Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Khamis Suedi Kagasheki
amewataka askari wa Wanyamapori popote waliko nchini kufanya kazi kwa
bidii na bila uoga wakati wanapotekeleza kazi zao za kila siku maana
mafanikio ya uhifadhi hapa nchini yako mikononi mwao.
Aliwaasa watumishi wote wa Idara ya Wanyamapori kuzingatia ushirikiano
(team work) ili kufanikisha uhifadhi kwa manufaa ya kizazi hiki na
vizazi vijavyo. Alisema ushirikiano huo unawahusu watumishi wote wa
Wanyamapori popote waliko nchini, yaani wale walioko chini ya Wizara
ya Maliasili na Utalii, TANAPA, Ngorongoro na Serikli za Mitaa.
Mheshimiwa Kagasheki aliyasema hayo jana katika kikao alichokiitisha
cha viongozi wa Idara ya Wanyamapori kutoka Makao Makuu ya Wizara
pamoja na mameneja wa mapori yote ya akiba kilichofanyika Matambwe,
kituo kilichoko katika Pori la Akiba la Selous. Alisema aliitisha
kikao hicho ili kupata maoni kutoka kwa washiriki hao kuhusu namna ya
kuboresha uhifadhi.
Kikao hicho cha siku mbili kilihudhuriwa pia na Kaimu Mkurugenzi wa
Idara ya Wanyamapori Bw. Paul Sarakikya, Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za
Taifa (TANAPA) Bw. Alan Kijazi na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya
Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) Dakt. Mduma. Wengine waliohudhuria ni
Makamanda wa Kanda 8 wa Kikosi Dhidi Ujangili.
Washiriki wa kikao hicho walimshukuru Waziri kwa kutambua kazi yao na
kuwatia moyo na wakaahidi kuwa wataendeleza mapambano wanayoendelea
nayo sasa kwa bidii zaidi hususan ya kutokomeza ujangili.
Walimwambia Waziri kuwa ushindi wa vita dhidi ya ujangili utafikiwa
maana wameshabadili mbinu za mapambano baada ya kufanya utafiti na
kugundua kuwa majangili nao wanatumia mbinu na silaha za kisasa.
Waziri Kagasheki aliwaambia wahifadhi hao kuwa Wizara inao mkakati wa
kuongeza fedha, raslimaliwatu na vitendea kazi kwa mapori yote nchini.
Vitendea kazi hivyo ni kama vile magari silaha, na vifaa vya
mawasiliano.
Alisema kuwa mafunzo kwa askari wa wanyamapori walioajiriwa hivi
karibuni yanayoendelea Matambwe hivi sasa ni sehemu ya mkakati huo.
Akiwa huko Waziri alipata fursa ya kukagua askari hao wapya wakiwa
mafunzoni.
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII