe na pia hutumia kununua mbogamboga na matunda kwa ajili ya kula.
Hata hivyo, changamoto kubwa inayomkabili dada huyo ni
utegemezi kwa ndugu kwani hata wao wana familia zao na majukumu mengine ya
kifamilia.
Anasema “Kaka yangu ni mfanyabiashara, huwa namtegemea anipe
fedha ili ninunue yale mahitaji ambayo nimeshauriwa kutumia, hali yangu duni na
sina uwezo wowote wa kifedha, lakini kuna wakati huwa anasafiri na mimi huwa
wakati mwingine nahitaji kupata matunda lakini sina fedha za kununua,”.
“Dawa tunazotumia ni kali mno na tunahitaji chakula cha
nguvu ili miili yetu ipate nguvu, tutafanyaje wakati uwezo wenyewe sina?”
alisema Kurwa.
Siyo yeye peke yake ambaye huitaji msaada wa chakula ili
aweze kupambana na dawa anazotumia bali wapo wengi.
Nilifanikiwa pia, kuzungumza na Mganga Msaidizi wa Hospitali
ya Wilaya ya Kisarawe Dk. Stephen Kimweri ambaye amekuwa akitoa huduma za
ushauri kwa wagonjwa wa ukimwi Wilayani hapo alisema, wagonjwa ambao
huwahudumia wengi hutoka mbali akimaanisha kwamba wanatoka maeneo ya Dar es
Salaam kwa kuficha usiri.
Lakini pia, anaeleza kuwa miongoni mwa wengi walioko katika
maeneo ya Kisarawe ni maskini wa kipato kwani wengi hali zao ni duni.
Upatikanaji wa chakula miongoni mwa wagonjwa wengi ni mgumu.
Anasema kuwa dawa hufanya kazi vizuri ikiwa kuna lishe
nzuri. Uzoefu wake umebaini kuwa kuna idadi kubwa ya wagonjwa mtaani ambao
walikuwa wakihudhuria katika kliniki za kunywa dawa ambao wengine wameacha kwa
kuona kwamba hawana chakula.
“Wapo baadhi ya wagonjwa wanaona kwamba hawawezi kunywa dawa
kwasababu hawana chakula, na mara nyingi dawa hizi mtu anapokunywa husikia njaa
mara kwa mara hivyo, anahitajika kula kila asikiapo njaa na hilo ni tatizo
kubwa,”.
Hospitali ya Kisarawe imekuwa ikijitahidi kuwapa wagonjwa
dawa za ARVs kwa wakati ndio maana wengi hutoka katika maeneo ya Dar es Salaam
na Kwenda huko ili kupata huduma. Changamoto kubwa iliyopo ni kwa wagonjwa hao,
ambao wamekuwa wakitumia nauli kubwa kufuata dawa mbali.
Wengi wanategemea ndugu kuwasaidia nauli na mahitaji mengine
kufuata dawa na ikiwa watakosa tayari ni hatari kudhurika kiafya.
Pamoja na hayo, ili kutaka kujua zaidi iwapo kama Hospitali
ya Wilaya ya Kisarawe inatoa huduma ya lishe kwa wagonjwa wanaoshindwa kutumia
dawa kwa kukosa lishe, nilizungumza na Mganga Mfawidhi wa Kisarawe Dk. Rahim
Hangai ambapo alisema kuwa siku zilizopita walikuwa na utaratibu wa kutoa lishe
kwa wagonjwa.
Utaratibu wa kutoa lishe ulikuwa zaidi unategemea ufadhili
kutoka Shirika lisilo la kiserikali la ICAP. Anasema kuwa wamekuwa wakitegemea
bajeti ya Shirika hilo jinsi itakavyopangwa katika kuwahudumia wagonjwa hao.
Kwa mwaka huu bado hawajaweza kutoa msaada wa lishe kwa wagonjwa wa ukimwi.
Pia, katika mazungumzo na Baraza la Misikiti Tanzania ambalo
limekuwa likitoa huduma mbalimbali kwa wagonjwa wa ukimwi katika kata
mbalimbali za Kisarawe (Bamita-tunajali) walisema walikuwa wakitoa chakula kwa
wagonjwa hasa kutokana na asilimia kubwa ya watu wengi walikuwa hawana lishe na
wengi wanaishi katika mazingira magumu.
