JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

TAARIFA KWA UMMA
TANZANIA IMECHAGULIWA KUWA MWENYEKITI WA MKUTANO MKUU WA
UHIFADHI WA URITHI WA UTAMADUNI – ICCROM, UNAOFANYIKA ROMA TAREHE
14/11/2011 HADI 16/11/2011

Bw. Donatius Kamamba, ambaye ni Mkurugenzi wa Mambo ya Kale katika
Wizara ya Maliasili na Utalii, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mkutano
Mkuu wa Baraza la Kituo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Uhifadhi na
Ukarabati wa Urithi wa Utamaduni (ICCROM). Uchaguzi huo umefanyika
wakati wa Mkutano Mkuu wa ICCROM ambao unaendelea mjini Roma Italia,
tangu tarehe 14/11/2011 hadi 16/11/2011.

Hii ni mara ya kwanza toka kuanzishwa kwa kituo hicho, nafasi ya
uwenyekiti kushikwa na mjumbe kutoka Bara la Afrika.

Kituo hicho cha International Center for the Preservation and
Restoration of Cultural Property (ICCROM) kilianzishwa mjini Roma,
Italy mwaka 1959, na hadi sasa mji huo ndiyo makao makuu yake.
Kuanzishwa kwa kituo hicho ilikuwa matokeo mkutano wa UNESCO
uliofanyika mjini Delhi mwaka 1956.

Tanzania ni nchi mwanachama wa kituo hicho toka mwaka 2004. Bw
Donatius Kamamba, alichaguliwa na Baraza la ICCROM kuwa mjumbe wa
baraza hilo kuwakilisha Tanzania kwa mwaka 2007 – 2013. Muda wake wa
uwakilishi utakapomalizika mtalamu mwengine kutoka Tanzania
atapendekezwa kugombea nafasi hiyo.

Kituo cha ICCROM kwa sasa kina idadi ya nchi wanachama hai 128, ambao
wamesaini mkataba kwa nyakati tofauti. ICCROM, hutoa misaada ya
kifedha inayowezesha kuendesha shughuli za Uhifadhi wa Rasilimali za
nchi mbalimbali, na kuwezesha tafiti muhimu kufanyika.

George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
16 Novemba 2011