Biashara ya Kahawa mbichi yafifisha soko la kilimo hai

Biashara ya Kahawa mbichi yafifisha soko la kilimo hai

Na Mariam Juma:

Emiliana Eligaisha (70), mjane aishie anayetegemea zao ka kahawa huko
Kituntu katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, amelalamikia wakulima
wanaouza kahawa mbichi kwa kuchanganya na kavu kuwa wanaua soko.
Akiishi katika kaya yenye ukubwa wa takribani ekari sita zilizosheheni miti
ya kahawa, maharage, mahindi na migomba kwa mtindo wa kilimo hai, mjane
huyo ambaye pia ni mshindi wa pili wa Shindano la Mama Shujaa wa chakula
2012 “Maisha plus” lililokuwa likirusha na kituo cha Tbc1 alisema soko la
mazao ya kilimo hai linatibuliwa na wakulima waroho.
Alisema kushamiri kwa uuzaji wa kahawa mbichi unaoendeshwa na wakulima
wengi wilayani hapo wenye kupenda utajiri pasipo kuzingatia matakwa ya soko
kunafanya soko la uhakika lililokuwepo.
“Kilimo hai ni kulima kwa kutumia mboji, kutumia dawa asili zitokanazo na
mimea na kuepuka kutumia kemikali za viwandani, mazao yatokanayo na
kilimohai yana soko la uhakika lakini pia bei yake ni kubwa ikilinganishwa
na bei ya mazao yasiyo zingatia kanuni za kilimo hai,” alisema staa huyo wa
chakula.
“Kwa mfumo huu wa kilimo hai tuliweza kupata soko la uhakika Ulaya kwa
kupitia shirika la Karagwe Development and Relief Services (KADERES) lakini
kutokana na wakulima kutokuwa waaminifu kwa kuingiza kahawa mbichi na chafu
sokoni, hivyo kujikuta soko hili likikumbwa na changamoto mbalimbali,”
alilalamika Shujaa huyo.
“Kahawa inapovunwa ikiwa Mbichi inapokaushwa hupoteza ubora kwa kuwa ni
grade ya mwisho ambayo hauwezi kuingiza katika soko la kimataifa, hivyo
kuwapatia hasara mawakala wa soko la kimataifa ambayo hujikuta wakipoteza
uhakika wa soko hilo,” alisisitiza.
Na kuongeza kuwa, “ Kahawa mbichi huwapatia wakulima pia hasara kwasababu
huuzwa kwa bei ndogo zaidi kutokana na uzito wake kuwa mdogo inapopimwa
kwenye mzani”.
Shujaa huyo ambaye amepata mafanikio makubwa baada ya ushindi huo kwa
kupatiwa pembejeo za kilimo kutoka shirika la Oxfam ambazo zimemuwezesha
kuweza kuzalisha kahawa yenye kiwango kizuri na kupata faida, ikiwemo pia
miche aina ya hasi ya parachichi.
Shujaa huyo ambaye anakiri kuwa mafanikio yake kuchangiwa kwa kiasi kikubwa
na shirika la KADERES na wataalam kutoka shirika la wafanyakazi wa
kujitolea kimataifa (VSO), kwamba amekuwa mtafiti katika kilimo hai na
kusaidia kuendesha mafunzo kwa wakulima wenzake vijijini.
Pamoja na kilimo hiki kukuza kipato cha familia yake na kumpatia umaarufu
wa kufika ulaya, shujaa huyu pia amekuwa akizalisha miche ya kahawa aina ya
Robusta na Arabika na kuwauzia wakulima wengine wilayani Karagwe na Kyerwa.
“Naomba wakulima wafute mawazo kwamba wakulima wadogo wadogo hawana faida
na mazao yao, ili kufanikiwa jitihada binafsi zinahitaji kuhakikisha
wanafanikiwa na kupata mafanikio kama mimi nilivyofanikiwa kwa kusomesha
watoto wangu tisa hadi chuo kikuu kutokana na kilimo hiki,” alisema mama
shujaa.
“Kilimo ni kama mtoto anahitaji malezi bora na matunzo, mimi nathamini sana
kilimo ndio maana hata ukiangalia shamba langu nalitunza na sasa nimepanda
mbegu mpya za parachichi, kahawa na migomba ili kuhakikisha elimu na
changamoto nilizo kutana nazo naviweka katika vitendo ili kuleta mabadiliko
kutoka kilimo cha mazoea na kuhamia kilimo chenye tija kwa kuzingatia
uhitaji wa soko,” aliongeza.
“Naomba nitoe wito kwa wanawake wajane na wale ambao si wajane kuwa
waachane na dhana ya kwamba wanaume ndio wana uwezo wa kupanga matumizi na
