Na Anil Kija

MJADALA umezuka kuhusu uwezekano wa kuapishwa kwa mgombea urais wa Chadema
Dk. Wilibrod Slaa endapo anashinda katika uchaguzi mkuu hivi karibuni,
wakati anaishi kinyumba na mwanamke mwenye ndoa halali. Tatizo lilianza pale
makuhani waandamizi wa makanisa tofauti (na hata imamu mwandamizi wa jiji la
Dar es Salaam) walipofika ofisini kwake, makao makuu ya Chadema, wakatoa rai
ya kusafisha – au kupuuzia – suala hilo. Walisema ni ‘mambo binafsi’ ambayo
hayahitaji kuinuliwa bango kuhusiana na uchaguzi mkuu, msimamo ambao
uliwashangaza baadhi ya ‘wanazuoni’ hata wa Kikristo.

Dhana tangulizi ambayo watetezi wa ‘ubinafsi’ wa suala la unyunba wa Dk.
Slaa wameonyesha ni kuwa ni tatizo la ufuska, na hilo si mojawapo ya makosa
au matatizo yanayohusiana na sheria ya uchaguzi, na wao kama wakuu wa
madhehebu hawana la kuongeza hapo. Kwa wanaoyafahamu maandiko ya Kikristo,
msimamo huo ni kielelezo cha wakuu wa makuhani kuacha maandiko na kufuata
ridhaa zao kwa nia ya kupata faida fulani endapo mhusika anafanikiwa katika
juhudi zake za kufika Ikulu. Ina maana wameacha pembeni kanuni ambazo
zinafundishwa kwa nguvu, zilizoainishwa katika Torati, iliyo ya wanadini
wote.

Hivyo hapakuwa na njia kwa suala hili kuishia tu mikononi mwa maaskofu
waliomtembelea Dk.Slaa ofisini kwake, kwani iligundulika kuwa inabidi
itolewe tafsiri pana na yenye uhalisia wa nani anafaa kufikishwa katika
madhahahu maalum ya kitaifa, aombewe utawala, hekima na amani kwa miaka
mitano ijayo. Ni kama kuuliza swali kama mtu aliye katika hali ya Dk. Slaa
katika unyumba wake anafaa kufikishwa mbele ya madhabahu hiyo maalum au la,
na jibu linakuwa ni hapana. Isitoshe, siyo swali la ‘stashahada’ ya
uanazuoni wa theolojia yaani uchambuzi wa maandiko; ni kipaimara – kuifahamu
Biblia. Kwa vile pale alipo hawezi kupewa sakramenti takatifu hadi hali
irekebishwe, hawezi kuapishwa; period.

Walichosema maaskofu kwamba kuwa na mke halali wa mtu ndani ya nyumba yako
ni ‘ufuska’ ni batili kwani hiyo ni dhulma, siyo ufuska. Mtu anapooa akawa
na mwanamke kihalali, hawezi tena kushindana na mtu mwingine kwa utii wa mke
wake, hasa kwa suala la kurudi nyumbani au kutorudi, hata kama – kutokana na
kutokuwepo sharia – mwanamke anaweza akafanya ukahaba huku au kule, akitaka.
Ni kejeli kwa mfano Josephine kuandikwa eti anawahimiza watu ‘wampigie kura
shemeji yao Dk. Slaa’ – kwa mahari aliyopokea nani? Anaweza kusimama
kuapishwa na hawara – anayezungumza lugha ya bar?

Hilo suala ni wazi kwa mtu anayejua Mungu alichokifanya kwa Farao kuhusu
Sarai mke wa Ibrahimu, halafu kwa Abimeleki kwa Sarai huyo huyo, na
kuchukizwa na kitendo cha Daudi ‘kumchakachua’ vitani Uria ili yeye amrithi
mkewe akijifanya amekuwa mjane. Tukio kubwa ni kuuawa kwa Yohana Mbatizaji
akimkemea Mfalme Herode kuishi kinyumba na shemeji yake, mke wa Filipo
nduguye, yaani akiitetea Torati. Hivyo inabidi Dk.Slaa apate ridhaa ya huyo
mke kuachwa kwa talaka, vinginevyo atakuwa hafai kuapishwa, na taifa
likipuuzia viwango hivyo na tahadhari hiyo, litakuwa limemchezea Mungu;
litashaa.

(mwisho)