Na Robert Mndeme
Mwanasayansi mtafiti:Tafiti kuhusu uhusiano wa hisia za mwanadamu kwa
afya na ustawi wa jamii;
Kwa ushirikiano, faundation of human understanding usa na alternative
medicine collage of Canada.
Mnamo tarehe 23 August 1973 katika mji mkuu wa Sweden, Stockholm
lilitokea tukio lililoishangaza dunia nzima. Majambazi yalivamia benki
kwa lengo la kufanya wizi wa kutumia silaha na kushikilia mateka
wafanyakazi wa benki ya mjini hapo. Baada ya jitihada kadhaa polisi
walifanikiwa kuwazidi maarifa majambazi tayari kwa kuwaokoa mateka
ambao sasa walikuwa wanashikiliwa karibu siku ya sita.
Kwa mshangao wa dunia nzima, wafanyakazi-mateka hao kama watu
waliokuwa usingizini wakiota, badala ya kuukubali ukombozi ule wa
polisi walionyesha dalili zote za kuupinga na kuwakumbatia majambazi.
Pamoja na udhalilishaji, mateso makali na ya hatari waliyokuwa
wameshafanyiwa, ilitokea wakashindwa kabisa kuwachukulia majabazi
katika ukweli wao na badala yake kuanza kuonyesha dalili za kuwatetea
na baadaye kuwahifadhi na kuwatengenezea mazingira ya kutokuadhibiwa
wakitoa visingizio kama walitupa fursa nzuri ya kula, kulala,
hawakutuua nk.
Mbele ya mateka wale polisi na misaada mbalimbali ya serikali katika
kuwakomboa ikaonekana kama ndio tatizo na wala sio majambazi na
ukatili wao. Tukio hilo la kustaajabisha na kushangaza likatokea kuwa
ni gumzo kubwa na hatimaye kupewa jina la Stockholm Syndrome.
Ikimaanisha maradhi ya fikra. Dalili zake zikiwa kujitoa kutawaliwa na
kutetea kile kinacho kudhalilisha kupitia uzalishaji wa hisia hasi.
Maradhi yaliyoshuhudiwa wazi hadharani huko Stockholm, Sweden.
Tafiti mbalimbali na ufuatiliaji vilifuatia na kudhibitisha kuwa ni
kweli kwa kile kilichotokea. Katika misingi ya kanuni ya ‘emotional
intelligence’ yaani werevu wa hisia; Ni kweli kuwa mwanadamu anapo
kandamizwa, kupigwa mshindo au msongo na kuzalisha hisia hasi, bila ya
matarajio kabisa na kwa viwango tofauti; kile kilichotumika
kumshinikiza na kumzalishia hisia hizo kwa namna fulani, kinabadilika
na kuwa kimbilio na faraja. Hata kama kitakuwa ni Jambazi wa benki,
Mtawala wa kikoloni, Ugonjwa sugu, Matatizo ya kiuchumi, Mateso
mbalimbali ya kimahusiano, kiimani, kiusalama au hatari na mateso
mengine yeyote.
Katika somo la ‘implanted identity’, kwenye kitabu how to conquer
negative emotions, Roy masters anaandika hivi; “Wakati wowote
unapochochewa na kusisimka kwa hisia hasi, mbegu ya kisababishi cha
msisimko huo inajipandikiza kwenye ufahamu ndani yako. Kinachofuatia
baada ya hapo ni maajabu matupu. Badala ya kutishwa na kukipinga
kisababishi hicho unajikuta ukivutiwa, kusisimuliwa, kukihitaji na
hata kukitetea.” Anaendelea! “Unaweza kujikuta kwenye mazingira ya
kupenda na kuvutiwa na hali hatarishi za kudhalilisha, zisizo za kiutu
wala za kimaadili bila wewe kuona kasoro yoyote katika mahusiano hayo
mapya ya utumwa wa fikra.”
