Na Tiganya Vincent-MAELEZO-Dar es salaam:
Serikali imewaagiza wakaguzi wa ndani wa Sekretarieti za mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa hesabu za miradi yote ya maendeleo
katika maeneo yao ya kazi inakaguliwa ili kuhakikisha kuwa inatoa matokeo
mazuri yanayolingana na thamani ya fedha kwa matumizi yanaliyofanywa.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha Ramadhan Khijjah wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa wakaguzi wa
ndani wa Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mkutano wa siku tatu wa wakaguzi wa ndani wa Sekretarieti za mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa unalenga kuwaelimisha juu ya marekebisho ya
Sheria ya Fedha Sura 348 ya juni 2010 yaliyopelekea Wizara ya Fedha
kuanzisha Idara ya Mkaguzi wa Ndani wa Serikali(Internal Auditor General
Division) ambayo pia inajukumu kusimamia na kuboresha ukaguzi wa ndani
kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekrietarieti za Mikoa.
Alisema kuwa ni wajibu wa wakaguzi kuanzia serikali kuu hadi Serikali za
mitaa kuhakikisha kuwa miradi zaidi ya maendeleo inakaguliwa na taarifa
kuifikia Wizara ya Fedha mapema ili hatua muafaka ziweze kuchukuliwa kwa
lengo la kuboresha dosari zinazojitokeza ili miradi inayopelekwa katika
jamii inasaidia e kuleta maendeleo yaliyokusudiwa na wananchi.
“Ni wajibu wenu katika kuongeza uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa
matumizi ya rasilimali za umma , ili Serikali iweze kupata thamani ya fedha
zinazotumika na kuboresha huduma kwa jamii “ alisema Khijjah.
Aidha Katibu Mkuu huyo aliwaagiza kuwa wakaguzi hao wa ndani kujielimisha
zaidi kwa kusoma miongozo mbalimbali ya ukaguzi wa ndani na namna ya
kuweka kumbukumbu vizuri ili kufanya kazi ya ukaguzi katika viwango
vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.
Alisema kuwa hatua hiyo itawasaidia kuwa watendaji wazuri na wanaotoa
taarifa zinazoonyesha ukweli halisi wa matumuzi ya fedha na rasilimali za
wananchi kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Khijjah alisema kuwa Serikali ilianzisha Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa
Serikali kupitia marekebisho ya Sheria ya Fedha Sura 348 yaliyopitishwa na
Bunge Juni ,2010 kwa lengo ya kuimarisha utendaji na uwajibikaji katika
udhibiti na usimamizi wa matumizi ya rasilimali za umma na utawala bora.
Mkutano
MWISHO