Bamita walikuwa wakitoa chakula mara nne kwa mwaka. Lakini
kwa vile walikuwa wakifanya kazi na baadhi ya mashirika ya nje, wadau wao
waliona ni muhimu zaidi kuwawezesha kujikomboa na umaskini kuliko kupewa
chakula na kutumia kwa siku moja kisha shida iko pale pale.
Mratibu wa Mradi wa Bamita Ally Mandai anaeleza kuwa utoaji
wa chakula kwa wagonjwa sio suluhisho, bali suluhisho ni kuwapa uwezo wa
kuzalisha chakula ambapo waliandaa mkakati wa kuwawezesha wagonjwa katika kata
nane za Kisarawe.
Alisema tayari wametafuta mashamba hekta 18 na nusu ambayo
yatakuwa yanamilikiwa na wagonjwa ambao wameunda vikundi katika vijiji, lengo
hasa ni kuweza kuzalisha chakula kwa wingi kwa ajili yao na pia kufanya
biashara itakayowakomboa kutoka katika hali ngumu wanayokabiliwa nayo.
Alisema walikuwa wakitoa mbegu za mahindi, ufuta, mpunga na
mihogo. Hata hivyo, anasema changamoto bado kubwa hasa ya fedha ili kuweza
kutimiza malengo waliyojiwekea ya kusaidia vikundi vinavyoishi na virusi vya
ukimwi.
“Baadhi ya maeneo yalifanikiwa na kuwa na maendeleo lakini
pia kuna maeneo mengine hatukufanikiwa hasa kutokana na watu wengine katika
kundi kuwa wavivu, tumeamua kwa sasa tutafute mtu mmoja mmoja katika kundi ndio
awe mzalishaji mali lakini pia awe na mchango katika kikundi chake,”alisema.
Alisema umaskini ni sehemu ya ongezeko la ukimwi katika
maeneo ya Kisarawe huku akitolea mfano wa baadhi ya akina dada ambao hujiuza
katika eneo la Buguruni jijini Dar es Salaam wengi ni wenyeji wa Kisarawe.
Mandai alibainisha kuwa sababu kubwa ya vijana wengi kutoka
Kisarawe na kwenda sehemu nyingine kutafuta fedha kwa njia ya ngono inatokana
na wengi kuwa ni maskini wa kipato. Lakini mbaya zaidi wanapougua ugonjwa huo
hulazimika kurudi tena katika hali duni nyumbani kwao.
Alisema Ukimwi unachangia kwa kiasi kikubwa kuwa na
umaskini, kwasababu watu ambao ni wazalishaji wanapougua wanashindwa kuzalisha,
hivyo kusababisha pia Mkakati wa kupambana na Umaskini kukwama.
Lakini pia, anabainisha chanzo cha umaskini katika eneo la
Kisarawe kwamba jamii ya pale imekuwa ikitegemea zao moja la muhogo kukuza
uchumi, hili husababisha umaskini, pia anasema kukosa viwanda vya kusindika
mazao, ubovu wa miundombinu pamoja na elimu duni kuhusu uzalishaji huchangia
kuendelea kuwepo kwa umaskini sio tu kwa upande wa Kisarawe peke yake bali pia
hata kwa taifa.
Mandai anasema wagonjwa wa ukimwi wanapata mateso hasa
kutokana na mfumuko wa bei kuendelea kuwa juu. Wanahitaji kufikiwa maeneo
wanayoishi ili kuhudumiwa lakini kutokana na hali ngumu hivi inashindikana.
Wagonjwa wanapohitaji mahitaji muhimu kwa ajili ya lishe zao
inashindikana hasa kutokana na bei za bidhaa mbalimbali kuwa kwa kiwango cha
juu, hivyo kuwa ngumu kupata kile wanachokihitaji.
Serikali hivi karibuni ilitangaza kuwa kuna bodi ambayo
itakuwa ikishughulikia tatizo la bei za bidhaa, na matumaini makubwa
yanategemewa kutekelezwa mapema ili jamii maskini ipate yale mahitaji muhimu.