kutunza familia, kwani asilimia kubwa ya wanaume wamekuwa wakifaidi mapato
ya kahawa kuliko wanawake na watoto licha ya wao kutekeleza kazi hiyo kwa
kiwango kikubwa zaidi,” alitoa rai shujaa huyo.
Mnamo mwaka 2005 shujaa huyo aliweza kuwa mjumbe wa Halmashauri ya chama
cha ushirika cha kahawa cha Karagwe (KDCU) akiwa ni mwanamke wa kwanza
kuchaguliwa katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka sita, kabla ya
kujiunga uanachama wa kudumu katika kilimo hai kwa shirika la KADERES na
kuanzisha kikundi cha wanachama 26 wa kilimo hai.
“Natoa shukrani kwa shirika la KADERES na VSO kwa kuweza kushirikiana na
mimi kwa ukamilifu hadi sasa, ila kilimo hai bado kina changamoto nyingi
licha ya kuwa na soko kubwa ulaya ila nina imani elimu ikitolewa ipasavyo
tutafanikiwa katika kilimo hiki,” alisisistiza.
Emiliana Eligaisha ni mzaliwa wa Karagwe mkoani Kagera, aliwahi kufundisha
kwa miaka 36 kwa jumla ya shule tano tofauti kwa shule za msingi Kayungu na
Nyakagoyagoye iliyopo Bweranyange, Nyaishozi, Ihembe na Itembe zote za
wilayani Karagwe mkoani hapo.
Akizungumzia mafanikio ya ualimu alisema kuwa, anajivunia kuwezesha
wanafunzi kusoma na kuandika na kuona wamefanikiwa kielimu kwa ngazi za juu
zaidi.
“Kwenye ualimu najivunia kuona nikipita sehemu nasikia mtu ana niita
mwalimu karibu soda, lakini pia niliweza kupata makazi ya kudumu ya kuishi
kwa sababu pesa ya kilimo niliitumia kusomesha watoto wangu,” aliongeza.
Shirika la KADERES lililo anzishwa mwaka rasmi 1998 limeweza kuwekeza
kikamilifu katika kilimo hai na soko la Haki kwa kahawa; pia lilifanikiwa
kuanzisha kampuni ya Kaderes Peasant Development (KPD Plc) mwaka 2008
ambayo msimu uliopita iliweza kununua kahawa kwa bei ya shilingi 1500 kwa
kilo, na hivi sasa kampuni hiyo inajenga kiwanda cha kisasa cha kukoboa
kahawa kinachotarajiwa kukamilika mwakani.
Shirika hili ambalo limefanikiwa kuweza kuteka soko la ulaya kwa nchi za
Ujerumani, Ufaransa, Italia, uholanzi na Uingereza.
Akizungumza katibu mtendaji wa kampuni hiyo, Leonard Kachebonaho alisema
kuwa, kuptia mauzo ya kahawa wana uwezo wa kuwapatia wakulima bei nzuri kwa
kahawa nzuri.
“Tuna hitaji kahawa iliyokomaa, safi na inayozingatia kanuni za kilimo hai;
kahawa yetu hukaushwa kwenye jua, hukobolewa na kusafishwa kisha kupakiwa
katika mifuko ya kilogramu 60 na huwa katika madaraja mawili ya juu ambayo
ni standard na superior (karibu asilimia 85),” alisema Kachebonaho.
“Kahawa yetu inazalishwa katika viwango vya masoko ya haki na kilimo hai
kwa kuepuka matumizi ya kemikali zenye sumu na mbolea za viwandani na ndio
maana kuanzia Julai hadi sasa jumla ya tani 296,774 zimekusanywa ambazo
ndizo zilizo kidhi vigezo,” alisema katibu huyo.
Na kuongeza kuwa, “ili kuhakikisha tunapata kahawa ya kutosha kulingana na
uhitaji wa soko, tumeamua kuwapatia mafunzo na mbegu ili kulima kilimo
chenye tija kwa kuweza kuwapatia bei nzuri kutokana na ubora wa viwango wa
kahawa watakazo zalisha”.
Hivi karibuni, KPD Plc kwa kushirikiana na mtandao wa Trade Africa Network
Tanzania (TAN TANZANIA) na shirika la ushirikiano wa kimataifa la nchini
ujerumani (GIZ) waliweza kutoa mafunzo ya mnyororo wa thamani kwa nchi za
Tanzania, Rwanda na Burundi, ambapo kutoka Burundi waziri mstaafu
aliwakilisha katika ukumbi wa ELCT Kayanga wilayani Karagwe mkoani Kagera.
Kahawa ni moja ya zao kuu la biashara linalolimwa katika wilaya ya Karagwe
na Kyerwa ambao huzalisha asilimia 90 ya kahawa aina ya Robusta na asilimia
10 aina ya Arabika; kahawa hulimwa katika maeneo yaliyo kati ya mita 1500-
2500 usawa wa bahari.