BARUA YA WAZI KWA MASHEIKH

Mkataeni kabisa Dk. Slaa, mwambieni JK aanze kurekebisha uchumi

Na Anil Kija

KUFANYIKA kwa kongamano la kutoa mwelekeo wa uchaguzi mkuu lililopangwa wiki
ya kuelekea uchaguzi mkuu wenyewe wiki inayofuata, linakumbusha usemi wa
Kiingereza kuwa ‘he who laughs last laughs best,’ hivyo itakuwa ni siku ya
kura ya turufu nani mshindi wa uchaguzi mkuu. Tayari maelekezo na ishara
zote kutoka katika makanisa zimeonyesha kuwa mgombea wao ni Dk. Wilibrod
Slaa wa Chadema, mwenye historia tata katika Kanisa Katoliki, na mwenye hali
ya utata kimaadili na kisiasa. Ni kiongozi wa chama chake ambaye alianza
kuapisha watu kuanzia mwaka 2007 baada ya Mwembeyanga.

Pia ziko dalili kuwa kutokana na uadui wa wazi wa viongozi hao wa Chadema
kuhusu serikali iliyopo madarakani, wanatoa nia za kuvuruga utawala wa
sheria endapo wataingia madarakani, hali ambayo inakuwa ni tishio kwa
usalama na matazamio ya watumishi katika ngazi tofauti. Matokeo yake ni kuwa
tahadhari zinaanza kutolewa kuhusu mgombea huyo na kama akishinda
itawezekana amani kubaki nchini – kwani uwezekano wa kuelewana katika chama
chake serikali yao iwe na sura gani ni tatizo la kwanza. Ukiongeza tatizo la
kutofaa kwake kupata baraka kwa utata wa unyumba wake, ni hali ngumu.

Kinachoonekana hapa ni kuwa kuna mtego wa kimaadili ambako mtu asiyefaa kwa
kazi muhimu kama ile kwa mustakabali wa nchi analetwa mbele za watu, wakuu
wa makuhani wa dini yake wanafunika kombe ‘mwanaharamu apite’ lisijadiliwe
lolote kuhusu hali hiyo. Sababu ya kufanya hivyo siyo kuchelea mfumo wa
demokrasia usiharibike, kwani watu wanachujwa kwa masuala mengi, na hata
maadili ni mojawapo ya watu kuchujwa au kujiuzulu, ila ni faida
zinazotazamiwa kupatikana kama anachukua uongozi. Ni kwa sababu hiyo ambako
utata wa alichokifanya katika Kanisa Katoliki na katika jamii unafichwa,
utugharimu.

Kutokana na kushindwa kwa wakuu wa makuhani wa dini yake kuonyesha
kinagaubaga kuwa mgombea huyo hana kielelezo chochote cha kuwa mtu mwema
kuanzia akiwa katika utawala wa juu wa Kanisa na hata katika uanajamii wake,
kwa ndoa yake ya kwanza na unyumba wake wa sasa, inabidi masheikh sasa
walifanyie kazi hilo. Ni katika kulinusuru taifa lisimfuate mtu ambaye
amewekwa kama mtego wa hali ya imani ya nchi hii, uwezo wa kupambanua jema
na baya, tofauti na ‘kufuata nyuki ule asali,’ wakati pia inawezekana
wakakugeuka, ikawa ndiyo mwisho wako. Na ‘asali’ ni tuhuma feki za ufisadi
kupatia kura.

Ingefaa ieleweke kuwa tatizo la msingi la kampeni ya Rais Jakaya Kikwete
kuendelea madarakani ni jinsi umma ulivyoaminishwa kuwa serikali ya Tanzania
imejaa wezi, au inaendeshwa kwa wizi. Licha ya kuwa hili ni suala pana
ambalo haliwezi kujadiliwa hapa kwa kina, ni rahisi tu kuona kuwa
kinachozungumzwa ni matumizi ya fedha za serikali katika uchaguzi mkuu
uliopita, kutokana na hali kuwa ni Watanzania wachache wanaomudu kulipia
wenyewe mawasiliano ya simu muda wote, katika hali ya kampeni. Na kama ni
suala la mtu kumfanyia mwingine kampeni, ni wazi gharama zinakuwa kwa yule
mhitaji, hivyo chama cha siasa husika kinakuwa na ulazima wa kutafuta fedha
za kuwawezesha wagombea wapite.