Anasema kuwa limewagusa hata wao hasa kutokana na kwamba
viwango wanavyokadiria katika bajeti na jinsi hali inavyokwenda ni tofauti,
hivyo anaomba serikali kushughulikia tatizo hilo mapema ili kuwasaidia maskini
ambao kipato chao ni kidogo.
Mandai amekuwa akifanya kazi na wagonjwa wa ukimwi kwa muda
mrefu anaeleza kuwa wagonjwa wengi huishi katika mazingira magumu na makazi
duni. Kwa maana kwamba wengi huishi kwenye nyumba ambazo ni za nyasi kiasi
kwamba ikinyesha mvua kubwa watadhurika.
Pia, anasema hata vitanda ambavyo wagonjwa katika maeneo
hayo wamekuwa wakilala ni vile vitanda vilivyotengenezwa kwa magunia, ambavyo
vilikuwa vikitumika miaka ya zamani. Pia, vingine havina godoro.
Wagonjwa wanahitaji kuishi sehemu nzuri kutokana na hali
yao. Lakini ni tofauti kwa baadhi ya maeneo watu wanateseka kwa kiasi kikubwa.
Hawana chakula, makazi ni mabovu hivyo pia hata uhakika wa kuishi kwa muda mrefu
ni mgumu pia.
Mandai anaona kuwa kutokana na wananchi wengi hasa wagonjwa
wa ukimwi kuishi kwenye mazingira magumu kama hayo, kuna haja mapambano ya
kupunguza umaskini nchini yaendane sanjari na mapambano dhidi ya ukimwi.
Ikiwa serikali itakuwa inazungumzia tu Mkakati wa kupunguza
umaskini na kukuza uchumi bila kuzungumzia Mkakati wa kupambana na ukimwi
itakuwa inakosea, na wapo wadau mbalimbali wanahamasisha yote kwa pamoja
yapambaniwe pamoja.
Kwa upande wake, Mratibu wa Ukimwi Wilaya ya Kisarawe Rehema
Mwika anasema kuna haja ya jamii kuwezeshwa ili kupunguza matamanio ya kupata
fedha za kujikumu kimaisha.
Anaamini kuwa”Ikiwa jamii hasa wanawake watawezeshwa
itasaidia kwa kiasi Fulani kupunguza maambukizi ya ukimwi kwa vile wanawake
ndio huongoza kwa asilimia kubwa kupata maambukizi kutokana na maumbile
yao,”alisema.
Aliongeza kuwa ni muhimu ugonjwa wa ukimwi ukaenda sanjari
na mapambano dhidi ya umaskini, kwa vile yakiondolewa kwa pamoja itasaidia
kupunguza kasi ya maambukizi ya ukimwi.
Baadhi ya wanaharakati wanaeleza kuwa ili kufanikiwa
kupambana na janga la ukimwi elimu juu ya kufuta umaskini itolewe sanjari na
elimu juu ya kujikinga na magonjwa ya maambukizi likiwemo gonjwa hilo hatari la
ukimwi.
Fatma Alloo ni mwanaharakati wa siku nyingi nchini anaeleza
kuwa bila kuzungumzia umaskini na kutafuta mbinu za kuweza kutatua tatizo hilo
hata mapambano dhidi ya ukimwi hayawezi kuisha kwasababu watu wataendelea na
kutafuta fedha kwa njia ya kujiuza na nyinginezo na kuongeza kasi ya maambukizi
hayo.
Alisema watu wengi wa vijijini hasa wanawake na wasichana
huwa wanatumia nafasi ya kujiuza au kumuozesha mtoto wa kike ili tu aweze
kupata mali na hivyo kusababisha kupata matatizo.
Hiyo yote ni kutokana na kukabiliwa na hali ngumu ya maisha
ndio maana wanawake wengi wa maeneo hayo wanajikuta wanaingia katika vishawishi
vinavyomwingiza kwenye matatizo hayo.
Ni katika familia za watu maskini ambako hali ya kiuchumi
inawafanya wanawake kugeuzwa zana za ngono, tena katika umri mdogo. Ni huko
ambako mahusiano ya kujamiiana yanaanza mapema na bila elimu juu ya matokeo
yake.
