Chadema Kuapisha watu na hatari ya usalama

Na John Kimbute

BADO mjadala unaendelea kuhusu hatua ya wakuu wa majeshi ya ulinzi na
usalama kutoa tamko rasmi kuwa hakuna atakayeruhusiwa kukataa matokeo, tamko
ambalo limepata upinzani mkubwa kutoka kwa vikundi tofauti vya jamii, na
kupelekwa malalamiko balozi mbalimbali. Inavyoelekea mabalozi au ofisi za
kibalozi zilizopelekwa malalamiko hayo walipendelea kuwatuliza
waliolalamika, wakiainisha matazamio yao kuwa uchaguzi ujao utakuwa wa huru
na wa haki. Ni mazingira ambako mgawanyiko ulikuwa bayana – kuwa wanaounga
mkono hisia za ‘damu itamwagika’ wanaona ni hisia za kisiasa, na si suala la
usalama.

Ni jambo la kushangaza kuwa watu walitazamia kuwa hali ya kuashiria ‘damu
kumwagika’ iachwe hivyo ilivyo, kana kwamba ni sehemu tu ya ukereketwa wa
kisiasa, na siyo tangazo la vita ambalo inabidi wale wanaohusika na tangazo
hilo walijibu. Kwani hata kama kuna wasiwasi wa kuiba kura, kinachofuata
baada ya hapo ni amani, kwa mujibu wa fikra ya Mahatma Gandhi, na hata kwa
upande wa Mwalimu Nyerere mwaka 1958, ambako alikuwa bado hajafikiria
masuala ya ‘vita vya ukombozi’ ikiwa hujuma ingeelekezwa kwa TANU. Haina
maana kuwa usiporidhika ‘damu inamwagika,’ au muulize Maalim Seif.

Kwa upande mwingine, ni kweli kuwa inawezekana kukitokea hali ya chama
fulani kutoridhika na jinsi kura zilivyohesabiwa, uvunjikaji wa amani
unaweza kutokea. Lakini kubadilika kwa hali hiyo na kuingia katika mchakato
halisi wa ukinzani wa kisiasa au kuchukua silaha haitokani na mazingira ya
kura yalivyo ila mkondo wa matazamio na mvutano kijamii unaoendana na
upigaji kura, na hata kuzihesabu. NI ile mantiki ya ‘vita ni siasa kwa
nyenzo nyingine,’ na hivyo kuingilia mtiririko wa kura na uwezekano wa hali
ya siasa kuchafuka inatokana na siasa, au hali halisi. Si chama kinachoamua
kuwa sasa ‘tumwage damu.’

Ikiwa chama cha siasa kinaamua kuingia msituni na mazingira ya kupambana na
dola iliyopo hayapo bado, ‘kinajimaliza chenyewe’ kwa sababu inaowawakilisha
wanakipendelea kwa kura, lakini si kwa kuacha familia zao wakifuate chama
msituni. Kuchukua silaha kunafuatana na hali halisi ya kijamii ambayo
inawezesha mapambano kufikia hatua ya juu zaidi, na ina maana chama hicho
kinaungwa mkono kwa kina, kwa mahitaji na mtazamo yakinifu au adilifu. Ikiwa
kimejikusanyia mashabiki tu kwa haraka na kiko katika mtandao wa maslahi
kama makundi mengine ya jamii, inakuwa ni matamshi tu.

Hata hivyo suala hili la ‘damu kumwagika’ katika mazingira ya uchaguzi mkuu
siyo la nadharia katika hali ya awali ila tabia, kuwa anapoona mambo
yanamwendea vyema, mwenyekiti wa Chadema anaanza hulka za kuapisha watu, ni
kama ‘kupandisha mashetani.’ Kutaka watu waape kuichukia serikali ni
kutafuta damu kwa nguvu, na pia kuleta mfumo wa utumwa, kwani mtumwa
akishanunuliwa anakuwa na utii usiotiwa shaka kwa bwana wake, kwani hana
nafsi ila ni mali ya bwana wake. Katika mfumo wa demokrasia mtu hawezi
‘kuapisha watu’ waichukie serikali kwani ni kuwageuza kuwa watumwa wake.

Ndiyo alivyoanza kufanya Freeman Mbowe kuanzia pale ‘mduara’ wa Mwembeyanga
na uongo wa EPA kuanza kuzunguka, kwa vile tu serikali haiwezi kumwaga mtama
hadharani ikaeleza kilichotokea, ila katika vikao husika, ili wawakilishi
huko waeleze kwa waliowatuma vikaoni. Sasa akitoka mtu katika kikao akakataa
yaliyoelezwa, na ni mbunge wa watu, inakuwa vigumu kuwa na umoja wa chama au
kuzuia umma ‘usidanganyike’ kuwa kuna mtu anaweza ‘kuchotewa’ sh. bilioni 40
atie tu kibindoni, kwa vile ni ‘swahiba’ wa mtawala, n.k. Ni katika mandhari
hayo ambako ‘mashetani yanapanda’ viapo vianze.