Kielelezo kimojawapo cha hali hiyo ni ‘makampuni 22 ya EPA’ ambayo kwa
haraka yanaendana na mikoa ya nchi, halafu katika suala la Richmond, kupata
mwekezaji wa ndani anayelipwa ndani ya miaka miwili ilikuwa ni jambo bora
zaidi kuliko kampuni ya nje inayoifunga Tanesco kwa miaka 20 kama IPTL.
Tatizo ni kuwa katika mchakato wa Richmond wakubwa wa Tanesco, wizara na
kamati za Bunge wanatia tu saini ya maamuzi, na hawana nafasi ya kupanga
jinsi ya kumega bilioni mbili au zaidi ili kugawana. Hali hiyo inawasha moto
mkali jinsi Waziri Mkuu alivyompendelea mtu fulani, kumbe suala liko
kwingine kabisa.

Kinachosemwa hapa ni kuwa ingefaa kongamano la maimamu likatae mkanda wa
‘vita vya ufisadi’ kuwa ni uasi ndani ya Bunge unaotokana na kutofikiwa
matazamio hasa katika kuunda serikali mpya mapema 2006 – kwani kundi la
mgombea wa CCM lilikuwa kubwa mno. Ni kwa mtaji huo danganyifu ambako wengi
kati ya wapiga kura wameelewa kuwa ‘ufisadi’ ndiyo unazuia maisha kuwa bora,
wakati ambacho kinaitwa ni ‘ufisadi’ ni bilioni 120 za EPA (bilioni 30
zikarudi), na maeneo mengine (kwa mfano kuunda mkakati wa kustaafisha
maofisa wa ngazi za juu jeshini, na siyo wastaafu wakilaani umaskini wao).
Ni wazi hakuna kielelezo cha umaskini wa fedha za aina hiyo za mwaka 2003
hadi 2005 wakati Bajeti ya nchi imefikia shilingi trilioni 11, hivyo hakuna
kielelezo chochote cha mkwamo wa uchumi cha ‘ufisadi.’

Tofauti na madai hayo, ni sera ya Kanisa iliyoainishwa mwaka 1993 katika
‘barua ya kichungaji’ ambayo ilitolewa Bagamoyo ikiungwa mkono kimya kimya
na hayati Mwalimu Julius Nyerere kumwonya Rais Ali Hassan Mwinyi ‘aache sera
yake ya kuuza nchi,’ ndipo lilipo tatizo. Wakuu wa makuhani wamekuwa na
mtindo wa kuwasililiza maswahiba wao wa kiimani, yaani wakuu wa idara
tofauti za serikali na mashirika ya umma, kwani Ukristo siyo jumuiko la
wafanyabiashara (kijamii) kama Uislamu. Matokeo yake ni kuwa ajenda muflisi
ya kubakiza kazi kubwa za kusimamia sekta tofauti, halafu kujaza nafasi za
bodi tawala za maeneo hayo, na mianya ya kugawana fedha kwa tafiti, ushauri,
n.k. unakwamisha mageuzi ya uchumi.

‘Nshomile’ wanaoshika nafasi za juu serikalini na mashirika ya umma, mamlaka
simamizi kadhaa katika sekta tofauti, wana ajenda moja ya msingi ambayo pia
ni kiainisho cha uzalendo wao, yaani kubakiza mashirika ya umma hata kama
nchi inatembea kwa magoti kutokana na udhaifu wa mashirika hayo. Leo hii
ingetakiwa treni zinapishana kuingia na kutoa vituoni, lakini hata safari
za wiki ni haba; kampuni ya Artumas ikaanza kuunganisha wananchi umeme kwa
sh. 45,000 halafu ‘wabunge wa Tanesco’ wakaanza kulia ‘Tanesco
inabinafsishwa mkoa kwa mkoa,’ hivyo mradi huo ukaondolewa au kuwekwa vyema
chini ya Tanesco. Kimsingi maslahi ya kushika vyeo katika mashirika
yanafukarisha nchi, kwa kuzuia mitaji mingi ya kuboresha miundombinu na
sekta tofauti, kupunguza gharama za biashara, na kuingiza kodi.

Kinachotakiwa katika hali ya sasa ni kutekelezwa kwa ibara ya 56 na 57 ya
Hotuba ya Bajeti ya mwaka huu ya Waziri wa Fedha Mh. Mustafa Mkulo, ambako
aliainisha umuhimu wa kurekebisha muundo wa mashirika ya umma ili
yasiendelee kuwa mzigo. Kinachotakiwa siyo kubadili kipengere hiki au kile
cha mfumo wa mashirika ya umma kwani utendaji wake unalindwa na Bunge (hivyo
Gavana wa Benki Kuu anathubutu kuchota sh. bilioni 1.2 eti ‘kukarabati
nyumba yake’ kwa mujibu wa wakaguzi wa serikali). Ni urekebishaji wa kina
kwa kuyaingiza mashirika sekta binafsi, siyo ubia bali kuuzwa mali zake
kikamilifu.