Tukio la Sweden ni mfano mmoja tu kati ya mingi; inayo dhihirisha na
kufafanua kiuwazi uhalisi wa kanuni ya utumwa wa fikra ‘hypnotised
state of mind’ unavyoweza kutokea na kuathiri jamii. Kwa namna fulani
kupitia hisia hasi za mateka hao wa benki, iliwezekana kuzipindua,
kuzipumbazisha fikra zao na kuwafanya wawe watumwa watetezi wa
majambazi ambao waliwatesa na kuwadhalilisha. Ni utumwa kwa kuwa
muathirika bila ridhaa yake ila kwa kufanywa tu azalishe hisia hasi
imewezekana fikra zake kutekwa na kupandikizwa ujumbe wa kutawaliwa
kwa faida ya majambazi bila yeye kujitambua.
Hebu tulia na utafakari kwa makini; Idadi kubwa ya jamii iwe imetekwa,
kuteswa na kudhalilishwa na kikundi kidogo tu cha majambazi ambao sio
kama wale wa benki ya Sweden bali ni “majambazi wa kijamii” kama
walivyokuwa “watawala wa kikoloni” au walivyo “mafisadi na walarushwa
wakatili” au lilivyo “janga la ugonjwa wa ukimwi” nini kingetokea kwa
uhuru wa fikra wa jamii hiyo iliyoteswa na kudhulumiwa? Ukweli ni kuwa
kikundi hicho kidogo na janga hilo vitakuwa na uwezo wa kuwatawala
wanajamii hao mateka kwa mtindo uleule wa majambazi wa benki ya
Sweden. Tunauliza pamoja na kuwa na Uhuru wa miaka 45, Watanzania
wangapi wako huru kifikra dhidi ya mafisadi na walarushwa waliopo sasa
au wakoloni waliotutawala zamani? Au watu wangapi wanauhitaji,
kuulilia, kuudumisha na kuutetea ugonjwa wa ukimwi bila ya wao kuona
waziwazi kuwa wanaongozwa na fikra za kitumwa dhidi ya ugonjwa
wenyewe?
Katika misingi ya sayansi ya hisia hasi na dhana nzima ya E.I yaani
werevu wa hisia, maradhi ya utumwa wa fikra hayachukuliwi kama swala
la juu juu na la kisaikolojia tu. Ni kanuni inayokwenda kwa upana
mkubwa na kupenya ndani kabisa kwenye swala zima la afya, ustawi wa
jamii na dhana ya kutawaliwa kwa namna yeyote ile. Sayansi ya hisia
hasi na dhana ya werevu wa hisia ni kanuni zinazodhihirisha kuwepo kwa
maradhi ya utumwa wa fikra na kuwa hayana mipaka katika kuathiri jamii
kwa misingi ya viwango vya kisomo, dini, itikadi mbalimbali na
matabaka mengine ya kijamii. Yeyote anaweza kuwa muathirika.
Hebu pima kwa makini; Maradhi haya yanapoathiri kiasi kikubwa cha
wataalam wa nyanja muhimu za kijamii na viongozi katika ngazi
mbalimbali. Wakati wote, kwa mshangao na maajabu yasiyotegemewa
makundi hayo yawe maadui wa Ukweli. Yawe yanasimamia na kutetea upande
wa adui katika maendeleo ya jamii, yatetee na kutawaliwa na upande wa
adui katika utu na yatetee hali zilizo adui wa misingi ya kibinadamu.
Fikra za wataalam na viogozi zilizogeuka na ‘bila ridhaa yao’ ziwatume
kumlinda adui wa jamii kwa kutumia nyadhifa na taaluma zao. Jaribu
kuona ambavyo watakuwa wanaona kuwa wanapunguza matatizo ya kijamii
huku wakiwa ndio kabisa wanayawezesha kukua na kuota mizizi. Kwa hiyo
viongozi na wataalam wetu watakuwa wametusaliti, wametekwa utumwani;
Wanakwaza maendeleo na ustawi wa Taifa.
