Na Anna Atugonza:
Kuna msemo unaosema kufa kufaana. Msemo huu ambao unaangalia zaidi faida ya
upande mmoja kwa madhara ya upande mwingine, unaonekana kuchukua mkondo
katika kilimo cha mpunga mwaka huu.
Hali hiyo inatokana na kuporomoka kwa bei ya mchele, ambayo ni faida kubwa
kwa mlaji lakini ikiwa ni hasara kubwa kwa mkulima wa mpunga.
Wadau katika sekta hii wamesema kwamba pamoja na kuongezeka kwa zao la
mpunga, kilichoua bei ni kuingizwa kwa mchele kiasi cha tani 69.452 kutoka
nje ya nchi.
Kupungua kwa bei ya mchele ni furaha kubwa kwa walaji ambao walikuwa
wakiona bidhaa hiyo ikizidi kupanda katika soko. Lakini furaha hiyo imekuwa
karaha kwa upande wa wakulima wa mpunga ambao sasa wanalalamikia bei ndogo
na kukosekana kwa soko.
Bei ya mchele imeshuka kutoka shilingi 2,800 kwa kilo moja mwaka 2012
kufikia shilingi 1,000 kwa mwaka 2013.
Mathalani katika wilaya ya kilombero pekee takwimu zinaonesha kwamba
kumekuwepo na ongezeko la mavuno la asilimia 98 kutoka asilimia 85 za
mwaka jana na kufanya soko la mpunga wilayani hapo kuporomoka.
Hata hivyo kilimo cha wakulima hakitokani na kuporomoka kwa bei ya mpunga
bali kushindwa kupata thamani halisi ya kazi yao ukizingatia kwamba kilimo
chenyewe ni ghali.
Mmoja wa wakulima aliyejitambulisha kwa jina moja la Mdegera alisema kwamba
gharama za uzalishaji kwa ekari kuanzia maandalizi, kupanda hadi kuvuna na
kusafirisha ni zaidi sh 60,000 kwa gunia na anapolaizmika kuliuza gunia
hilohilo kwa shilingi 45,000 hadi 50,000 kunamuumiza.
Mkuu wa wilaya ya Kilombero Bw. Hassani Masala, akizungumzia tatizo hilo
amewataka wakulima kuhifadhi mazao hayo kwenye maghala ya yaliyopo maeneo
yao hadi bei itakapopanda ili waweze kuuza kwa bei itakayowanufaisha na
kupata mitaji ya kuwawezesha kulima msimu mwingine.
Bw.Masala alisema pamoja na kutengeneza mfumo wa hifadhi kusbiri bei,
aliwataka wakulima wilayani humo ,kubadilisha tamaduni za kulima zao moja
la mpunga,huku akiwahamasisha kujiunga na vyama vya ushirika.
Alisema kushuka kwa mchele kunakotokana na kuwapo kwa sera za soko huria
naona pia mchele ulioingizwa kwa ajili ya kusaidia kuweka sawa usalama wa
chakula na bei umevuruga bei ya mpunga.
Tathmini ya usalama wa chakula Septemba mwaka 2012 na Januari
2013,ilionesha kuwapo kwa maeneo yenye dhiki ya chakula.Jumla ya
Halmashauri za wilaya 47 katika mikoa 19 zilikuwa na uhaba wa chakula na
ndipo serikali ilipotoa kibali cha kuingizwa chakula cha ziada.
Mikoa ambayo ilikuwa na matatizo ya chakula ni Mwanza, Kagera, Arusha,
Manyara, Kilimanjaro, Morogoro, Lindi,Tanga,Shinyanga,Mtwara, Pwani
,Simiyu,Tabora,Iringa,Dodoma,Singida,mbeya na Rukwa.
Sehemu kubwa ya mikoa hiyo chakula chake ni mchele na kutokana na upungufu
uliokuwapo katika zao la mpunga na mahitaji ya mchele kuwa makubwa bei
ilipanda kutoka shilingi 1,500 kwa kilo moja mwezi Agosti mwaka 2012 hadi
wastani wa shilingi 2,800 kwa kilo mwezi Februari 2013 katiaka masoko ya
jumla.
Kufuatia na bei hiyo kuwa ya juu na kuwanyima fursa wananchi wa kipato cha
chini kupata , Desemba 2012 , serikali iliteua Makampuni tisa yaagize
tani 60,000 za mchele ili kupunguza makali ya bei kwa walaji, mbapo
serikali iliwataka wafanyabiashara hao kuuza shilingi 1,300 kilo moja ya
mchele kwa bei ya jumla, bei kwa wasambazaji kilo moja shilingi 1,450 na
bei ya rejareja isiyozidi1,700 kwa kilo.
Baada ya ruksa hiyo kufikia Machi 30,2013 jumla ya tani 34,689.54 za mchele
zilikuwa zimeingizwa nchini.
Bw.Yusuphu Makuli ,ofisa masoko kutoka asasi isiyo ya kiserikali
inayofanya shughulizake mjini na vijiji (RUDI)kwa lengo la kuwapatia
wakulima elimu ya uzalishaji kilimo bora na cha biashara pamoja na
kuwatafutia masoko wakulima yeye alisema wakulima wamekata tamaa kutokana
na sera ya masoko iliyopo kutowalinda.
Alishauri kuwa serikali ikazane na kutengeneza sera ambazo zitamwangalia
mkulima ili asikate tama na kutelekeza kilimo chake hali ambayo hufanya
mustakabali wa chakula kutokuwa mzuri.
Alisema kama sera zikiwa nzuri na zikafuatiliwa mnunuzi wa chakula
atanufaika na mkulima pia na hivyo kilimo kuwa shughuli endelevu.
Akizungumza kwa niaba ya na wafanyabiashara Juma Adalah,anasema sheria
kandamizi za masoko zisizowajari wakulima wa mazao ya kibiashara, ni
kikwazo mojawapo katika uzalishaji wa zao la mpunga kutokuwepo masoko ya
uhakika kwa wakati ,serikali kuagiza vyakula kutoka nje ,kuwazuia kuuza
mazao yao nje ya nchi ambapo kuna masoko ya huhakika inawanyima haki
wakulima wa kuzalisha kilimo cha kibiashara.
MWISHO