HOTUBA YA MAOMBOLEZO
Na Ndugu Elly Kimbwereza
KIFO CHA MSANII MKONGWE HODI MAME SIKU YA MAZISHI YAKE IJUMAA TAREHE 6-2-2015 MBAGA
Nasimama mbele yenu, kama mwakilishi wa Tona Lodge na mratibu wa utalii wa kiutamaduni na asili milima ya upare nikiungana nanyi nyote kwa majonzi ya msiba uliotupata. Kijiji kinaombeleza na dunia nzima imeguswa.
Tumeunganishwa wote hapa si kwa ajili ya kutoa heshima zetu tu kwa mzee Hodi mame bali pia na hitaji la kufanya hivyo.
Hodi Mame alikuwa na mvuto wa kipekee kwa maelfu ya watu hapa duniani na hivi sasa ulaya na Marekani wako watu wanaomboleza msiba huu uliotokea jioni ya Ijumaa kama wamepoteza mtu aliyekuwa wa karibu nao.
Leo ni siku yetu ya kipekee kukuambia asante sana mzee Hodi Mame kwa namna ulivyong’arisha maisha yetu ingawaje Mungu imempendeza akuchukue.
Tunajihisi kama uliyepokonywa mikononi mwetu lakini ni vema tukajifunza kushukuru kwamba angalao tulipata bahati ya kuwa nawe.
Sasa umetangulia ndipo tunapotambua tutakachokosa na tunataka ujue tu kwamba shughuli zetu bila wewe zitakuwa ngumu kweli kweli.
Wote tuko katika hali ya kukata tama kwa kukupoteza na nguvu pekee uliyotubakishia ni ujumbe uliotuachia kupitia kipaji chako ambapo tunapata nguvu ya kusonga mbele.
Tutakukumbuka sana kwa kipaji chako cha ucheshi na namna yako ulivyoshangilia maisha yako na tabasamu lako ulipocheka na macho angavu yasiyoweza kusahaulika na nguvu na mbwembwe za ajabu ulipocheza kwa ajili yetu.
Lakini zawadi kubwa aliyokupa Mungu ni namna ulivyoweza kuishi kwa kufuata hisia zako na ulitumia zawadi hiyo vizuri.
Marehemu aliwahi kufanya kazi katika wizara ya Utamaduni wa Taifa na vijana chini ya marehemu Mbunge wa Same na waziri Chediel Mgonja.
Mwalimu Nyerere alipoanzisha wizara ile alisema na nukuu. ‘‘Nimeanziasha wizara hii kusaidia kurudisha heshima na fahari ya utamaduni wetu.Natafuta yale yaliyo bora kabisa katika mila na desturi zetu za makabila yote na kuyafanya sehemu ya utamaduni wa Taifa. Lakini singependa mtu yeyote afikirie kwamba kufufua tamaduni zetu maana yake nikudharau tamaduni za nchi nyingine . Taifa linalokataa kujifunza mila na desturi kutoka mataifa ya nje ni Taifa la wapumbavu na vichaa. Binadamu hangeweza kupata maendeleo yaliyofikiwa kama tungekataa kujifunza kutoka kwa wengine lakini kujifunza toka Tamaduni zingine haina maana ya kuacha utamaduni wetu. Aina ya kujifunza kwa manufaa ni ile inayosaidia kupanua wigo wa tamaduni zetu. Mwisho wa kunukuu.
HODI MAME ni nani kwetu?
Mchango wake kwa maendeleo ya Tona Lodge na Mbaga na Taifa kwa ujumla ni mkubwa kuliko wengi mnavyojua.
Alishawahi kwenda Addis Ababa Ethiopia na hayati Mwl. Nyerere kwenye mkutano wa marais wa Afrika kuonyesha ngoma za utamaduni wa Tanzania.
Yeye na kikundi chake waliwahi kualikwa sherehe za uzinduzi wa kitabu kuhusu utalii katika milimam ya Upare jijini Dar es Salaam.
Binafsi nilipoteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya mfuko wa Utamaduni hapa nchini yeye na kikundi chake walialikwa Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa Bodi ya mfuko.
Ushiriki wake sherehe za kupokea mwenge wa uhuru unajulikana nasi sote. Wakati yeye anapamba ukurasa wa mbele wa kitabu kihusisho utalii upareni – Mke wake mama Hodi Mame anapamba ukurasa wa mbele wa kitabu cha kijerumani kihusicho maelekezo ya sehemu za kutalii duniani (Germany Reisen Hower)
Alishiriki kikamilifu sherehe za miaka 100 ya Jubilee KKKT Mbaga mimi nikiwa mwenyekiti wa kamati ya maandalizi yale.
Mchango wake katika sanaa na burudani ni mkubwa. Sanaa ni fani muhimu ya utamaduni ambayo ni ustadi wa kuweka na kupanga fikra kwa njia ya hisia au zana. Ambapo burudani ni shughuli ambazo mtu anazifanya kwa hiari yake ili kurudisha nguvu,akili na ari baada ya kazi. Changamoto kubwa ni namna ya kubuni aina na taratibu nzuri zitakazoifanya burudani kulenga zaidi kwenye kuimarisha maadili, kuongeza ufanisi katika kazi, kuwaongezea wananchi kipato na kujenga undugu na mshikamano katika jamii.
Baada ya kusema hayo sasa nitamke tu kwamba sisi wa Tona Lodge tunatoa ubani wetu kwa kugharamia sanda, jeneza na fedha taslim sh. 100,000/- kwa mjane wa marehemu.
Nawashukuru kunisikiliza na Mungu wetu awatie nguvu na moyo wa ustahamilivu.