Ukiangalia katika uchaguzi mkuu wa sasa, kinachogomba ni uongo kuhusu nini
kilitokea mwaka 2005, ambako mfumo wa siasa ‘unaona haya’ kukiri kuwa
inabidi watu walipiwe madeni waingie katika kampeni, walipiwe muda wa
maongezi katika simu ili waweze kufanya kampeni. Ni hali halisi kuwa vipato
vya wastani vya Watanzania na mpangilio wa kodi katika matumizi ya simu za
mkononi unaleta ukizani katika uendeshaji wa siasa au demokrasia, hivyo
inabidi ‘kazi ya ziada’ ifanyike. Pia uwezekano upo wa kada tofauti za watu
kufaidika na hali hii, lakini haitofautiani na kufaidika katika miradi
mingine.

Upande mwingine wa uhatarishi wa usalama kutokana na mpangilio au uelekeo
hasi wa kupiga kura ni athari za kushindwa kufanya mageuzi ya uchumi hivyo
wahitaji wa fadhila za serikali katika Bunge na jamii kwa jumla wanakuwa
wengi mno. Pale ambapo sekta binafsi inakuwa kwa haraka, na wananchi
wanatumia ardhi kupata mitaji kwa kuuza na wanaonunua ardhi wanakuwa na
kinga ya kupata mikopo na siyo kwa mchakato wa biashara ambao benki hauna
kazi nayo, matazamio ya maisha yanainuka. Ni nadra katika hali hiyo
ushindani wa siasa uwe mkali kupita kiasi, na kushindwa kufikia kileleni iwe
uadui.

Ndiyo mandhari ambako JK amejikuta na makambi au makundi tofauti ndani ya
CCM ambayo ni hasi moja kwa jingine, kutokana na matazamio yasiyofikiwa ya
kundi moja au ya wanasiasa binafsi. Halafu mkusanyiko wa waliochukizwa na
kutopewa nafasi, ambao ni hasi kimaadili kwani wana machungu na siyo kuwa
wanatakiana heri miongoni mwao – kwani wao pia walikuwa wanashindana kwa
nafasi hizo hizo – wanakutana na kuunda ‘jumuia’ hasi ya chuki za ‘kuachwa.’
Ndiyo maana jumuia hiyo ya ‘kundi la 55’ la Richmond na EPA ikasambaratika
baada ya JK kuonyesha kukerwa na juhudi zao; si lingeinua CCJ?

Hivyo kuungwa mkono kwa mgombea wa Chadema ni mwendelezo wa hali hii, kuwa
ilikwama bungeni na sasa imepelekwa kwa wananchi, hasa kwa vile wengi
hawaelewi kuwa vita dhidi ya ufisadi ni usanii wa kiutawala kupinga
kupendelewa kundi dogo badala ya maslahi ya kifisadi ya kundi kubwa zaidi.

Ikiwa chuki hizi za kupandikiza ambazo zinatumia mwanya wa ugumu wa maisha –
ambao makundi haya ya watawala na wawakilishi wangefanya yawe magumu zaidi
kwa kandarasi kwa ‘kampuni yenye uwezo’ iifunge nchi kwa miaka 20 ya mkataba
– zitajijazia kura, inabidi hali irekebishwe. Uadui haushindi kura.

Lugha ya ki-‘demagogue’ ya ‘cha-demagogues’ bado haijaelewa kuwa demokrasia
inafanya kazi vyema pale wahusika wote wanatakiana heri, na kwa vile siyo
rahisi kujua wananchi wanataka nani aongoze, au ni sera zipi zinafaa (yaani
mbinu za kutawala uchumi, siyo ‘ndoto za ndaria’ za ahadi Bongo), wanapiga
kura. Ikiwa ‘cha-demagogues’ wanasema wakiingia madarakani wote
wanaotuhumiwa na chochote basi wakimbie nchi, itabidi wao wakimbie nchi kwa
maana hawatapewa nchi. Kimsingi utawala unawezekana na kuapishwa madarakani
pale vyombo vya ulinzi na usalama vikiwa na imani kuwa watawala wanafaa kwa
maslahi ya nchi; hawawezi kukaribishwa watu wenye kufurika hasira wapewe
mafaili waanze kazi…

*(mwisho)*