Jaribu kuona akilini; Usugu wa maradhi haya ya utumwa wa fikra utakapo
ikumba jamii yetu. ‘Majambazi wa kijamii’ kama umasikini, magonjwa,
ujinga, rushwa, dhuluma, ufisadi nk yatakavyokomaa na kushamiri huku
yakitolewa ushahidi wa fikra za kitumwa ‘hypnotic justification’ kuwa
yanapungua na kutoweka. Hakuna shaka jamii itakuwa kwenye janga la
athari za utumwa wa fikra. Waathirika watahitaji tiba na ukombozi wa
kuwarudisha kwenye afya ya fikra huru. Tuseme hivi; Taifa la Tanzania
linahitaji ukombozi wa kulifikisha kwenye Uhuru wa fikra timamu sasa
kuliko wakati mwingine.
Kwenye kitabu, Maadili ya Taifa na Hatma ya Tanzania, somo la ‘Mtizamo
wa Mwalimu Nyerere kuhusu ukombozi. Ibrahim Mohamed Kaduma Anaandika;
‘Wakati wa uhai wake, hayati Baba wa Taifa Mwalimu JK Nyerere alitamka
kwamba…Ukombozi hautakamilika mpaka kupitia hatua kuu tatu: Uhuru wa
bendera, Uhuru wa fikra na Uhuru wa kiuchumi.’
Kaduma anaendelea kuchanganua mtizamo wa Baba wa Taifa kwenye
kipengele cha Uhuru wa fikra katika kufikia ukombozi kamili. “Uhuru wa
fikra ni hatua ngumu na nyeti. Inahusiana na kumbadilisha mwananchi
kutoka mawazo ya ukoloni yaliyomgandamiza akawa hajiamini na kuvaa
utii wa woga wa amri za wakoloni hata kama zilikuwa zinamdhalilisha
utu wake. Hatua hii ikifanikiwa mwananchi atakuwa…. amevikwa Utu
mpya wa uhuru wa kweli na kujiamini. Kwani mtu aliye huru kweli kweli
hutetea Utu wake na haki zake. Huyu ndiye mtu mpya ambaye
anahitajika”.
Tafiti mbalimbali zimebainisha kuwa kwenye maradhi ya utumwa wa fikra
muathirika ‘hypnotised zombie’ kwanza anakuwa adui mkubwa wa ukweli wa
aina yeyote ile. Pili huwa hatetei haki za utu wala ubinadamu
anazikana, kuzipinga na kuzisaliti hali hizo waziwazi hadharani; hii
inawiana na nukuu “Mtu aliye huru kweli kweli hutetea utu wake na haki
za maadili ya utu wake. Huyu ndiye mtu mpya ambaye anahitajika”.
Tunaenzi na kuheshimu mchango wa Baba wa Taifa kuelimisha kuhusu jambo
hili la msingi kwenye jamii yetu. Hakufanikiwa kuishi kulishuhudia
likitimia, lakini kiu ya utimilifu wake ni kubwa sasa kuliko
ilivyowahi kuwa wakati mwingine.
Katika sayansi ya hisia hasi ni wazi kuwa dawa ya ‘utumwa wa fikra
katika maisha’ yaani ‘hypnosis of life’ ni kutumia njia za kitaalam,
kujenga utambuzi kama ambavyo imeshaelezwa kwenye makala
zilizotangulia. Hatimaye utambuzi huo umomonyoe nguvu hasi za chuki,
woga, mashaka, ubinafsi na hisia hasi nyingine ambazo ndizo pekee
zenye uwezo wa kupindua fikra huru kuzifanya fikra hasi na hatimaye
fikra za kitumwa. Mmomonyoko wa hisia hasi unapokamilika unatupa hali
inayoitwa ‘dehypnotic state of life’ au Upendo kwa jina la kawaida.
