*Na Tulizo Kilaga*
*Waziri wa Maliasili na Utalii,* Mhe. Balozi Khamisi Kagasheki
amewataka wahariri
wa vyombo vya habari nchini kupanga utaratibu wa kukutana na viongozi wa
wizara kwa shabaha ya kuuliza ama kupata uhakika wa mambo yaliyojitokea
ndani ya wizara.
Mhe. Kagasheki aliyasema hayo katika mkutano na wahariri wa Jukwaa la
Wahariri uliofanyika jijini Dar es Salaam leo, kuhusu viupaumbele na
mwelekeo wa mpango wa bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Mhe. Waziri anabainisha kwamba, kuna mambo mengi yanayoripotiwa kuhusu
Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo hayako sawa. Hivyo Wizara imeoana kuna
haja ya kuweka utaratibu ambao utawalazimu viongozi wakuu kukutana na
wahariri mara kwa mara kuwapa nafasi ya kuuliza mambo mbalimbali wanayotaka
kuihabarisha jamii.
“Kuna nchi nyingine kuna uataratibu ambao hauepukiki ambapo mawaziri ama
viongozi wa juu inabidi wakutane na wahariri pengine mara moja kwa wiki ama
kwa mwezi kwa shabaha ya kuuliza na kupata uhakika wa mambo ambayo
yametokea kwa wiki ama kwa mwezi huo na kuuhabarisha ulimwengu,
“Mimi ni utaratibu ambao naupenda kwa maana ya kusema kwamba tunawekana
wazi kwani kuna mambo mengi ambayo yanaripotiwa ambayo hayana uhalisia wa
ukweli ndani yake, hii ni Wizara muhimu inayogusa maisha ya kila mtanzania.
Hivyo kuna umuhimu wa Jukwaa la Wahariri kuzungumza na kuafikiana juu ya
mara ngapi Wizara ikutane na wahariri ili tuweze kuwapa tarifa na kuwapa
nafasi ya kuuliza mambo mbalimbali,” Alisema Mhe. Kagasheki.
Alisema kuwa, Wizara imefikia uamuzi huo si kwa sababu ina mambo ya kuficha
ama inahitaji upendeleo maalumu katika uripotiwaji wa habari zake, bali
inataka kutumia fursa hiyo kuweza kujua mambo mbalimbali ambayo yapo ili
kuweza kuyafanyia kazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa* **Jukwaa la Wahariri** *Tanzania (TEF),
Absalom Kibanda aliishukuru Wizara kwa kutoa nafasi hiyo na kuwataka
wahariri kuona haja ya kuripoti habari zinazolenga kujenga na si kuibomoa
tu Wizara ili kuisaidia Wizara na Watanzania.
Akichangia hoja hiyo, Katibu wa TEF, Neville *Meena*, aliipongeza wizara
kwa kuona umuhimu wa kupanua wigo wa mawasilinao na wahariri wa habari na
kutaka kuangalia uwezekano wa kufanya mikutano ya namna hiyo nje ya jiji la
Dar es Salam ili kuweza kutoa nafasi kwa wahariri kushiriki kikamilifu na
kufanya kazi kwa pamoja.
Meena aliongeza kuwa, Wizara ina haja ya kubadiri utaratibu wa kutoa habari
kwa kutumi makaratasi na kuona umuhimu wa kutoa taarifa kwa wakati ili
wanahabari waweze kutoa taarifa sahihi kwa wananchi.
Akizungumzia suala la utoaji wa habari Wizarani, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali wa Wizara, Yustina Mallya alisema Wizara imepanua
wigo wa utoaji wa habari kwa kuanzisha ukurasa wake facebook na twitter
ambao kila mtu anaweza kuuliza chochote na kupata majibu ndani ya wakati.
Mallya alitoa wito kwa wananchi kutumia ukurasa wa facebook, Ministry of
Natural Resources and Tourism – Tanzania na twitter, @mpingo1 pindi
wanapotaka kufahamu juu ya jambo lolote ama kutoa maoni yanayoihusu Wizara
ya Maliasili na Utalii.