Alloo anaeleza kuwa wanawake hao mara nyingi hutoka maeneo
ambayo wazazi au watu wanaendelea kuamini mila na desturi ambazo hazina muda wa
kuwahamasisha wasichana kusema hapana pindi wanapokutana na vishawishi vya
wanaume wanaotumia fedha kuwalaghai wasichana.
Ushahidi wa umaskini huo ni utafiti wa mwaka 2003 unaoeleza
kuwa kuna zaidi ya watoto yatima milioni 43 katika Afrika na kati ya idadi
hiyo, milioni 12 wakiwa wanatokana na vifo vilivyosababishwa na Ukimwi.
Mwisho.
2. Muhogo: Zao la biashara lililochukua nafasi ya nazi na
korosho Kisarawe
Baadhi ya wakulima wanalalamikia kutofaidika ipasavyo
Na Grace Mkojera
Kwa miaka mingi iliyopita Kisarawe ambayo ni Wilaya ya Mkoa
wa Pwani ilikuwa ikijulikana kwa zao lake la biashara ya Korosho na Nazi.
Kilimo hicho kilichukua nafasi kubwa kwa wakati huo na hivyo kuifanya jamii ya
eneo hilo kulima nazi kwa wingi ili kuinua uchumi wao na Wilaya hiyo.
Pamoja na kuwa inaaminiwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo na
ndicho kinategemewa zaidi nchini katika kuinua uchumi wa nchi, lakini pia, bado
kuna matatizo mengi ambayo huwakumba wakulima hasa wadogo katika kufikia
malengo yao ya kimaisha.
Mwandishi wa Makala haya alifanya utafiti katika baadhi ya
kata za Kisarawe ambazo ni Masaki na Msanga kwa ufadhili wa Shirika la Panos
ili kuangalia kama pamoja na kuwepo kwa mazao ya nazi na muhogo kama mazao ya
biashara kwanini bado kuna umaskini.
Wakazi wa Kisarawe wana utajiri mkubwa wa ardhi lakini wengi
hawajui kuitumia. Na mara tu wanapoona serikali inachukua maeneo kwa ajili ya
kuwapa wawekezaji ili kuwekeza kwa manufaa ya mkoa na Taifa kwa ujumla ndipo
wananchi wanaanza kuzinduka na kulalamika kuhusu kuchukuliwa kwa ardhi hiyo.
Kwa asilimia kubwa wananchi wa Kisarawe ni Wazaramo.
Ilifahamika miaka iliyopita kuwa wamekuwa hawatafuti mbinu kujikomboa kiuchumo
bali wengi wamekuwa wakijuhusisha katika mambo ambayo hayamsaidii kujikomboa
ikiwa ni pamoja na kuthamini ngoma zaidi kuliko kufikiria nini cha kufanya ili
kusonga mbele.
Hata hivyo, kwa kipindi hiki kuna baadhi ya makabila
yameongezeka kutokana na kazi mbalimbali. Licha ya utajiri wa ardhi walionao
bado hawajui kuitumia ipasavyo.
Historia inaonyesha kuwa Kisarawe iliundwa rasmi mwaka 1906
na ilianzishwa na watawala wa Kijerumani.
Baadaye mwaka 1945 baada ya vita kuu vya pili vya dunia,
wilaya hiyo iliendelea kuendeshwa na watawala wa kikoloni wa Kiingereza. Kwa
kipindi hicho ni kirefu sana kwa binadamu kufikia maendeleo .
Lakini, hivyo si ilivyo kwa wilaya hiyo kongwe ambayo kwa
kweli bado imebaki kuwa nyuma zaidi kimaendeleo ikilinganishwa na nyingine
zilizoanzishwa katika miaka ya hivi karibuni. Ni wilaya ambayo kiuchumi
kiuchumi bado iko nyuma.
Zao la Korosho ambalo lilikuwa likithaminiwa zaidi Kisarawe
liimebaki likizalishwa katika maeneo machache ikiwemo Kata ya Msanga na maeneo
mengine ya mkoa wa Pwani, lakini katika maeneo mengine watu wamekata miti hiyo
hasa baada ya wakazi wa eneo kushindwa kuitunza hivyo kushambuliwa na magonjwa.