Pale ambapo serikali inatoa mashirika ya umma kwa wawekezaji wenye mitaji ya
kutosha, na kuingiza trilioni kadhaa za fedha, itaondoa mzigo wa madeni
ambao mwaka huu ni trilioni 2.1 ambazo zitalipiwa sh. trilioni tatu katika
Bajeti mwakani. Hali hii pia itawezesha shilingi kupata nguvu pale
inapozungukwa na wingi wa fedha za kigeni kutokana na ubinafsishaji, na hali
hiyo mpya itajaza fedha za nje katika maeneo fulani – hasa pale ardhi
inapoingia kuwa mali binafsi. Ni hapo itawezekana kasi ya kuwekeza katika
viwanda ikue, na pia mashamba, huduma nyingi zipate soko, vijana waanze
kuondoka barabarani.

Mabadiliko hayo yanawezekana ikiwa kongamano la maimamu litawezesha
kuondolewa kwa tishio la mgombea wa Kanisa kwa Rais Kikwete, na akiwa
anafahamu alipata msaada kupunguza au kuondoa kabisa hatari hiyo – au kuwa
na wabunge wengi mno wa chama cha wasema uongo na kupika hadithi za ufisadi
– atakuwa na nguvu zaidi kuelekea katika urekebishaji uchumi. Ndiyo ‘ari
mpya’ inayotakiwa na siyo ‘ari zaidi’ ya kubishana bila kikomo kuhusu kila
mkataba kutokana na kuheshimu sera za Kanisa za kuwaonea wageni;
inapoonekana kuwa wametendewa haki lazima wahusika wapelekwe mahakamani –
kwa kuzuia mapato ya serikali. Ni kiburi cha Misri ambako kitaigharimu nchi
hii kwa kuelekea kulipuka.

Cha msingi hapa ni kuwa inafaa kuwepo na ‘alliance’au mfungamano kati ya
maimamu na Rais Kikwete kuwa wamwondolee mzigo huu wa vuguvugu la upinzani
wa kutoa ahadi za Kusadikika na tuhuma feki za ufisadi, naye aahidi kupeleka
nchi kueleka kufanikisha biashara, na kuvunja mabaki ya Ujamaa wa Mwalimu
Nyerere na ‘nshomile’ wa Kanisa wanaofukarisha nchi. Upana halisi wa
mabadiliko hayo ni kurudia amri ya Malaika Gabrieli ya mwaka 1954 kuwa
‘Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja,’ na siyo kubaki tu katika
amri mbadala (ya Mungu wa Misri) kuwa ‘Binadamu wote ni sawa’ (ila kila
mmoja akae kwake, na wageni wasipate riziki katika nchi yetu, ardhi iwe ya
koo na makabila, wasinunue kama wanavyofanya kwingine). Kwa vile Waislamu
wanahiji na kukutana na wenzao wa dunia nzima, amri hii kwao siyo ngumu
kuielewa, lakini Ukristo mara nyingi unagubikwa na uzalendo, si imani
halisi.

Kukubali amri hiyo ni hatua ya kwanza inayoleta mabadiliko katika sehemu
nyingine nne, ya kwanza ni kurudia pendekezo la Gavana Edward Twining
kupeleka muswada LegCo mwaka 1958 kuwa ardhi iingie mali binafsi (kwani
Tanganyika huru ingesimamia suala hilo, hivyo wazawa wasingeonewa na mtu
yeyote). Eneo la pili ni kuondoa athari za Mapinduzi ya Zanzibar na
inapowezekana liwekwe fungu la fidia la Serikali ya Muungano, kwa walipoteza
maisha au kunyang’anywa mali, ili kuondoa laana ya tukio hilo inayodumu hadi
leo. La tatu ni athari za Azimio la Arusha katika imani ya mashirika kuficha
uzalendo unaofukarisha nchi, wakati suala la elimu au tiba bure ni la
Bajeti, si Ujamaa, na eneo la nne ni sheria ya kutwaa majumba ya kupangisha
ya mwaka 1971 ambayo iliwaonea wakazi wa asili ya Kihindi, na kuzuia uwezo
wao wa kuwekeza hapa, kwani hawakujisikia wako nyumbani baada ya hapo.
Inabidi kurekebisha.

