Tanzania yazindua Kampeni ya kutangaza Utalii nchini Marekani

Na Pascal Shelutete, TANAPA:
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Sued Kagasheki ameshiriki
katika kampeni maalum ya kutangaza vivutio vya utalii nchini katika
mji wa Seattle nchini Marekani na kuelezea matarajio yake ya
kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini katika kipindi kifupi kijacho.
Kampeni hiyo ilizinduliwa jana katika mji wa Seattle nchini Marekani
na kushuhudiwa na uwepo wa matangazo yanayotangaza vivutio vya utalii
nchini katika mechi ya Mabingwa wa Ulaya, Chelsea FC na wenyeji.
Balozi Kahasheki alieleza kuwa Tanzania imekuwa ikitumia mpira wa
miguu kwa ajili ya kutangaza vivutio vyake katika maeneo mbalimbali
laikini safari hii waligeukia soko la mji wa Seattle ambao unao
wapenzi wengi wa soka na ambao kufuatia matangazo haya ya utalii
wanaweza kuvutiwa na kutembelea vivutio vya utalii nchini.
Waziri Kagasheki amesema kuwa inatarajiwa matangazo ya utalii
yaliyozinduliwa yatawafikia watazamaji wapatao milioni mia nane kwa
mwaka kupitia vituo mbalimbali vya televisheni vinavyorusha matangazo
hayo pamoja na wale wanaofika uwanjani kwa ajili ya kuangalia mechi
mbalimbali katika uwanja wa Seattle Sounders.
Mji wa Seattle ni soko muhimu magharibi mwa Marekani lenye wakazi
wenye kipato kizuri na wanaotembelea maeneo mbalimbali duniani kwa
ajili ya shughuli za utalii.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Marekani Bi. Mwanaidi Maajar
naye alieleza kufurahishwa kwake na kampeni hiyo ya utalii ambayo
alisema anaamini kuwa imekuja kwa wakati muafaka kwa kuwa mahitaji ya
Wamarekani kutembelea vivutio vya utalii nchini yamekuwa yakiongezeka
kila mwaka na kwamba kampeni iliyozinduliwa itasaidia kuongeza idadi
ya wageni nchini na kufikia lengo la wageni milioni moja kwa mwaka
kutoka laki nane waliopo hivi sasa.
Aidha, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii nchini Dk. Aloyce
Nzuki ambaye Bodi yake inahusika na utangazaji wa vivutio vya utalii
nchini alieleza kuwa Kampeni ya Utalii iliyozinduliwa ni mojawapo ya
mikakati madhubuti ya bodi yake ya kuhakikisha kuwa wanatumia mbinu
mbalimbali kupenya katika masoko mapya ili kuvutia wageni kutembelea
nchi yetu kwa shughuli za utalii na hivyo kuongeza pato la taifa.
Katika uzinduzi wa matangazo haya Timu ya Tanzania ilipata fursa ya
kuwa na banda maalum ambapo iliweza kutoa maelezo juu ya vivutio vya
utalii nchini kwa wageni mbali mbali waliofika kwa ajili ya kushuhudia
mchezo wa Chelsea na Seattle Sounders kwa kugawa vipeperushi
mbalimbali.