Vile vile, kwa zao la nazi, miti mingi imetelekezwa
mashambani , na mingine kutokana na kutotunzwa vizuri imeshambuliwa na ugonjwa
unaojulikana kama Mwarabu. Licha ya kwamba kwa sasa nazi inauzika sokoni kwa
maana kwamba hata bei imepanda kwa kasi mtaani lakini bado wakazi wa eneo hilo
hawajaona umuhimu wa kuliendeleza na kuwa zao la biashara.
Pia, muhogo ni zao ambalo hutegemewa kwa asilimia 60 na
wakazi wa eneo hilo kama chakula kikuu na pia, kama zao la kuwakomboa na
umaskini.
Ili kutaka kujua ni kwanini mikorosho na nazi haijapewa
kipaumbele katika eneo la Kisarawe na hivyo zao la muhogo kuthaminiwa zaidi
nilizungumza na baadhi ya wakulima ambapo wengi walisema kwamba Korosho na nazi
huchukua muda mrefu kuzaa wakati wao wanataka zao ambalo watavuna mapema na
kuuza ili liweze kuwasaidia kujikomboa na maisha.
Mmoja wa wakulima hao ni Said Kisomahaki ambaye ni mkulima
wa mazao mbalimbali yakiwemo muhogo na matunda katika eneo la Sungwi Masaki.
Anasema nazi huchukua umri wa miaka saba ili kuzaa, wakati muhogo huchukua muda
wa mwaka mmoja, hivyo anaona kuwa ni muhimu kulima muhogo kwa wingi.
Anasema kuwa muhogo umemsaidia kujikomboa kwa vile kwa sasa
ni zao ambalo linauzika kwa wingi ndani na nje ya nchi.
“Muhogo umekuwa ukitusaidia sana kuliko korosho na nazi,
tunauza sana na kuna wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitufuata shambani ,
tumeweza kufanya mambo mbalimbali ya kimaendeleo kama kuwasomesha watoto,
kuboresha nyumba tunazoishi na shughuli nyingine,”alisema.
Anasema hata kibei muhogo uko juu, anaeleza kwa mfano kwamba
wamekuwa wakiuza zao hilo kwa steki kwa maana kwamba gari aina ya kenta chuma
ya juu hadi chuma nyingine ni shilingi laki moja na nusu, tena hiyo ni kwa sasa
kutokana na magonjwa katika muhogo.
Kisomahaki anasema siku chache zilizopita walikuwa wanauza
muhogo zaidi kuanzia laki mbili hadi tatu kwa steki lakini kilichofanya bei
kuanguka kidogo na magonjwa ya muhogo, wafanyabiashara wengi wanaogopa kwa sasa
kununua muhogo shambani.
Wakati Kisomahaki akiona kwake kuna unafuu mkubwa, baadhi
waliona kuwa zao hilo haliwasaidii ipasavyo hasa baada ya kuvamiwa na magonjwa
na hivyo kuambulia migogo michache ambayo wamekuwa wakitumia zaidi kwa chakula
na kuuza michache ambayo bado fedha wanazopata haziwasaidia kujikomboa na
umaskini.
Kuruthumu Mizoka ni miongoni mwa wakulima ambao anasema bado
hawajaona mafanikio yoyote kutokana na mazao hayo ya biashara.
Anasema toka aanze kulima mazao hayo kwa maana ya muhogo,
nazi na korosho amekuwa akipata fedha kidogo, na hata hivyo bado wanaishi
katika mazingira magumu kutokana na kuwa fedha anazopata kutokana na mazao hayo
ni kidogo kiasi kwamba inabidi azitumie kwa chakula tu.
Mizoka anasema gharama za maisha ni kubwa kwa sasa na fedha
wanazopata hata wakitaka kununua bati ili kujenga bado hazitoshelezi. Wengi
inawalazimu kuishi katika nyumba za udongo na nyasi, ambazo huatarisha usalama
wao.
Hata hivyo, licha ya kuwa muhogo hutumia pia kama zao kuu la
uchumi lakini pia ni zao kuu la chakula, hivyo wakati mwingine wanapouza na
kupata fedha, huzitumia fedha hizo kubadilisha vyakula vingine.