Ikiwa na maana kuwa Upendo ni nguvu ya kijamii iliyoishinda nguvu ya
chuki na hisia hasi zote. Fuata ufafanuzi zaidi www.duniahai.com
Kwa bahati nzuri sana, michakato na chambuzi mbalimbali zimedhibitisha
kuwa ushindi huo wa Upendo dhidi ya chuki na hisia hasi zote ndio
msingi wa ujumbe kwenye adhma ya kuwashwa kwa mwenge wa uhuru na
kuuweka kilimanjaro siku ya uhuru wa Taifa la Tanzania. Au kwa lugha
rahisi; Utanzania halisi ni Utambuzi wa nguvu ya Uhuru na Upendo
isiyoruhusu hisia hasi na utumwa wa fikra. Ikimaanisha kushindwa kwa
matendo ya kitumwa na kumpata Mtanzania huru kwenye nyanja zote. Kama
tafsiri hii imeangukia kuwa ni bahati tu au kama kweli waasisi wa
Taifa hili walidhamiria kuificha siri hii kubwa kwenye tendo la
kuwashwa kwa mwenge wa uhuru hatujui! Lakini tunawaenzi na kuwaheshimu
kwa alama na ishara hizo, zitakazo dumu na kuhitaji ufafanuzi wa kina
kwa faida ya vizazi vingi vijavyo.
Mtanzania kamili ni mwanadamu aliyehuru kweli. Anadhibitisha kuwa
amefikia kiwango cha juu kabisa cha utu na ukombozi wa kibinadamu
ndani ya jamii yake. Mtetea Utu wake, mtetea haki zake za Ubinadamu na
mtetea Taifa lake. Anafanya utetezi huo kwa kujiamini na kwa
ukamilifu wote bila kutumia nguvu ya HISIA HASI kwani yuko huru kiasi
cha kutosha kutambua kuwa hisia hasi ni nguvu geuzishi na pumbazishi
kwa fikra huru na kumpelekea kujikuta akitumikia ‘majambazi wa
kijamiii’ kama ilivyotokea kwa mateka wa Sweden. Mtanzania wa dhati
mwenye kulipenda na kuliheshimu Taifa lake hajapumbaa kifikra na
hataona ugumu kuamini matamshi ya aya ifuatayo ikiwa endelezo la nukuu
ya maelezo ya Ibrahim Kaduma katika kuonyesha mtizamo wa Mwalimu
Nyerere kuhusu ukombozi wa kiuchumi kwa jamii ya Tanzania.
“Umasikini tulionao, sio mapenzi ya Mwenyezi Mungu kama wakoloni na
mabeberu wanvyotaka tuamini. Mungu ametuumba kuwa sawa sawa kabisa na
binadamu wengine na ametupa rasilimali nyingi ambazo kama
zingelitumika kwa faida yetu, zinaweza zikatuinua tukawa matajiri
kuliko hao wanaotunyanyasa sasa. Tunadiriki kusema hivyo kwa sababu ni
kweli isiyopingika kwamba elimu ya kuchimba madini ya aina yoyote
inaweza kutafutwa popote duniani. Lakini dhahabu iliyoko Kahama,
Geita, Tarime na kadhalika haiwezi kupatikana popote pengine isipokuwa
Kahama, Geita, Tarime na kadhalika. Kwahiyo tunapowaachia watu wengine
waichimbe dhahabu hiyo bila kuchangia vyakutosha katika maendeleo ya
nchi hii ni ujinga wetu wenyewe kwa sababu Mungu aliiweka dhahabu
hiyo hapa ili watanzania tuweze kujitajirisha nayo na kutokomeza
umasikini wetu…Na kushindwa kuweka uchumi mikononi mwa wananchi
wageni wanaotawala rasilimali zetu watajilipa kwanza wao kile
wanachodhani ni stahili yao na kuwapa watanzania makombo
tu…mishahara ya kipagazi tu. Hiyo ndiyo hali iliyopo hivi sasa
katika nchi yetu”
Tunazidi kuona; Muathirika wa utumwa wa fikra aliye taabani chumba cha
wagonjwa waliozidiwa, hatua ya kwanza na ya msingi kwa maendeleo yake
kamwe haiwezi kuwa kumjaza mapesa au hazina kubwa ya dhahabu, almasi,
tanzanite au rasilimali nyingine yeyote ya thamani zaidi ya tiba ya
fikra zake kwanza. Tafiti zinaonyesha kuwa ni hakika, kwa fikra za
muathirika na kwa mikono yake mwenyewe atautwaa utajiri wake na
kuwakabidhi maadui wake wa kijamii na kwa mshangao mkubwa hata zaidi
ya ule wa Stockholm Sweden atayaita hayo kuwa ndio maendeleo ya jamii
yake. Hili ni wazi karibu kwa mataifa yote ya Afrika. Mwalimu Nyerere
yuko sahihi: Uhuru wa kiuchumi lazima utanguliwe na uhuru wa fikra, ni
hatua ngumu na nyeti lakini pia ni kweli kuwa haikwepeki.
