Dar es Salaam: TAARIFA KUHUSU UWEPO
WA DAWA BANDIA YA KUTIBU UGONJWA WA MALARIA IITWAYO ELOQUINE (Quinine Sulphate
300mg USP).
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ni wakala wa Serikali iliyo chini ya
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii yenye jukumu la kudhibiti ubora, ufanisi na
usalama wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya ya jamii.
TFDA inapenda kuutaarifu umma kuwa imebaini kuwepo kwa dawa bandia ya
kutibu ugonjwa wa Malaria katika soko. Dawa hiyo inaitwa Eloquine (Quinine Sulphate 300mg
U.S.P) na ipo katika makopo ya vidonge 1000 (elfu moja) kila moja. Maelezo
yaliyopo katika lebo yanaonesha kuwa
dawa hiyo imetengenezwa na kiwanda cha Elys Chemical Industries Ltd cha nchini
Kenya.
Hata hivyo, TFDA imebaini kuwa kiwanda cha Elys Chemical Industries Ltd
hakitengenezi dawa yenye jina la biashara la ‘ELOQUINE’. Kiwanda hicho
kimesajili Tanzania Quinine Sulphate 300mg B.P isiyo na jina la kibiashara. Aidha,
kiwanda cha Elys Chemical Industries Ltd kimebainisha tofauti mbalimbali
zilizopo katika lebo ya dawa bandia ikilinganishwa na dawa halisi
inayotengenezwa na kiwanda hicho iliyosajiliwa na TFDA na hivyo kuthibitisha
kuwa kiwanda hicho hakitengenezi dawa hiyo.
Katika kudhibiti usambazaji wa dawa hiyo hapa nchini, hadi sasa TFDA
imekamata jumla ya makopo 155 ya dawa hiyo bandia ya Eloquine jijini Dar Es
Salaam yaliyokuwa yakisubiri kusambazwa. Aidha, kopo moja lenye vidonge 115
limekamatwa Moshi, Kilimanjaro. Tayari mtuhumiwa mmoja amekwishafikishwa
mahakamani na upelelezi wa chanzo na wasambazaji wa dawa hii unaendelea kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Uchunguzi wa dawa bandia katika maabara umebaini kuwa vidonge hivyo havina kiambato hai (active ingredient) cha
Quinine Sulphate kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa Malaria na hivyo matumizi
yake ni hatari kwa afya ya binadamu.
Maelezo ya kina yanayotofautisha dawa halisi iliyosajiliwa na dawa
bandia ni kama yalivyoainishwa katika jedwali hapa chini.
Dawa
halisi iliyosajiliwa
·
Jina la
dawa: Quinine Sulphate 300mg B.P.
·
Jina la
biashara: Haina jina la biashara.
·
Mtengenezaji:
Elys Chemical Industries Ltd, Road B, Off Enterprise Road, P.O Box 40411, 00100 Nairobi, Kenya.
·
Rangi ya
Lebo: Nyeupe na kahawia (Brown).
·
Namba ya
toleo: Huanzia na namba na siyo herufi.
Kwa mfano: 2167E.
·
Muda wa
matumizi (Shelf life): Miaka 4.
Maelezo ya dawa bandia;· Jina la dawa: Quinine Sulphate 300mg U.S.P. · Jina la biashara: ELOQUINE. · Mtengenezaji: Elys Chemical Industries Ltd, Road B, Off Enterpises Road, P.O Box 4011 00100 Nairobi, Kenya. · Rangi la Lebo: Njano na Nyekundu. · Namba ya toleo: GE410. · Tarehe ya kutengenezwa: 04/2009. · Tarehe ya mwisho wa matumizi: 4/2014 (Miaka 5).
Wafanyabiashara wote wa dawa na wananchi wanatahadharishwa kutozitumia
dawa hizi na wale wote waliouziwa dawa hizi
wanaelekezwa kuzirudisha dawa hizo katika ofisi za TFDA, vituo vya afya vya
Serikali au vituo vya polisi vilivyo jirani nao.
TFDA inapenda pia kuwakumbusha wafanyabiashara wa dawa, wasafirishaji wa
vifurushi na wananchi kutoa taarifa
haraka iwezekanavyo pale wanapohisi kuuziwa dawa duni, bandia au zilizoisha
muda wa matumizi. Taarifa zitolewe ofisi za TFDA makao makuu zilizopo Barabara
ya Mandela, EPI Mabibo External, Dar es Salaam na Ofisi za Kanda zilizopo mtaa
wa Nkurumah, Mwanza, Mtaa wa Sakina – Arusha, Hosptali ya mkoa ya Dodoma na
Jengo la Ofisi ya Mifugo Mkoa wa Mbeya.
Kwa maelezo zaidi tafadhali wasiliana na:-
MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA
EPI MABIBO EXTERNAL,
S.L.P 77150, DAR ES SALAAM
Simu: +
255 222 450512/450751/452108
Nukushi: + 255 222 450793
Barua pepe: info@tfda.or.tz
Tovuti: www.tfda.or.tz