Mkulima mwingine wa muhogo katika kata ya Masaki ni
Ramadhani Kitenga kwa upande wake anasema kilio kikubwa kwao ni magonjwa ya
muhogo ambayo yamekuwa yakishambulia zaidi zao hilo na hivyo kujikuta wakipata
mavuno machache.
Lakini yeye alikuwa tofauti ni Mizoka anasema muhogo
umemsaidia kujenga nyumba ya kisasa na kusomesha watoto. Kwa hayo, anaona ni
mafanikiwa makubwa kwake. Pia, ameweza kununua vyerehani vitatu na baiskeli
ambayo humsaidia kusafiria na kwendea shambani.
Pamoja na hayo, Afisa Ugani wa Kilimo wa Kata ya Masaki
Kisarawe Sahabi Namkumbe alisema jambo kubwa lililosababisha wakulima wengi
kuacha kulima korosho na nazi ni kutokana watu kwa sasa kushindwa kuyaendeleza
mashamba ya urithi walioachiwa kwani miaka ya zamani waliokuwa wakiendeleza
mazao hayo ni wazee waliopita.
Alisema watu wamekuwa wavivu, hawataki kufuata utaratibu wa
kuandaa mashamba hivyo kuwa rahisi kwa wadudu na magonjwa kushambulia
kiurahisi. Pia, anasema wengi wameona muhogo unawapa unafuu mkubwa hasa
kutokana na mapato wanayopata kuwaridhisha.
Kwa upande wake Mtaalam wa Mazao wa Wilaya ya Kisarawe Wetu
Nguzo ambaye alizungumza kwa niaba ya Afisa Kilimo wa Wilaya hiyo Dk. Kissamo
Minja, alisema wakazi wa Kisarawe hawataki kufuata kanuni za kilimo bora ikiwa
ni pamoja na shamba kuandaliwa kwa wakati na kutokuwa na mpangilio wa mazao
ndipo kunakosababisha wakulima kushindwa kufaidika ipasavyo.
Anasema “Wengi wanasubiri mvua inapoanza kunyesha ndipo
utawaona wanaanza kuandaa mashamba, jambo ambalo halitakiwi, akaongeza kuwa,
shamba linatakiwa kuandaliwa msimu wa jua na hivyo, hata mvua inapoanza
kunyesha linakuwa tayari limepata nafasi,”.
Nguzo anasema wakulima wanashindwa kunufaika ipasavyo
kutokana na kuwa wafanyabiashara huenda kuwanunuza bidhaa zao kwa bei ya chini,
wakati wao wanapopeleka sokoni huuza kwa bei ya juu hivyo kunufaika zaidi.
Anasema tatizo linalowasumbua wakulima wengi ni kushindwa
kuhesabu muda aliotumia na nguvu, wamekuwa wakilima ilimradi siku ziende.
Wamekuwa wakitoa elimu kwa wakulima lakini wengi wanaonekana kutofuata taratibu
wanazopewa ndio hawafaidiki.
Nguzo anasema katika kuhakikisha Wilaya ya Kisarawe
inaendelea kiuchumi msisitizo mkubwa wa serikali ni mazao hayo yauzwe kwa mfumo
wa stakabadhi mazao ghalani , ambapo katika maeneo mengine nchini kama Lindi na
Mtwara wamekuwa wakitumia mfumo huo ili wakulima waweze kunufaika.
Pia, wakulima wadogo wadogo wanahamasishwa kuwa na vikundi
vya ushirika ili waweze kujipangia bei za bidhaa zao, hata ikiwezekana
watanufaika kwa vile wataweza kujiendeleza na kuendeleza kilimo chao kwasababu
watakuwa na nafasi ya kukopa na kuendeleza kilimo.
Hiyo, itawasaidia kwa kiasi Fulani kutokandamizwa na
wafanyabishara wakubwa, kwa vile pia watakuwa na uwezo kwa kununua hata gari
ambalo litawapekelekea bidhaa zao sokoni na kuuza wenyewe kwa bei wanazotaka.
Mwisho.