Vuguvugu la kuukamilisha ukombozi wa fikra kwa Taifa la Tanzania yaani
“Dehypnotic state of Tanzania” linatokota kwa nguvu sasa kuliko wakati
mwingine, nalo halizuiliki. Mambo ya kutiliwa maanani; Elimu sahihi
itolewe. Pili; Udhibiti wa hisia hasi kwa njia za kitaalam, hasa
kujenga nguvu ya utambuzi dhidi ya hisia zenyewe ufanyike. Mwisho
msisitizo kwenye nguvu sahihi ya kijamii kama silaha na nyenzo ya
mapambano. Itumike nguvu inayoutafsiri Utanzania, Uhuru na Utaifa
wetu. Utanzania ni utu; Na sio nguvu hasi ya kijamii ya chuki. Utu na
Ubinadamu havikujengwa kwa nguvu ya hisia hasi. Hivyo silaha, nyenzo
na mbinu za ukombozi wa Tanzania haiwezi kuwa nguvu hasi ya chuki kati
ya makundi ya kijamii yanayo pambana. Nani hakielewi kiasilishi cha
utumwa wa fikra? Nani haoni kitakachotokea kama nguvu ya hisia hasi
itatumika? Hakika ushindi utakwenda kwa maadui wa ustawi wa Taifa.
Yeyote anayeshiriki katika mapambano ya ukombozi wa fikra na uchumi
kwa Taifa hili, ‘apambane kwa dhati kabisa’ lakini kwanza ajikague
vema kiwango cha Utanzania wake na ajikite kikamilifu kwenye nguvu ya
nuru ya maagano yetu ya Uhuru wa Upendo kwa jamii, Matumaini kwa jamii
na Kuheshimiana kati ya wanajamii wote. Ajifunze kwa undani siri na
maadili ndani ya alama za Taifa na aziheshimu kikamilifu. Kwani Taifa
la Tanzania si mali ya kundi lolote katika hayo yatakayokuwa
yanapambana ila, ni Taifa lililo asisiwa kwa Uhuru na Umoja wa
Watanzania wote.
Tofauti katika makundi yanayoshiriki mapambano yaishie kulifikisha
Taifa kuwa imara zaidi, lililo kamilifu kifikra na kiuchumi ndani ya
nguvu ya upendo isiyotikiswa na adui yeyote ndani au nje yake. Na
hatimaye Taifa lisijekujikuta na doa lolote la nguvu hasi na libakie
Nuru inayong’aa na kuheshimika duniani kote. Huko ndiko kumuenzi na
kumkumbuka Baba wa Taifa katika ujenzi wa ukombozi na utambuzi wa
uhuru wa fikra ndani ya Taifa la Tanzania. Eee, Mungu Uibariki Afrika.
Eee, Mwenyezi Mungu uibariki Tanzania.