Ndiyo mapungufu ya kiimani na kisera yanayofukarisha nchi, na yakirekebishwa
hayo au mwendo wa kufanya hivyo ukianza, matumaini yataongezeka na matunda
pia yataonekana. Napenda kutoa nukuu mbili kwani baraua hii ina chembe ya
unabii wa kuondoa mkasa unaonukia nchini, kuwa nabii Isaya anasema (1:18)
‘mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi, bali mkikataa mtaangamia kwa
upanga,’ yaani kukubali amri za kuwakubali wageni na kulinda mali zao – kama
sheria ya msingi ya Mungu (pamoja na ile ya kuheshimu ndoa ya mtu mwingine,
na mali binafsi kwa jumla). Pia nabii anasema katika kitabu cha pili cha
Mambo ya Nyakati 7:14 (historia ya ufalme wa Israeli) kuwa ‘watu wangu,
walioitwa kwa jina langu wakinililia, na kunitafuta uso – na kuziacha njia
zao mbaya – nitasikia kutoka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya
nchi yao.’ Nchi haiwezi kuokolewa katika kiburi kama Kanisa linavyotaka,
linalokataa amri zote za kuwezesha uchumi kukua (haki ya wageni kukaa
nchini, uwezo wao wa kununua mali binafsi na mali zote binafsi kuheshimiwa
kwa kuchukua mfumo huo uwe rasmi na sio ule wa makabila – ambayo ni jahiliya
katika undani wake, mapango ya matambiko, n.k.). Unapokataa kukubali wageni
(kama Wamisri kukataa kula chakula meza moja na ndugu wa Yusufu
alipojitambulisha kwao, kwani ni ‘chukizo’ kula na Waebrania) ardhi inakuwa
haina thamani, maendeleo yanategemea misaada kutoka nje kwani mapato ya
serikali yanatumika tu kulipa watumishi serikalini (asilimia 90 ya mapato ya
ndani). Msukumo huu inabidi utoke kwa maimamu kwani Kanisa halina uwezo wa
kufikiri hadi hapo; azma yake iko katika uzalendo, na umaskini unapozidi,
wanatafuta visingizio vya ‘ufisadi,’ na sasa wanapigana udi na uvumba
kuwaingiza madarakani watu ambao ukiwaangalia wana ufisadi pekee katika nia
zao – waendesha majumba ya kamari, wenye maduka London, wafilisi vikundi
uwekezaji – na siyo hilo jema wanalodai. Kwa maana hiyo Waislamu wamkatae
mgombea huyo wa Kanisa na kuvuka kizuizi hicho kwa Rais Kikwete, naye aanze
mikakati ya kutekeleza Ibara 56 na 57 ya Bajeti, ambayo takriban hata mbunge
mmoja hakuzungumzia suala hilo, au kuweka Bajeti rehani ili kukopa trilioni
2.1 – ambayo inaashiria hatari ya kulipuka uchumi wa nchi pale Bajeti
ikiwekwa rehani yote, hapo mwakani.

Ni wazi kuwa hatua zitakazochukuliwa na kongamano la maimamu zina uwezo
mkubwa siyo tu wa kutoa uelekeo katika uchaguzi mkuu bali muhimu zaidi,
kufanikisha mweleko chanya wa maendeleo, usiachiwe makarani na wanyapara wa
mashirika ya umma ambao wamelazimisha Bajeti Rehani kwani wafadhili
wanapunguza misaada, huku Kanisa limekataza mageuzi kwa msingi wa ‘nasaha za
Nyerere’ na ‘usawa wa binadamu’ ambao unadaiwa kutokana na Injili, wakati
Kristo anasema ‘ole wenu mafarisayo na waandishi kwa maana mnawazuia watu
kuingia mbinguni na nyie hamuingii,’ hivyo mashirika ya umma yanazuia
mabilioni ya mitaji kuingia nchini, na yenyewe hayana mitaji. Pia Kristo
anaeleza kuwa mbwa mwitu akitokea wakati kondoo wanakula porini, kama kondoo
ni mali yake, yule mchungaji ataishika silaha yake, na mbwa mwitu ataenda
zake. Lakini kama kondoo si mali yake, atakimbia na mbwa mwitu atawatawanya
kondoo (yaani waliwe waishe porini). Ni vivyo hivyo mashirika ya umma,
yanavuja ‘propoza’ kutoka meneja mkuu hadi mfagizi au mlinzi mlangoni, na
hayawezi katu kuwa msingi wa uchumi wenye tija, lakini yanalindwa na Kanisa
kwa misingi ya uzalendo, kuona choyo wageni wakiwa ndiyo mameneja wakuu,
watawala fedha, n.k.,hulka inayofukarisha nchi. Ni suala la imani kubadili
hilo.

Wa Ramatullahi, Wabarakatu

ANIL KIJA